Uhuru mbioni kufufua Nasa

Uhuru mbioni kufufua Nasa

Na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta, Jumanne aliendelea na mikutano yake ya kisiri na vigogo wa kisiasa wanaokamia kumenyana na naibu wake, Dkt William Ruto katika uchaguzi mkuu ujao wa urais.

Rais Kenyatta alitua Mombasa kutoka Uingereza mnamo Julai 30 na tangu wakati huo, hajaongoza hafla yoyote ya umma hadharani.

Jumanne, Rais alikutana na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, Bw Kalonzo Musyoka ambaye ni Kiongozi wa Wiper, Musalia Mudavadi wa Amani National Congress (ANC), Seneta wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula anayeongoza Ford-Kenya na mwenzake wa Baringo, Bw Gideon Moi ambaye ndiye Mwenyekiti wa Chama cha KANU.

Rais Uhuru Kenyatta (kati) alipokutana na wanasiasa wa upinzani ambao ni kiongozi wa ODM Raila Odinga, Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetangula (Ford Kenya) na Gideon Moi (Kanu) katika Ikulu ya Mombasa, Agosti 10, 2021. Picha/ PSCU

Mkutano huo uliohudhuriwa pia na Naibu Kiongozi wa ODM, Bw Wycliffe Oparanya ambaye pia ni Gavana wa Kakamega, ulifanyika siku chache baada ya rais kukutana na Bw Odinga ambaye amekuwa Mombasa tangu Alhamisi iliyopita.

Mabw Musyoka, Mudavadi na Wetang’ula ni washirika katika muungano mpya wa One Kenya Alliance (OKA).

Wadadisi wa maswala ya siasa sasa wasema rais anacheza karata za kisiasa kichinichini wakati uhusiano kati yake na naibu wake unazidi kudorora.

Wiki iliyopita, Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee, Bw David Murathe alisema mkutano wa rais na Bw Odinga ulinuiwa kupanga mikakati ya siasa za mwaka 2022.

Rais Kenyatta huwa hafichi nia yake ya kutaka kuwe na muungano wa vigogo wakuu wa kisiasa kuelekea uchaguzi ujao wa urais.

Lengo lake kuwaunganisha viongozi hukumbwa na vikwazo kwa vile kumekuwa na misukosuko baina ya vigogo hao, kwa kuwa kila mmoja anasisitiza ndiye anafaa kuongoza serikali.

Wandani wake wa karibu hudai analenga kumuunga mkono Bw Odinga. Waziri huyo mkuu wa zamani alionekana kutengwa na wenzake ambao kwa kauli moja waligura Muungano wa NASA na kuunda ule wa OKA.

Bw Odinga kufikia sasa hajatangaza rasmi kutaka kuwania urais katika uchaguzi ujao.

Msemaji wa ikulu, Bi Kanze Dena alithibitisha mkutano huo wa Jumanne bila kutoa maelezo mengi kuhusu yaliyojiri mkutanoni.

“Miongoni mwa masuala ambayo viongozi hao walijadili ni kuhusu athari ya Covid-19 kwa nchi, jinsi ya kufufua uchumi, na umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano,” akasema kwenye taarifa kwa wanahabari.

Akizungumza Jumapili baada ya kuhudhuria ibada katika Kanisa Kuu la Dayosisi ya Mombasa la Anglikana (ACK), Bw Odinga alikataa kufichua yale ambayo walijadiliana kwenye mkutano wao wa Jumamosi.

“Nilikutana na Rais Uhuru Kenyatta na tumekuwa tukikutana. Lakini hatukuwa na kitu cha kutangaza. Tulikutana kupiga gumzo,” alisema Bw Odinga.

Mkwaruzano kati ya Dkt Ruto na maafisa wa serikali walio waaminifu kwa Rais Kenyatta ulizidi mwishoni mwa wiki iliyopita alipozuiwa kusafiri nchini Uganda baada ya kusubiri kwa saa kadhaa katika uwanja wa ndege.

Kisa hicho kilifuatwa na tukio ambapo rafiki yake ambaye ni raia wa Uturuki, Bw Harun Aydin, alikamatwa na makachero wa kikosi cha kupambana na ugaidi aliporejea nchini kutoka Uganda na kuzuiliwa kwa siku mbili kabla arudishwe nchini kwao bila kupelekwa kortini.

Dkt Ruto na wandani wake wamedai matukio hayo ni sehemu ya njama za kutishia mtu yeyote anayeshirikiana naye ili kumpunguzia ushawishi kabla ya 2022.

You can share this post!

AFYA: Vidonda vya tumbo

Kuna pilipili mboga za rangi tofauti, kila moja ina faida...