Habari Mseto

Uhuru kuteua makamishna wapya wa NCIC

November 16th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta, Jumatatu anatarajiwa kuwateua rasmi watu wanane waliopigwa msasa hivi majuzi kuchukua nafasi za wanachama wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC).

Hii ni baada ya bunge la kitaifa Alhamisi jioni kuidhinisha ripoti ya Kamati ya Uwiano na Usawa iliyoidhinisha majina ya wateule hao wakiongozwa na Samuel Kobia aliyependekezwa kuwa mwenyekiti wa tume hiyo.

Wale ambao waliidhinishwa kushikilia nafasi za wanachama wa kamati hiyo ni wabunge wa zamani Philip Okundi (Rangwe), Abdulaziz Farah (Mandera Mashariki) na Dorcas Kedogo (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Vihiga).

Wengine ni; Danvas Makori, Bi Peris Nyutu, Fatuma Tabwara na aliyekuwa mwenyekiti wa Bodi ya wasimamizi wa Mamlaka ya Ustawishaji wa Eneo la Kerio (KVDA) Samuel Kona.

Kasisi Kobia na wenzake watachukua mahala pa Francis Ole Kaparo na wenzake ambao muda wao wa kuhudumu ulikamilika mapema mwaka 2019.

Ripoti iliyowasilishwa bunge na mwenyekiti wa kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge Maalum Maina Kamanda inasema hivi: Baada ya kuendesha vikao vya kuwachunguza watu hawa tisa waliopendekezwa kujaza nafasi za mwenyekiti na makamishna wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) kamati imeridhishwa kwamba wamehitimu kwa nafasi hizo na inapendekeza kwamba bunge liidhinishe uteuzi wao.”

Wakati wa mjadala kuhusu ripoti hiyo, wabunge walitaka wanachama hao wapya kupambana na uhasama wa kikabila unaoshamiri nchini hasa kutokana na majibizano miongoni mwa wanasiasa baada ya kukamilishwa kwa uchaguzi mdogo wa Kibra.

“Nataka kuwaambia makamishna hawa wapya kwamba kazi kubwa inayowasubiri sasa ni kupambana na wanasiasa wanaotoa matamshi ya chuki hasa baada ya uchaguzi mdogo wa Kibra. Na wale wanaochochea uhasama katika maeneo mengine kote nchini pia wanapasa kuchukuliwa hatua kali,” akasema kiongozi wa wengi Aden Duale.

“Tunamtaka Kasisi Kobia na wenzake kurejesha utulivu na amani nchini. Tume inayoondoka ilishindwa kutekeleza wajibu huu,” akaongeza kiongozi wa wachache John Mbadi.

Wito wa ndimi kudhibiti kauli

Wawili hao walitoa wito kwa wanasiasa wanzao kudhibiti ndimi zao na kukoma kutoa matamshi ya kuchochea chuki.

“Sisi kama viongozi tunafaa kuchuja yale tunayoyanena hasa katika majukwaa ya kisiasa. Tusichochea vita, uhasama na mapigano baina ya Wakenya ambao tunawawakilisha,” akasema Duale ambaye pia ni Mbunge wa Garissa Mjini.

Bw Mbadi ambaye ni mbunge wa Suba Kusini alisema inasikutisha kuwa viongozi wanawake nao sasa wameiga mfano wa wenzao wanawaume, kwa kuendeleza chuki na migawanyiko katika mikutano yao ya hadhara.

“Inasikitisha kumsikia mbunge mwanamke akitusi mwenzake baada ya wao kutofautiana kisiasa. Na nyakati zingine viongozi hao wa kike hutumia maneno machafu ambayo ni ya aibu mbele ya hadhara. Mwenendo kama huu unafaa kukoma,” akasema.

Akaongeza: “Wengi wetu hatukuridhishwa na utendakazi wa makamishna walioongozwa na Kaparo. Walitizama tu huku wanasiasa wakigonganisha jamii moja na nyingi. Hamna faida yoyote kwa sisi viongozi kurushiana cheche za matusi kila mara.”

Mbunge wa Mwea Kabinga Wachira alisema wakati huu ni NCIC pekee inayoweza kupambana na taharuki inayopanda nchini kutokana na joto lililoibuliwa na uchaguzi mdogo wa Kibra.