Uhuru mbioni kuwapatanisha Raila, Museveni

Uhuru mbioni kuwapatanisha Raila, Museveni

Na AGGREY MUTAMBO

NAIROBI, KENYA

IMEBAINIKA kuwa Rais Uhuru Kenyatta ameanza mchakato wa kuwapatanisha Rais wa Uganda Yoweri Museveni na Kinara wa ODM Raila Odinga huku akilenga kuhakikisha wawili hao wanaridhiana kabla hajaondoka afisini Agosti 2022.

Wiki hii, Rais Kenyatta kwa mara nyingine alikuwa mwenyeji wa mwanawe Museveni, Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, wawili hao wakikagua miradi ambayo inalenga kukuza zaidi uhusiano kati ya Kenya na Uganda.

Jenerali Kainerugaba ni kamanda wa jeshi la ardhi la Uganda (UPDF) na anaonekana kama mrithi wa Rais Museveni katika siasa za taifa hilo jirani iwapo mkongwe huyo ataamua kustaafu siasa.

“Rais anataka urafiki ambao umekuwepo kati yake na Rais Museveni uendelee hata baada ya kuondoka mamlakani na uongozi kukabidhiwa mtu mwengine,” afisa mmoja wa ngazi ya juu serikali alieleza Taifa Leo huku akiweka wazi kuwa uhusiano kati ya Rais Museveni na Bw Odinga umekuwa wa vuguvugu.

Bw Odinga kwa sasa yupo kwenye ushirikiano wa kufana na Rais Kenyatta na inaaminika kuwa anaungwa mkono na serikali ili achukue hatamu za uongozi 2022.

Ingawa Rais Museveni na Bw Odinga walikuwa marafiki wa karibu miaka ya nyuma na hata waziri huyo mkuu wa zamani alimfanyia kampeni mnamo 2011, wawili hao wanaonekana kutalikiana tena kisiasa, kiongozi huyo wa Uganda akionekana anaegemea upande wa Naibu Rais Dkt William Ruto.

Dkt Ruto pia analenga kiti cha Urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.Rais Museveni na Dkt Ruto ni washirika wakubwa wa kibiashara na Naibu Rais amekuwa nchini Uganda mara nyingi akikutana na kiongozi huyo.

“Ni vyema kwa Rais Kenyatta kuhakikisha kuwa Uganda na Kenya zinaendeleza ushirikiano wa karibu hata baada ya uchaguzi mkuu mnamo Agosti. Kuna majadiliano yanayoendelea ili anayeungwa mkono na Rais Kenyatta halipizi kisasi dhidi ya utawala wa Rais Museveni akichukua uongozi,” akasema afisa huyo ambaye hakutaka anukuliwe kwa kuwa hana ruhusa ya kuzungumzia siasa za Uganda na Kenya.

Mnamo Jumanne, Rais Kenyatta na Luteni Jenerali Kainerugaba walitembelea bandari kavu ya mizigo ya Naivasha, bandari ya Kisumu na daraja la Mbita huku wakionekana kumakinikia reli ya sasa ya SGR kujengwa hadi mpakani Malaba kurahisisha usafirishaji wa mizigo.

Iwapo hilo litatimia basi Uganda na Kenya zitapata nafuu kibiashara kutokana na urahisi katika kusafirisha mizigo.

“Namshukuru ndugu yangu mkubwa Rais Kenyatta kwa kunialika Kenya ili kujiunga naye kuzindua bandari kavu ya Naivasha. Kenya ni kama nyumbani na uhusiano imara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ni jambo la kukumbatiwa na kuenziwa,” akaandika Jenerali Kainerugaba kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Hii si mara ya kwanza kwa Rais Kenyatta na Luteni Jenerali Kainerugaba, 47 kukutana.

Mnamo Oktoba 2021, mwana huyo wa Rais Museveni alitembelea ikulu huku akitundika picha kwenye ukurasa wake wa Twitter zilizoonyesha wawili hao wakiwa wamefurahi huku wakipiga gumzo.

Mkuu huyo wa jeshi bado hajatangaza kujitosa kwenye siasa na wadhifa anaolenga kama tu babake ambaye hajatangaza atastaafu siasa lini na kuachia mwengine uongozi wa Uganda ambao ameshikilia kwa miaka mingi.

  • Tags

You can share this post!

Pigo kwa Obado korti ikikataa kesi dhidi yake kusikilizwa...

Mnangagwa aachia naibu wake mamlaka akianza likizo ya siku...

T L