Uhuru kuacha raia katika kona mbaya

Uhuru kuacha raia katika kona mbaya

NA PETER MBURU

RAIS Uhuru Kenyatta atakapoondoka madarakani mwezi ujao – Agosti – atamuacha Mkenya wa kawaida katika hali mbaya zaidi kiuchumi kuliko alivyokuwa alipopokea madaraka kutoka kwa marehemu Mwai Kibaki mnamo 2013.

Ushahidi wa kuzorota kwa maisha ya Mkenya katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wa Rais Kenyatta ni kupanda kwa bei za bidhaa kiasi cha wananchi wengi kushindwa kununua bidhaa za kimsingi hasa chakula, kumudu matibabu na karo ya wana wao.

Utafiti wa Taifa Leo unaonyesha kuwa gharama ya bidhaa zinazotegemewa katika maisha ya kila siku imekuwa ikipanda tangu 2013 kwa kati ya asilimia 30 na 124 ikilinganishwa na wakati wa uongozi wa Mzee Kibaki.

Watengenezaji bidhaa wanalaumu ushuru wa juu na mazingira magumu ya kibiashara kama sababu kuu za kupanda kwa gharama ya maisha chini ya utawala wa Rais Kenyatta.

Kupanda huko kwa bei za bidhaa kumewaacha wananchi wakitumia pesa nyingi zaidi hasa katika kununua chakula, na wataalamu wa uchumi sasa wameanza kuonya kuhusu uwezekano wa wananchi wa tabaka la chini kulemewa kabisa kimaisha.

Baadhi ya bidhaa ambazo bei zake zimepanda zaidi ni vyakula, petroli ambayo hutegemewa katika sekta zote za kiuchumi na bidhaa za ujenzi ambazo zimekuwa zikitumika zaidi.

Kulingana na watengenezaji bidhaa humu nchini, kupanda kwa bei za bidhaa hizi kumetokana na hali ya serikali kupandisha ushuru ambao zinatozwa, hali inayoziacha zikigharimu kiwango cha juu zaidi na ugumu wa kufanya biashara na kwa katika siku za majuzi misukosuko ya kiuchumi ambayo imeshuhudiwa ulimwenguni.

“Kama taifa, tunakumbana na nyakati ngumu kutokana na masuala ya hapa nchini na ya ulimwengu na uvumilivu wetu unaelekea kufika mwisho. Kwa miaka mitatu ambayo imepita, tumeona bei za bidhaa muhimu zikipanda kupindukia, huku uwezo wa wananchi kuzinunua ukipungua, hali inayofanya vigumu zaidi wananchi kuweka chakula mezani,” anasema Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Muungano wa Watengenezaji Bidhaa (KAM), Tobias Alando.

Watengenezaji bidhaa wanalaumu serikali kwa kulimbikizia bidhaa zinazotengenezwa humu nchini na zinazoagizwa kutoka nje ushuru wa juu, ambao matokeo yake yamekuwa kupanda kwa bei kwa viwango vinavyopita uwezo wa wananchi.

Kiongozi wa muungano wa wafanyakazi wa Cotu Francis Atwoli wiki iliyopita alisema kuwa pesa wanazolipwa wafanyakazi sasa ni za chini sana kuweza kukimu mahitaji ya sasa kutokana na jinsi bei za bidhaa zimepanda, akisema kuwa muungano huo unapanga kuzungumza na serikali itakayoingia mamlakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, kuona kuwa mshahara wa chini zaidi unaongezwa na serikali.

“Tutaketi kutafuta suluhu ya kudumu kuhusu masuala ya bidhaa muhimu na kulinda mapato ya wafanyakazi. Mazungumzo hayo pia yatahusu uongezaji wa kiwango cha chini zaidi cha mishahara nchini ili kutilia maanani kupanda kwa gharama ya maisha,” Bw Atwoli akasema.

Kwa mfano, kilo mbili za unga wa ugali ambao uligharimu Sh109 Machi 2013, mwezi mmoja kabla ya Kibaki kuondoka sasa umepanda kufikia wastan wa Sh210 madukani, ikiashiria ongezeko la asilimia 92.7.

Unga wa ngano ambao uligharimu Sh138 Rais Kibaki alipokuwa akiondoka sasa unagharimu wastani wa Sh208 madukani baada ya gharama yake kupanda kwa asilimia 50.7, huku nusu lita ya maziwa ya pakiti yaliyouzwa Sh39 mnamo Machi 2013, sasa yakiuzwa hadi Sh70.

Kilo moja ya mboga za sukuma wiki ambazo hutegemewa kila siku na familia kuandamana na lishe aina mbali mbali zilikuwa zikiuzwa Sh39 miaka kumi iliyopita, lakini sasa zinauzwa Sh60, ongezeko ambalo limeacha familia nyingi hasa zisizo na uwezo mkubwa kifedha zikiteseka kupata mlo.

Hii ni licha ya kuwa kando na bidhaa za vyakula, bei za bidhaa nyingine kama sabuni pia zimepanda kwa viwango vikubwa miaka ya majuzi huku sabuni ya kipande, ambayo iligharimu takriban Sh85 mnamo 2013 sasa ikigharimu hadi Sh191, ongezeko la asilimia 124.7.

Bei ya mafuta taa, ambayo hutumiwa na wananchi wengi wasio na uwezo wa kifedha kwa mapishi, imepanda kutoka Sh88.01 mnamo Machi 2013 hadi Sh128.86 sasa, ongezeko la asilimia 46.

Bei za dizeli na petroli, ambayo matumizi yake ni mengi kiuchumi katika usafiri wa watu, bidhaa na viwandani zimepanda kwa asilimia 36.1 (petroli) na 30.1 (dizeli), ongezeko ambalo linaathiri bei za bidhaa nyingine kote katika uchumi wa taifa.

  • Tags

You can share this post!

Ulimwengu kuadhimisha Siku ya Kiswahili kesho Alhamisi

BI TAIFA JULAI 06, 2022

T L