MakalaSiasa

Uhuru na Ruto wapeleka vita vyao vya ubabe katika makanisa

July 26th, 2020 2 min read

VIONGOZI wa makanisa wamejipata katikati ya ubabe wa kisiasa baina ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto.

Rais Uhuru Kenyatta ameanzisha harakati za kupitia kwa viongozi wa makanisa na wazee kuzima ushawishi wa Dkt Ruto katika maeneo ya Mlima Kenya, Bonde la Ufa na Magharibi.

Naibu wa Rais amekuwa akitumia viongozi wa makanisa kupenya katika eneo la Mlima Kenya ambayo ni ngome ya Rais Kenyatta.

Naibu wa Rais pia amekuwa akijaribu kujipendekeza kwa vijana na kujionyesha kama ‘mwakilishi’wa maskini ili kujipatia uungwaji mkono miongoni mwa Wakenya wa mapato ya chini.

Wadadisi wanasema kuwa kwa kujifanya ‘maskini’, Dkt Ruto analenga kuwafanya Rais Kenyatta, kinara wa ODM Raila Odinga na Seneta wa Baringo Gideon Moi kuonekana kama watoto wa matajiri wasiojali masilahi ya watu wa mapato ya chini.

Kulingana na Kiranja wa Wengi katika Seneti Irungu Kang’ata, Rais Kenyatta amekuwa akiendeleza kampeni ya chini kwa chini kuwafikia viongozi wa makanisa na wazee katika eneo la Mlima Kenya ili waunge ajenda yake ya maendeleo.

Rais Kenyatta, kulingana na duru za kuaminika, alichukua hatua hiyo kutokana na ukweli kwamba umaarufu wa Dkt Ruto umekuwa ukiongezeka katika eneo la Mlima Kenya licha ya kiongozi kuonyesha wazi kuwa hana haja naye kisiasa.

Rais Kenyatta pia amekuwa akitumia mmoja wa mawaziri kutoka Bonde la Ufa kuwafikia viongozi wa makanisa na wazee ili kuwashawishi kuunga mkono handisheki baina yake na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Rais Kenyatta analenga kuondoa madai ambayo yamekuwa yakienezwa na wanasiasa kutoka Bonde la Ufa kwamba handisheki imetenga jamii ya Wakalenjin.

Katika eneo la Magharibi, Rais Kenyatta amekuwa akitumia Gavana wa Kakamega na Waziri wa Ugatuzi Eugine Wamalwa kufikia viongozi wa makanisa na wazee.Dkt Ruto alijitokeza na kuwa mtetezi wa makanisa, maeneo ya ibada yalipofungwa kufuatia janga la virusi vya corona.

Naibu wa Rais amekuwa akikutana na viongozi wa kidini kutoka eneo la Mlima Kenya, hatua ambayo imetia tumbojoto kambi ya Rais Kenyatta.

Alhamisi, Dkt Ruto alikutana na viongozi wa Kanisa la Africa Inland (AIC) kutoka Kaunti ya Baringo ambayo ni ngome ya kiongozi wa Kanu Bw Moi.

Katika mkutano huo, Naibu wa Rais aliahidi kuwasaidia kujenga hoteli inayoendelea mtaani Karen, Nairobi.

“Ninaahidi kusaidia kanisa ili kuwawezesha kujikimu kimaisha kufuatia hali ngumu ambayo imesababishwa na janga la virusi vya corona,” akasema Dkt Ruto kupitia akaunti yake ya Twitter.

Siku hiyo hiyo, Naibu wa Rais alikutana na viongozi wa Kanisa kutoka Kaunti za Kiambu, Murang’a na Laikipia ambazo ni ngome ya Rais Kenyatta.

Viongozi hao wa makanisa waliandamana na mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto.