Habari Mseto

Uhuru azima pensheni ya wabunge wa zamani

September 10th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MATUMAINI ya wabunge wa zamani waliohudumu kati ya miaka ya 1984 na 2001 ya kufurahia pensheni ya Sh100,000 kila mmoja kila mwezi sasa yamezimwa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukataa kutia saini mswada uliopendekeza walipwe pesa hizo.

Rais Kenyatta Alhamisi aliurejesha bungeni mswada huo na maelezo ya kuwataka wabunge waondoe kipengele kinachopendekeza pensheni hiyo akisema “haiwezekani kisheria”.

Alisema pensheni hiyo itagharimu mlipa ushuru Sh450 milioni kila mwaka, na itachochea makundi mengine ya wafanyakazi wa umma kuitisha nyongeza ya malipo hayo ya kustaafu ambayo serikali haiwezi kumudu.

“Mswada huo pia unakiuka wajibu wa Tume ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu ya Watumishi wa Umma (SRC) ambayo miongoni mwa majukumu yake ni kukadiria mishahara na pensheni ya watumishi wa umma,” Rais Kenyatta akasema kwenye memoranda iliyowasilishwa bungeni na Spika Justin Muturi.

“Pensheni ya Maafisa wa Serikali, wakiwemo wabunge, hukadiriwa kulingana na kiwango cha mchango katika hazina maalum. Lakini mswada huu haujajumuisha hitaji hili muhimu,” akaongeza.

Mswada huo wa marekebisho ya sheria ya pensheni ya wabunge ulidhaminiwa na Kiongozi wa Wachache John Mbadi na ukapitishwa na wabunge mnamo Agosti 5, 2020, kisha ukawasilishwa kwa Rais Kenyatta.

Ulipendekeza kuwa jumla ya wabunge 290 waliostaafu kati ya 1984 na 2001 walipwe Sh100,000 kila mwezi kuanzia Julai 1, 2010. Hii ilimaanisha kuwa kila mmoja wao angepokea malimbikizo ya karibu Sh11 milioni endapo Rais angetia saini mswada huo.

Akitetea mswada huo Bw Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini alisema hivi: “Ni aibu kuwa wenzetu waliotumikia taifa hili kwa taadhima kama wabunge sasa wanaishi maisha ya ukata kwani baadhi yao hupokea malipo ya Sh7,000 pekee. Malipo ya Sh100,000 kila mwezi yanalenga kuhakikisha wanisha maisha ya heshima.”

Ili kubatilisha pendekezo la Rais Kenyatta, Bw Mbadi sasa atahitaji uungwaji mkono kutoka jumla ya wabunge 233 kati ya 349 kulingana na hitaji la kipengee cha 115 cha Katiba. Idadi hii ni sawa na thuluthi mbili ya idadi jumla ya wabunge.

Huenda ikawa vigumu kwa idadi hii ya wabunge kufikiwa ikizingatiwa kuwa wabunge wamegawanyika kwa misingi ya mirengo ya ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’.