Habari Mseto

Uhuru azindua kampeni ya uboreshaji wa mazingira Nairobi

August 14th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amezindua kampeni ya kurejesha hadhi ya Jiji la Nairobi kupitia uhifadhi wa mazingira; hatua ambayo amesema ni mwamko mpya jijini.

Akizungumza Ijumaa katika Bustani ya Kumbukumbu ya John Michuki karibu na mzunguko wa Globe, alisema kampeni ambayo iko katika awamu ya majaribio ni sehemu ya mpango wa Serikali Kuu ya kudumisha usafi kote nchini.

Mpango huo pia unahusisha upanzi wa miti kama hatua ya kuboreshwa kwa mazingira.

Mpango huo utazinduliwa rasmi Septemba 1, 2020, na utaongozwa na Wizara ya Usalama wa Ndani pamoja na ile ya Mazingira.

Maafisa wa utawala kama vile machifu na manaibu wao watahakikisha kuwa mpango huo unafanikishwa katika ngazi za mashinani.

“Mpango huo utaendeshwa na kusimamiwa na machifu wetu kwa ushirikiano na maafisa wa serikali kuu na zile za kaunti, pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali,” akasema Rais Kenyatta.

Alitoa onyo kali kwa machifu na maafisa wengine wa serikali watakaozembea katika utekelezaji wa kampeni hiyo, serikali yake haitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu.

“Na watakaofanya vyema katika mpango huo watazawidiwa huku wazembe wakiwajibikia makosa yao,” Rais Kenyatta akasema.

Akaeleza: “Na ieleweke kuwa kampeni hii inatekelezwa sambamba na mpango wa Kazi Mtaani ambao tayari umeingia awamu ya pili katika kaunti zote 47.”

Miongoni mwa maeneo yaliyolengwa kwa kuboreshwa chini ya mpango huo ni pamoja na Nairobi Arboretum, Msitu wa Karura, Central Park, Uhuru Park, Msitu wa Ngong’ miongoni mwa sehemu nyinginezo.