Habari

Uhuru awaruka Wakenya kuhusu ushuru nafuu

December 24th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatatu aliruka ahadi yake kwa Wakenya kuwa ushuru wa VAT ungesalia asilimia 14 hadi Juni 30 mwaka ujao.

Kwa kuweka saini Mswada wa Ushuru jana, Rais aliashiria kuwa ushuru huo utarudi asilimia 16 kuanzia Januari 1, 2021 kinyume na alivyokuwa ameahidi mnamo Septemba mwaka huu.

Hii ni baada ya wabunge mnamo Jumanne kupitisha Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Ushuru, unaolenga kuondoa afueni ya ushuru ambayo serikali iliwapa Wakenya mwezi Aprili kuwapunguzia makali ya kiuchumi yaliyosababishwa na janga la Covid-19.

Kenya bado haijafanikiwa kukabili kikamilifu virusi vya corona na maambukizi yanaendelea kuongezeka huku mapato ya makampuni na watu binafsi yakipungua.

Hatua ya wabunge na Rais Kenyatta inaipa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) idhini ya kurejesha kiwango cha ushuru wa ziada ya thamani (VAT) ya asilimia 16, badala ya asilimia 14 ambayo imekuwa ikitozwa tangu Aprili.

Hatua hii inashiria kuwa huku KRA ikiimarisha kiwango cha ukusanyaji ushuru, wafanyabiashara wataongeza bei ya bidhaa ili kuziba hasara itakayotokana na ongezeko hilo la ushuru; mzigo ambao utabebeshwa wanunuzi au watumiaji huduma.

Mafuta ya kupikia, umeme na salio la kuzungumza kwa simu (airtime) ni miongoni mwa bidhaa na huduma zitakazopanda bei.Nafuu ambayo waajiriwa walipata serikali ilipopunguza ushuru unaotozwa mishahara (PAYE) pia imeondolewa.

Inamaanisha kuwa asilimia 30 ya mishahara itakatwa na KRA kuanzia Januari 1; badala ya asilimia 25 ambayo imekuwa ikitozwa tangu Aprili ili kuwakinga dhidi ya makali ya Covid-19.

Mswada huo ambao uliwasilishwa bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha, Bi Gladys Wanga, pia umerejesha kiwango cha zamani cha ushuru unaotozwa kampuni (Corporate Tax); ambacho ni asilimia 30.

Katika afueni iliyotolewa na serikali mwezi Aprili, ushuru huo ulipunguzwa hadi kima cha asilimia 25.Hata hivyo, wafanyakazi wanaopokea mshahara wa Sh24,000 kwenda chini, wataendelea kufurahia afueni ya serikali kwani hawatatozwa ushuru wowote, kama ambavyo wamekuwa wakifurahia tangu Aprili.

“Lengo kuu la mswada huu sio kuumiza wananchi bali kuwasaidia kwa kuiwezesha serikali kuongeza mapato yake ili iweze kutoa huduma mbalimbali, ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi wa umma.

“Wafanyabiashara hawapasi kuongeza bei za bidhaa kwa sababu kimsingi viwango vya ushuru havijaongezwa. Kile mswada imefanya ni kurejesha viwango vya ushuru ambavyo vilikuwepo awali kabla ya afueni ya serikali,” alieleza Bi Wanga.

Lakini Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa alitofautiana na kauli hiyo akisema wafanyabiashara wataongeza bei za bidhaa za kimsingi haswa wakati kama huu wa sherehe za Krismasi.

“Wafanyabiashara huongozwa na uchu wa kutaka kuchuma faida. Nina hakika wataongeza bei kwa kisingizio kwamba KRA imeongeza ushuru wa VAT kutoka asilimia 14 hadi 16, ilhali hili sio jambo jipya,” akasema Bw Ichung’wa.

Mbunge huyo alihoji kuwa wafanyabiashara hawakupunguza bei kuendana na afueni ya serikali.Wabunge waliochangia mjadala kuhusu mswada huo waliuunga mkono wakisema itawezesha serikali kuongeza mapato yake na kuondoa hitaji la kukopa fedha. kutoka ng’ambo na katika mashirika ya kifedha ya humu nchini.

“Uchumi wa Kenya uko katika ICU na tukiondoa mpira wa hewa, utaporomoka kabisa. Mzigo wetu wa madeni umefikia Sh7 trilioni na kiwango hicho kinaendelea kupanda. Kwa hivyo, njia ya kipekee ya kuiwezesha serikali kupata pesa ni kuipa idhini ya kutoza viwango vya zamani vya ushuru,” akasema Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale.

Bw Duale ambaye ni kiongozi wa wengi wa zamani aliongeza kuwa hatua ya serikali ya kupunguza VAT, PAYE na ushuru kwa kampuni mnamo Aprili iliwafaidi wafanyabiashara na waajiri na wamiliki wa kampuni husuka wala sio raia wa kawaida.

Mbunge wa Emuhaya Omboki Milemba naye aliitaka serikali kutumia mapendekezo ya mswada huo kukusanya fedha za kupelekwa shuleni chini ya mpango wa elimu bila malipo, fedha za kugharamia mahitaji ya wahudumu wa afya waliogoma, fedha za mgao kwa serikali za kaunti na za kugharamia miradi ya hazina ya ustawi wa maeneo bunge (CDF).