Uhuru awataka wawaniaji wakubali matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9

Uhuru awataka wawaniaji wakubali matokeo ya uchaguzi wa Agosti 9

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa wanasiasa wanaowania viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, mwaka huu kukubali matokea ili amani idumu nchini.

Akiongea Alhamisi, Mei 26, 2022, wakati wa Dhifa ya Maombi ya Kitaifa katika mkahawa wa Safari Park, Nairobi, rais pia amewataka Wakenya kudumisha umoja kabla, wakati na baada ya uchaguzi huo.

“Ni matumaini yangu kwamba tutamaliza uchaguzi tukidumisha umoja na nguvu. Lakini mkumbuke kuwa kutakuwa na mshindi mmoja pekee katika kila kiti. Ukishindwa, kubali matokeo na usubiri kujaribu tena wakati mwingine,” Rais Kenyatta akasema huku akishangiliwa na waliohudhuria kikao hicho.

Kiongozi wa taifa alitumia fursa hiyo kutakia kila la kheri wale wote wanaoshindania viti mbali mbali katika uchaguzi huo.

Awali, Naibu Rais William Ruto alitoa hakikisho kuwa yeye na mrengo wake wa Kenya Kwanza watafanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unaendeshwa katika mazingira ya amani.

“Kwa upande wangu na kundi langu tutakubali matokeo ambayo yatatangazwa kwa sababu Kenya ni kubwa kuliko kila mmoja wetu,” akasema.

Dkt Ruto pia alimtakia Rais Kenyatta amani na utulivu atakapostaafu baada ya kukamilisha muhula wake wa pili na wa mwisho kama rais wa Kenya.

“Hata hivyo, ikiwa kwa njia moja ama nyingine sikutekeleza mambo fulani kulingana na matarajio ya Rais, ninaomba anisamehe. Na wale wote ambao walinikosea kwa namna fulani, nimewasamehe,” akasema.

Wengine waliozungumza katika halfa hiyo ya maombi ya kitaifa ni mgombea mwenza wa mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Raila Odinga, Martha Karua, Jaji Mkuu Martha Koome na Maspika Justin Muturi (Bunge la Kitaifa) na Kenneth Lusaka (Seneti).

  • Tags

You can share this post!

Kilimo: Wanafunzi 20 wa UoN wanufaika na mpango wa mafunzo...

Liverpool wamsajili kinda matata wa Fabio Carvalho kutoka...

T L