HabariHabari MsetoSiasa

Uhuru kusherehekea Idd na Joho Mombasa

June 13th, 2018 3 min read

MOHAMED AHMED NA KAZUNGU SAMUEL

RAIS Uhuru Kenyatta anatazamiwa kukutana na hasimu wake wa kisiasa Gavana Hassan Joho katika sherehe za Idd-Ul-Fitr kisha wazindue miradi kadhaa ya maendeleo pamoja.

Wawili hao ambao wamekuwa hawali chungu kimoja kwa muda wanatazamiwa kukutana kesho (Alhamisi) wakati Bw Kenyatta atakuwa jijini humo kwa ajili ya ufunguzi wa barabara ya kisasa ya Dongo Kundu.

Licha ya Bw Joho kuwa nchini Makkah kwa ajili ya ibada ya Umrah, kwa kawaida ifikapo Ramadhan ya 29 huwa amerudi jijini Mombasa kwa ajili ya sherehe za Eid.

Msemaji wa kaunti ya Mombasa, Richard Chacha alisema: “Hatuna uhakika kuhusu mipango ya gavana kwa sababu ya ibada zake lakini amesema kuwa kwa sababu ya mwafaka wa salamu ya Bw Kenyatta na Raila Odinga basi atamkaribisha rais akiwa atazuru eneo hili,”akasema Bw Chacha.

Mwezi Mei wakati alipokuwa amekutana na Seneta wa Baringo Gideon Moi alipokuwa amemtembelea afisini mwake, Bw Joho alisema kuwa anatamani kuona Bw Kenyatta anatembelea kaunti hiyo.

Alisema kuwa hapo awali amekuwa na shauku na safari za Bw Kenyatta katika kanda akaongeza “Lakini sasa tunatazamia ziara zake katika kaunti yetu kwa sababu muungano uliopo ni wakuungananisha Wakenya,”

Bw Joho amekuwa akimkashifu Rais Kenyatta na uongozi wake kwa muda na kumkosoa kwa cheche za maneno.

Baada ya uhasama wao kuzidi , Rais Kenyatta alifikia hatua ya kumfungia Bw Joho dhidi ya kwenda katika mikutano yake wakati anapozuru Pwani.

Aidha, kwanzia kuungana kwa Bw Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, Bw Joho ameonekana kupunguza kumuandama Rais.

Jana, matayarisho kabambe yalikuwa yanaendelezwa katika eneo la Miritini ambapo Rais Kenyatta atazuru kufungua rasmi barabara hiyo.

Katibu wa wizara ya usafiri Chris Obure alithibitisha ziara ya Rais Kenyatta siku ya Alhamisi.

Hapo jana, wahandisi wakiwemo mwanakandarasi aliyepatiwa kazi ya ujenzi wa barabara hiyo ya kilomita kumi waliendelea kumalizia kuipamba barabara hiyo ambayo iligharimu kitita cha Sh11 billioni.

 

Matayarisho yako shwari 

“Kila kitu kiko shwari na mikakati kabambe tumeweka kuhakikisha kwamba Rais anafungua barabara hiyo. Ilianza kutumika rasmi kwa umma mapema wiki iliyipipta,” akasema afisa mmoja wa barabara ambaye hakutaka atambuliwe.

Katika eneo ambalo Rais atalitumia kuzindua rasmi barabara hiyo, trakta zilionekana kumwaga michanga na kusawazisha eneo kutakapojengwa majukwa kwa ajili ya hafla hiyo.

Wanakadnarasi walionekana mara kwa mara wakirudia barabara hiyo wakichora alama za barabara, huku vibarua wakiendelea kuondoa takataka zilizokuwa zimebaki barabarani.

Matumaini ni mengi kwamba barabara hiyo sasa itaimarisha usafiri wa kutoka na kuingia jijini Mombasa ambao ulikuwa umekuwa ukikumbwa na msongamano kila mara.

Jiji la Mombasa ndio lango la kuingia nchi kwa njia ya usafiri wa baharini na ni mojawapo ya miji yenye rasmali kubwa zinazoiletea Kenya mabilioni ya pesa ikiwemo bandari ya Mombasa ambsayo inasimamiwa na halmshauri ya bandari nchini (KPA).

Naibu wa Rais Bw William Ruto alitangaza wakati wa ziara yake katika eneo la Pwani kwamba Rais Uhuru Kenyatta atafungua rasmi barabara hiyo ya umbali wa kilomita kumi.

 

Kufungua barabara ya Dongo Kundu 

“Wiki hii siku ya Alhamisi, Rais Uhuru Kenyatta atafungua rasmi barabara ya Dongo Kundu ambayo imekamilika. Baadaye sote tunajua kwamba barabara hiyo ya Dongo Kundu pia itatufikisha hadi katika kaunti ya Kwale. Haya yote yakikamilika, tunaamini Mombasa itakuwa imepiga hatua kubwa kimaendeleo,” akasema.

Hamlshauri uya barabara kuu nchini(KeNHA) inayomsimamia na mkurugneiz mkuu Peter Mundinia ilifungua rami barabara hiyo kwa matumizi ya umma wiki iliyopita.

Naibu afisa mkuu wa mawasiliano wa KeNHA Bw Charles Njogu alisema kuwa barabara hiyo inatarajiwa kupunguza kwa kiwango kikubwa msongamano katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi.

Ujenzi wa barabara hiyo ulianza mwaka wa 2016 na ulianzia katika eneo la pili la egesho la bandari ya Mombasa hadi eneo la Bonje karibu na mji wa Mazeras.

“Hii ni hatua kubwa kwa sababu barabara hiyo itafugnua upande wa Kusini na Kaskazini hivyo basi kurahisisha usafiri bila taabu yoyote,” akasema Bw Njogu.

Awamu ya pili ya ujenzi wa barabara hiyo inatarajiwa kugharimu kitita cha Sh30 billioni.

Utakuwa ni ujenzi wa barabara ya kilomita 8.9 kati ya eneo la Mwache na Mteza. Kisha kutakuwa na ujenzi wa madaraja katika kijiji cha Mwache na daraja lengine katika kijiji cha Mteza.