Habari Mseto

Uhuru awazomea wanasiasa ‘wapiga domo’

December 31st, 2019 1 min read

Na MARY WANGARI

MWANASIASA mkongwe Chares Rubia alizikwa Jumatatu nyumbani kwake Kandara, Kaunti ya Murang’a, katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Akimwomboleza marehemu aliyekuwa meya wa kwanza Mwafrika kuongoza Nairobi, Kiongozi wa Taifa alimtaja mwanasiasa huyo kama nguzo muhimu ya mfumo wa kidemokrasia.

“Kama Meya wa kwanza Mwafrika, Rubia alikuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya jiji la Nairobi na kulifanya kitovu cha uchumi kwa Afrika Mashariki na ya Kati.

“Ni katika hatamu yake kama baba wa jiji ambapo Nairobi ilipata lakabu ya jiji la kijani kibichi juani, kutokana na juhudi zake za kudumisha usafi na mpangilio jijini,” alisema Rais.

Wakati uo huo, Rais Kenyatta aliwashutumu baadhi ya wanasiasa wanaolaumu serikali kwa kutumia vibaya raslimali za kitaifa kuwatishia viongozi wanaoegemea misimamo fulani ya kisiasa.

Uhuru wa kujieleza

Rais aliyekuwa akijibu matamshi ya Mbunge wa Kandara Alice Wahome aliyemhimiza kulinda uhuru uliopiganiwa na viongozi waliotangulia, aliwakashifu wanasiasa wanaotumia vibaya uhuru wa kujieleza.

“Tumehifadhi na kulinda uhuru huo, hakuna aliyekatazwa kuzungumza hata kutoka kwenye paa kwa sauti kubwa lakini ni viongozi wanaotumia vibaya uhuru huo kwa kukosa kuutumia kusambaza amani, umoja na kukomesha ufisadi.”

“Hiyo ndiyo njia bora zaidi ya kulinda uhuru huo wala si matamshi kiholela maadamu hayo hayatasaidia katika kukomesha ufukara, ufisadi, ukosefu wa ajira na masaibu ya majani chai. Tutumie uhuru huo kujadili masuala yatakayoboresha maisha ya mwananchi wa kawaida,” alisema Bw Kenyatta akizungumza katika shule ya msingi ya Kariguini.

Aidha, katika juhudi za kudhihirisha jinsi usimamizi wake ulivyojitolea kulinda demokrasia na uhuru wa kujieleza, rais alifichua, japo si moja kwa moja, kwamba mkosoaji wake mkuu, Bw Miguna Miguna alikuwa huru kurejea nchini na kuendelea kutumia uhuru wake wa kujieleza.