‘Uhuru na Raila wanataka kura ya maamuzi upesi’

‘Uhuru na Raila wanataka kura ya maamuzi upesi’

Na MWANGI MUIRURI

MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge Kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) Muturi Kigano amedai kuwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wanataka mpango wa kuandaliwa kwa kura ya maamuzi kuhusu Mswada wa BBI uharakishwe.

Mbunge huyo wa Kangema alisema kuwa kamati yake imewekewa presha ya kuwasilisha ripoti kuhusu Mswada huo wa Marekebisho ya Katiba, 2020, bungeni ili ijadiliwe kabla ya kuwasilishwa kwa Rais Kenyatta. Baadaye Rais atakayeiwasilisha kwa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Bw Kigano hata hivyo aliungama kuwa wao kama kamati wanakabiliwa na changamoto kadhaa zilizochangia wao kufeli kutimiza makataa ya Aprili 1, 2021 yaliyowekwa na Spika wa Bunge la Kitaifa, Bw Justin Muturi.

Hata hivyo, alisema kamati yake inashirikiana na Kamati ya Sheria ya Seneti kutanzua changamoto zinazowazuia kukamilisha ripoti hiyo.

Bw Muturi alisema baadhi ya wanachama wa kamati ya Bw Muturi na ile ya Seneti inayoongozwa na Seneta wa Nyamira, Bw Okong’o Omogeni wangali wanashikilia kuwa sharti wabunge na maseneta waruhusiwe kuufanyia mageuzi mswada huo.

“Ni kweli kwamba wabunge hawataki kutumiwa tu kupitisha mswada huo bila kuufanyia mabadiliko machache. Wanataka waruhusiwe kufanya mabadiliko machache,” akasema.

Bw Muturi pia anasema uchambuzi wa memoranda nyingi ambazo kamati yake ilipokea kutoka kwa taasisi 65, wadhamini na wadau wengine wakati wa vikao vyake vya umma ni changamoto nyingine inayochelewesha kuwasilishwa kwa ripoti hiyo.

Alisema kuna masuala mazito ya kikatiba yaliyoibuliwa katika memoranda hizo ambazo zinahitaji kuchanganuliwa na kuamuliwa kwa umanikifu.

Bw Kigano, hata hivyo, alisema Mswada wa BBI umekingwa dhidi ya kufanyiwa marekebisho na “hakuna taifa lingine ambalo tunaweza kuiga kwani Kenya ndiyo taifa la kwanza kurekebisha katiba kwa njia hii ya kukusanya sahihi kutoka kwa umma”.

Hata hivyo, alisema kuwa kura ya maamuzi sharti ifanyike hata kama mswada huo utakataliwa na bunge la kitaifa pamoja na seneti.

Wiki jana, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Amos Kimunya alisema kura ya maamuzi inaweza kufanyika mwezi ujao “kwa kuwa mswada huo unasheheni masuala ambayo yataamuliwa wakati wa upigaji kura”.

Bw Kimunya alisema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haina sababu ya kuchelewesha maandalizi ya kura ya maamuzi kwa sababu “hata bila mchango wetu kama bunge, mswada huo bado utawasilishwa kwa kura ya maamuzi baada ya kupitishwa na zaidi ya mabunge 24 ya kaunti”.

Kufikia sasa, wanasiasa wakuu nchini wanapendekeza kuwa kura ya maamuzi ifanyike Julai, shughuli ambayo IEBC imekadiria kuwa itagharimu Sh14 bilioni.

Jana, Bw Muturi alisema kuwa JLAC itaandaa mkutano wa siku tatu wiki ijayo ili kupokea ushauri kutoka kwa wataalamu wawili waliokodiwa kutoa mwelekeo kuhusu masuala tata katika ripoti hiyo.

Tayari ripoti hiyo inaandikwa na makarani wa kamati hiyo. “Spika wa bunge la kitaifa pia amedokeza kuwa huenda akaitisha kikao maalum katika wiki ya mwisho wa Aprili, hatua ambayo imetupa muda zaidi kukamilisha ripoti hiyo,” akaeleza.

You can share this post!

Wizara yataka Wakenya waliopoteza ajira walipwe na serikali

Magavana wahepa suala la ubadhirifu wa pesa za corona