Habari Mseto

Uhuru kuenda Ufaransa kusaka wawekezaji

January 23rd, 2020 1 min read

Na NYAMBEGA GISESA

Baada ya kuhudhuria kongamano la uwezekezaji kati ya Afrika na Uingereza, Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kurudi Ulaya baadaye mwezi huu kuhudhuria kongamano la kihistoria la uwekezaji kati ya Afrika na Ufaransa.

Kongamano hilo litafanyika Ufaransa huku mipango ikiendelea ya mkutano kati ya Ufaransa na Afrika kufanyika Afrika Kusini mwezi Juni mwaka huu.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amewaalika marais 54 wa mataifa ya Afrika kuhudhuria kongamano hilo hapo Januari 31.

Jana, msemaji wa Ikulu Kanze Dena aliambia Taifa Leo kwamba hajafahamishwa iwapo Rais Kenyata atasafiri kwenda Ufaransa.

Mikutano ya uwekezaji katika mataifa ya Uingereza na Ufaransa inajiri baada ya iliyofaulu nchini Urusi na Uchina kati ya nchi hizo na mataifa ya Afrika.

Ni marais 16 waliohudhuria kongamano la Uingereza ikilinganishwa na 43 walioitikia mwaliko wa Urusi mwaka jana na 51 waliohudhuria kongamano kati ya China na Afrika maarafu kama Forum on China-Africa Cooperation (FOCAC).

Kabla ya kuhudhuria kongamano China, Rais Kenyatta alikuwa amekutana na Rais wa Amerika Donald Trump jijini Washington.

Akiwa Amerika, Rais Kenyatta alikutana na wawekezaji wa nchi hiyo.

Kongamano la kwanza la uwekezaji kati ya Afrika na Uingereza jijini London lilikuwa la kuzima umaarufu wa Amerika na China, ambazo zimekuwa zikiipa Afrika misaada ya kifedha miaka ya hivi majuzi.

China hasa imekuwa ikipiku Amerika na mataifa ya Ulaya kama mshirika mkuu wa kibiashara wa Afrika. Kwa wakati huu, China ndiyo iliyo na uchumi mkubwa baada ya Amerika na iliuza bidhaa za Sh390.62 bilion Afrika mwaka wa 2017.

ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.75 kutoka Sh337.46 bilioni mwaka wa 2016.

China inaongoza kwa nchi zilizokopesha Kenya pesa nyingi ikiwa ya pili nyuma ya benki ya dunia.

Mnamo mwaka wa 2013, China ilikopesha Kenya Sh500 bilioni nyingi ambazo zilitumiwa kujenga reli ya kisasa ya SGR kutoka Mombasa hadi Nairobi.