Habari

Uhuru na Ruto waungana na wapenzi wa Kiswahili kumwomboleza Prof Walibora

April 15th, 2020 2 min read

Na HASSAN WEKESA

RAIS Uhuru Kenyatta na naibu wake Dkt William Ruto wameungana na wapenzi wa Kiswahili kutuma salamu za pole kwa familia ya mwendazake Prof Ken Walibora aliyekuwa mwandishi mahiri wa fasihi na mwahabari mtajika.

Tanzia hii ilithibitishwa mapema Jumatano baada ya mwili wake kupatikana katika mochari ya Hospitali Kuu ya Kenyatta, ikiwa ni siku zaidi ya tano baada ya kutafutwa na familia na marafiki tangu Ijumaa wiki ilyopita.

“Prof Ken Walibora alikuwa mwandishi na mwanahabari aliyeielewa kazi yake na ambaye ubunifu wake ulitoa na utaendelea kutoa mchango muhimu kuchochea ari ya vizazi vijavyo,” amesema Rais Kenyatta.

Naye Dkt Ruto amesema Prof Walibora alikuwa mtetezi wa lugha ya Kiswahili ambaye alikuwa mchangamfu aliyependa tashtiti kwa lengo la kufurahisha wanajamii.

Kifo chake kilitokea baada ya kugongwa na gari la uchukuzi wa umma – matatu – katika barabara ya Ladhies jijini Nairobi mnamo Ijumaa.

Si pigo tu kwa tasnia ya uandishi, bali pia kwa mataifa 13 barani Afrika yanayokienzi Kiswahili na jumuiya pana ya wasomi wa fasihi ambayo ni kioo cha jamii ambapo huangazia uozo na pia mema.

Akithibitisha kifo chake, meneja wa mawasiliano katika Hospitali ya Kuu ya Kenyatta (KNH) Bw Hezekiel Gikambi aliyekuwa rafiki wake wa karibu, amesema Prof Walibora alikuwa mtu wa watu ambaye alikuwa na maono mengi aliyotaka kutimiza kuifanya Kenya na dunia nzima pahala salama.

“Profesa Ken Walibora kwa kweli ulitaka kutimiza mengi, lakini umetangulia,” ameandika Bw Gikambi ambaye pia ni mwandishi mahiri katika akaunti yake ya Twitter.

Mwalimu Abdilatif Abdalla amesema Ken alikuwa ni mwandishi aliyejitolea kufanya utafiti wa kina ili kuwapa wasomaji kazi za kujivunia.

“Machi 2020 nilihitaji makala yake aliyoandika kuhusu mtazamo wangu ambapo nilikuwa nimetoa maelezo miongoni mwa wapendao lugha ya Kiswahili kwamba kupelekea pia ni kusababisha naye akawa ameomba nambari yangu ya simu akiahidi kunitumia makala yenyewe,” amesema mwalimu Abdalla ambaye anatambulika sana katika fani ya ushairi, hasa diwani yake ya Sauti ya Dhiki.

Wakati wa uhai wake aliandika vitabu vingi, maarufu vikiwa riwaya ya ‘Siku Njema’, ‘Kidagaa Kimemwozea’ ile ya ‘Kufa Kuzikana’, na ‘Nasikia Sauti ya Mama’ ambacho daima aliweka picha ya jalada lake katika picha ya utambulisho kwa WhatsApp.

Pia alichangia katika uhariri na uandishi wa hadithi fupi katika diwani ya Damu Nyeusi.

Wapenzi wa kazi zake wametuma salamu za pole kwenye mitandao ya kijamii wakimtaja kwamba alikuwa mtu mpole licha ya kwamba alikuwa nguli mwenye sifa Afrika Mashariki na ulimwenguni kote.

Mwalimu Phyllis Mwachilumo akiwa mjini Kikuyu, Kaunti ya Kiambu ametoa salamu za pole akitaja sifa alizotambua mwendazake alikuwa nazo.

“Alikuwa mpole, mnyenyekevu na aliyefaa jamii yake kwa kuwapa watu matumaini – ujio wa siku njema – na ninatarajia kuwa anaenda kuiona siku njema peponi, ” amesema mwalimu huyo.

Profesa Walibora atakumbukwa na wasomaji na waandishi wa gazeti la ‘Taifa Leo’ waliopenda sana kufululiza hadi ukurasa wa 13 kujisomea kitengo cha Kina cha Fikira ambacho pia walizoea kukiita Kauli ya Walibora.

Makala yake ya Machi 2020 yaliangazia sana janga la virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid–19 ambapo alishajiisha wanahabari waite kirusi cha Korona na wala si virusi vya corona.

Pia aliangazia jinsi ambavyo kuna Korona nyingine mbali na maradhi haya, akiitaja kuwa ni ile ya wakoloni kuwafanya Waafrika wachukie lugha zao, hasa Kiswahili.

Ken amewahi kufanya kazi katika shirika la habari nchini Kenya (KBC), kushiriki mafunzo katika shirika la Deutsche Welle (DW) nchini Ujerumani, na pia kampuni ya Nation Media Group alipohudumu kama mkuu wa ubora wa Kiswahili huku akisoma taarifa za habari katika runinga ya QTV kabla ya kuondoka hapo Januari 2017.

Maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi kumkamata dereva aliyesababisha ajali iliyomuua msomi huyo ili baadaye wamfungulie mashtaka.