MakalaSiasa

UHURU KENYATTA: Rais wa vitisho bila kung'ata

February 4th, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

KWA mara nyingine, Rais Uhuru Kenyatta Alhamisi alitishia kuwafuta kazi mawaziri wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao au kushiriki siasa, suala lililoacha Wakenya wakishangaa ni nini kinachomzuia Rais kuwatimua wale wanaokaidi maagizo yake na wanaozembea kazini.

Tangu mwaka 2018, Rais Kenyatta amekuwa akiwaonya tu mawaziri kutekeleza majukumu yao au waache kazi, jambo linalofanya Wakenya kujiuliza kwa nini anawavumilia akijua kwamba wameshindwa na kazi.

Kulingana na baadhi ya viongozi wa chama cha Jubilee, Rais Kenyatta anafaa kuwachukulia hatua mawaziri badala ya kuwaonya kila mara.

Mbunge wa Kieni, Bw Kanini Kega, jana alimtaka rais kuwatimua mawaziri wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao badala ya kuwaonya tu.

“Wakati wa kutekeleza ahadi za chama cha Jubilee unayoyoma na kuna haja ya kuwa na mawaziri wanaoweza kufanya kazi,” alisema Bw Kega.

Akihutubia wakazi wa mji wa Kitengelea, Kajiado, Alhamisi alasiri alipokuwa njiani kuelekea Arusha, Rais Kenyatta alisema mawaziri wanafaa kutumikia Wakenya au kuacha kazi.

“Leo nimekutana na mawaziri. Niliwaambia kuwa ni lazima wachague ikiwa wanataka siasa au kufanyia wananchi kazi. Niliwaambia niko na vijana wengi wanaoweza kufanya kazi yao,” alisema Rais Kenyatta.

Katika mkutano huo, inasemekana rais aliwaambia mawaziri washirikiane na waziri wa usalama Dkt Fred Matiang’i aliyeteuliwa kushirikisha shughuli za maendeleo katika kila wizara au waache kazi.

Kulingana na mdadisi wa siasa Martin Andati, matamshi ya Rais Kenyatta yalikuwa ya kuwaandaa mawaziri kwa mabadiliko.

“Kimsingi, kile kiongozi wa taifa alikuwa akiwaambia Wakenya ni; mkisikia nimefuta kazi waziri huyo au yule, ni kwa sababu wamenikaidi kwa kuendelea kuchapa siasa badala ya kulenga ajenda ya maendeleo yenye manufaa kwao,” akasema Bw Andati.

Pili, kulingana na mchanganuzi huyo, Rais alikuwa akiandaa umma kwa mabadiliko ambayo anapanga kufanya hivi karibuni katika baraza lake la mawaziri, haswa, kwa kuwafuta baadhi yao.

Mdadisi wa siasa, Bw Jarvis Bigambo anasema kuwa Rais Kenyatta alionekana kama kiongozi aliyechoshwa na ukaidi wa mawaziri, akiwemo Naibu wake William Ruto, ndiposa akaamua kuwakemea hadharani mbele ya umma, ishara ya kujiondola lawamani endapo atawaadhibu.

“Matamshi yake kule Kitengela yalikuwa ni onyo la mwisho kwa Bw Ruto, mawaziri watepetevu kazini na wale ambao wamekuwa wakiendeleza siasa za 2022. Alikuwa akiwaambia Wakenya wasimlaumu endapo ataadhibu baadhi yao,” anasema.

Tangu mwaka jana, Rais Kenyatta amekuwa akiwaonya mawaziri kutekeleza majukumu yao au waache kazi jambo linalofanya Wakenya kujiuliza kwa nini anawavumilia akijua kwamba wameshindwa na kazi. Kulingana na mwanaharakati Ndung’u Wainaina, Rais Kenyatta anafaa kuwachukulia hatua mawaziri badala ya kuwaonya kila mara.

“Anafaa kuchukua uamuzi badala ya kulalamika. Anajua wazi kuwa mawaziri wake wameshindwa na kazi na kuwavumilia kunaonyesha kuna kitu kinachomzuia au si mwepesi wa kufanya maamuzi,” alisema.

Mnamo Oktoba 20 akiwa Kakamega kuongoza sherehe za Mashujaa Dei, Rais alimuonya waziri wa kilimo Mwangi Kiunjuri kuwasaka waliopora fedha za wakuzaji mahindi na miwa.

Akionekana kuwa mkali, alimweleza Bw Kiunjuri kwamba, hafai kuchukulia suala hilo kimzaha. Alimwambia aamue kuwasaka waliohusika au abebe msalaba wao mwenyewe.

Matamshi anayotoa hadharani kuhusu mawaziri wake yanamsawiri kama aliyekosa imani nao. Hata hivyo, kinachomfanya akose kuwachukulia hatua ni fumbo kwa Wakenya.

Mwaka 2018 akiwa Mombasa kuzindua kamati ya biashara ya baharini, Rais alieleza kwamba alilazimika kumteua mkuu wa majeshi Jenerali Samson Mwathethe kusimamia shughuli hiyo kwa sababu alifahamu mawaziri wake hawangeweza kuifanikisha.

“Tunaambiwa kwamba ni jambo gumu sana. Nilianza kazi hii na (Jenerali Samson) Mwathethe. Nilimwambia ninataka anisaidie na kazi hii kwa sababu nilijua nikitumia mawaziri nitaambiwa inagharimu mabilioni,” alisema Rais Kenyatta.

Mnamo Aprili mwaka jana, Rais Kenyatta alisema baadhi ya mawaziri wanapenda kuonekana katika runinga na magazeti lakini hawakuwa wakihudumia Wakenya.