Uhuru awasha upya moto mkali ngomeni mwake

Uhuru awasha upya moto mkali ngomeni mwake

Na MWANGI MUIRURI

MATAMSHI ya Rais Uhuru Kenyatta kwamba atatumia ushawishi wake kuhakikisha mahasimu wake Mlima Kenya hawaingii mamlakani, yamewasha moto upya katika ngome hiyo yake ya kisiasa.

Alipohutubu Jumamosi katika mkutano na wajumbe wa eneo hilo katika Ikulu ya Sagana, Kaunti ya Nyeri, aliwakashifu wandani wa Naibu wa Rais, Dkt William Ruto pamoja na wanaopinga mpango wa umoja wa kitaifa kupitia Muafaka wa Maridhiano (BBI) na kuwaonya kuhusu hatima yao ya kisiasa ifikapo 2022.

Seneta wa Tharaka Nithi, Prof Kithure Kindiki alimtaja rais kama asiye na shukran yoyote kwa waliojitolea kwa hali na mali kumshikilia hadi akapata urais.

“Mfano ni mimi ambapo baada ya kumfanyia kazi kwa kujitolea, nikawa hata wakili wake katika kesi yake ya ICC baada ya kuorodheshwa kama mshukiwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007, nikatumia taaluma na mali kumshikilia, ahsante yake iliishia kuwa ile ya punda,” akasema.

Prof Kindiki alisema, “Alinitoa kafara kwa genge la kisiasa la washirika wake wapya wa ODM katika Seneti na kwa masaa manne wakaning’atua kama kiongozi wa wengi, nikazomewa na kukumbushwa jinsi ya kumheshimu Uhuru Kenyatta.”

Katika kipindi cha wiki mbili sasa, Rais Kenyatta amewaangazia washirika wa Dkt Ruto kama wezi wa rasilimali za umma, matapeli wa kisiasa waliojawa na tamaa ya uongozi, kabla ya hatimaye kuzindua mpango mahsusi wa kupigia debe BBI Mlima Kenya ambapo leo hii anatamatisha ziara yake ya siku nne.

Rais amelenga kuimarishia udhibiti wa kisiasa katika Kaunti za Tharaka Nithi, Meru, Nyeri, Laikipia, Kirinyaga, Murang’a, Embu, Nyandarua, Nairobi na Nakuru zinazoorodheshwa kama ngome za jamii za Gikuyu, Embu na Meru (Gema.)Akiwa katika kikao na wajumbe 7, 000 katika ikulu ndogo ya Sagana, Jumamosi, rais alikanusha kuwa ashawahi kuwa na mkataba wa urithi wa urais na Dkt Ruto.

Jana, kinara wa Narc Kenya, Bi Martha Karua alimsuta Rais kama aliye na nia ya kuhadaa Wakenya kuwa BBI ina manufaa yoyote kwa taifa hili na pia kwa watu wa Mlima Kenya.

“Sisi si watoto na tuna uwezo wa kujiamulia. Akili tunazo za kujifanyia maamuzi yetu muhimu kuhusu masuala ya uongozi hasa 2022 na BBI. Ningemsihi awajibikie heshima tunayomwonyesha hadi sasa akihudumu awamu yake kama kiongozi na kisha aelekee nyumbani polepole akastarehe kama waliomtangulia,” akasema Bi Karua.

Bi Karua alikashifu BBI akisema kuwa imejaa sumu ya uongo na hadaa, lengo kuu likiwa ni kubomoa taasisi za kiutawala ili kuzigeuza kuwa butu na zisizo na nguvu za kuhudumia Wakenya kwa mujibu wa katiba.

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri ambaye pia ni kiongozi wa chama kipya cha The Service Party (TSP) alimshambulia rais kama aliye na mazoea ya kusukuma wengine pembeni huku akiwaharibia majina.

“Kile hatutakubali kama walio ndani ya mirengo mbadala ya kisiasa mbali na ule wa rais, ni atuhujumu kwa kutusukuma pembeni na hatimaye kutuharibia majina. Mfano wangu, alinifuta kazi na hadi leo hajawahi kutoa sababu za kufanya hivyo. Kisha, anaenda kwa mikutano akisema kwamba sikuafikia viwango vya utendakazi ilhali anajua vizuri alinifuta kwa msingi wa msimamo wangu wa kisiasa,” akateta Kiunjuri.

Akaongeza, “Akinishambulia, ajue hata mimi sitakuwa na lingine ila tu kujibu mipigo. Ajue kuwa akiendelea kiniharibia jina sitanyamaza huku nikimpa nafasi ya kunisambazia uoga na hofu ya kisiasa.”

Mbunge wa Mathira Bw Rigathi Gachagua alimtaka Rais aelewe kuwa “hakuna anayehitaji kupendekezwa na wewe ili awanie urais au aushinde na kisha aapishwe kukurithi.”

Bw Gachagua alisema kuwa wajibu huo wa kupendekeza, kuchagua na kuamua aapishwe ni wa raia wapiga kura “hivyo basi ukome kutusambazia vitisho”.

You can share this post!

Sina haja kulipwa deni 2022 – Ruto

Bodaboda wapiga teke punda Lamu