Siasa

Uhuru na Raila warai Wakenya waunge mkono BBI

October 26th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenya na Kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, jana waliwarai Wakenya kuunga mkono na kupitisha ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), wakisema ndiyo njia ya pekee ya kuunganisha nchi, kumaliza ukabila na kulinda maslahi ya vijana.

Rais Kenyatta alisema kuwa wanasiasa, akiwemo yeye binafsi, wamekuwa wakijifanya wana umoja ilhali ukweli ni kuwa wamegawanyika kulingana na makabila yao.

“Tuache kujifanya na kujidaganya eti sisi ni viongozi wa kitaifa ilhali tunaegemea makabila yetu. Ni kwa kukiri ukweli ambapo tutarekebisha yanayotuathiri kama taifa,” akasema Rais akihutubia wajumbe wakati wa kuzindua ripoti ya BBI katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi.

Alimmiminia sifa Bw Odinga kwa kukubali wazike tofauti zao za kisiasa kwa ajili ya Kenya: “Ninamshukuru kwa dhati ya moyo ndugu yangu Raila kwa hatua yake ya kizalendo,” alisema.

Pia alimkosoa naibu wake William Ruto kwa kuanza siasa za mapema na kutelekeza maono waliyokuwa nayo katika chama cha Jubilee: “Tulianza vizuri. Uongozi ni kupokezana kijiti lakini badala ya kusubiri, Ruto aliamua kurudi nyuma,” alisema.

Rais alikanusha madai ya Dkt Ruto na washirika wake wa kisiasa kwamba Bw Odinga alitumia handisheki kuingia serikalini, akisema anashangaa Ruto anakosoa BBI ilhali alimshirikisha katika kila hatua.

“Raila hajawahi kuwa serikalini. Hakutamani kuwa serikalini na hakutaka kuwa sehemu ya serikali. Tuliamua kuungana kwa ajili ya kufanya Kenya kuwa bora zaidi kwa vizazi vijavyo,” alisema.

Alisema BBI inalenga kuimarisha Ktiba ya 2010 hasa kwa kumaliza ukabila na kuwashirikisha vijana katika maamuzi ya serikali.

“Ukweli ni kwamba vijana wetu ni bomu linaloweza kulipuka na kutulipua kama taifa iwapo hatutawashirikisha kikamilifu katika maamuzi ya nchi. Nina furahi kwa sababu waandalizi wa ripoti hii wamewatambua,” alisema Rais Kenyatta.

Miongoni mwa mapendekezo yanayolenga vijana ni kuwapa afueni ya miaka minne kabla ya kuanza kulipa mikopo ya elimu ya juu, wanaoanzisha biashara kutolipa kodi kwa miaka saba na kuwapa mikopo nafuu ya kuanzisha biashara.

Bw Odinga alisema ili kumaliza ukabila waliamua kuanzisha filosofia ya utu ndani ya BBI.

Alipuuza wanaodai kwamba mpango wa maridhiano unanuia kumfanya rais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

“Mchakato wa BBI unalenga kuunganisha nchi na sio kunifanya rais. Mimi na Rais Kenyatta tuliamua kuanzisha BBI kwa sababu ya e ambayo yalikuwa yakiwakumba Wakenya,” alisema.

Bw Odinga na Rais Kenyatta walisema kwamba hawataki kura ya maamuzi itakayozua mgawanyiko.

“Wale ambao wana malalamiko wanafaa kuyaleta yajadiliwe. Kwa mfano, watu wanaoishi na ulemavu walilotoa malalamishi yao na yametiliwa maanani,” alisema.

Alisema kwamba wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022 haujafika, na akamtaka Rais Kenyatta na Dkt Ruto kutekeleza ajenda zao kwa Wakenya.