Uhuru, naibu wake wasuka njama ya kuangusha waasi

Uhuru, naibu wake wasuka njama ya kuangusha waasi

Na ONYANGO K’ONYANGO

WANDANI wa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto wanabuni njama inayolenga kufunga ngome zao za Mlima Kenya na Rift Valley, mtawalia kudhamini wagombeaji watakaoangusha “waasi” katika maeneo hayo mawili kwenye uchaguzi wa 2022.

Katika Rift Valley, wandani wa Dkt Ruto tayari wameanza mipango ya kusaka wagombeaji ambao wanahisi wanaweza kuwaangusha viongozi wandani wa Rais Kenyatta katika uchaguzi huo.

Kwa upande mwingine, viongozi wa Jubilee wanalenga maeneo bunge katika eneo la Mlima Kenya yanayowakilishwa na wandani wa Dkt Ruto.

Wanapanga kuteua washirikishi wa chama, kufungua afisi na kuwadhamini wagombeaji watakaobwaga wabunge wandani wa Naibu Rais katika eneo pana la Mlima.

Hii ni baada ya kubainika kuwa Rais Kenyatta amekataa katakata kuunga mkono azma ya Dkt Ruto kumrithi atakapostaafu mwaka 2022.

Wandani wa Rais Kenyatta ambao wanalengwa katika ngome ya Naibu Rais ya Rift Valley ni pamoja Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee Joshua Kutuny (mbunge wa Cherang’any), Alfred Keter (Nandi Hills), Silas Tiren (Moiben), William Chepkut (Ainabkoi) na Dkt Swarup Mishra (Kesses).

Wengine ni; Gavana wa Elgeyo Marakwet Alex Tolgos, Seneta wa Uasin Gishu Prof Margaret Kamar na mgombeaji wa ugavana wa Uasin Gishu 2017, Zedekiah Bundotich, almaarufu Buzeki.

Jumamosi, wandani wa Dkt Ruto wakiongozwa na Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi walifichua kuwa hawatawavumilia wale ambao wanapinga azma ya naibu huyo wa rais kuingia Ikulu 2022.

“Nawahimiza mahasidi wetu kisiasa Rift Valley kutii msimamo wetu au tuwaangushe. Hatutakubali propaganda zenu za kutaka kugawanya jamii yetu,” akasema Bw Sudi.

“Hatuwezi kukubali vitisho, propaganda na chuki kuingizwa katika UDA. Tulianza safari kitambo na ni mahasla pekee wanaokubaliana na sera zetu wataruhusiwa kuungana nasi, sio waasi,” akasema.

Akaongeza hivi: “Hata hivyo, wako huru kuendelea na mipango yao ya kisiasa ama kwa kusajili chama chao au kuungana na vyama vingine. Wako huru kujiunga na ODM, Kanu, ANC, Ford Kenya au wasalie na kiongozi wa chama chao Uhuru Kenyatta.”

Kwa upande wake, Mbunge wa Aldai Cornelly Serem aliambia Taifa Jumapili kwamba wabunge kutoka Rift Valley ambao hawaungi mkono ndoto ya Dkt Ruto ya Ikulu 2022, watakabiliwa na kibarua watakapotetea viti vyao.

“Kama viongozi kutoka Rift Valley, tumekubaliana kwa kauli moja kwa kila mwanasiasa sharti ampigie debe Naibu Rais,” akasema.

“Yeyote ambaye haungi mkono azma ya Naibu Rais kuingia Ikulu sharti ajue kwamba ataangamia kisiasa. Tumewashauri watu wetu kwamba watu hawa wakiongozwa na Kutuny wanawadanganya na hawastahili kuungwa mkono kwa wadhifa wowote,” akaeleza Bw Serem.

Katika eneo la Mlima Kenya, chama cha Jubilee kinalenga kuangusha wabunge; Alice Wahome (Kandara), Ndindi Nyoro (Kiharu), Rigathi Gachagua (Mathira), Moses Kuria (Gatundu South) na mwenzao wa Kikuyu Kimani Ichungwah (Kikuyu).

Bw Kutuny, Jumamosi alisema wakati huu wanasaka kuteua maafisa wapya wa Jubilee watakaokabiliana na wimbi la chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika eneo la Mlima Kenya.

“Chama kinapanga kuwa na maafisa wapya kuchukua nafasi za wale walijiondoa. Tutatoa tangazo hilo hivi karibuni. Pia tunataka kudhamini wagombeaji watakaowaangusha waasi hao katika maeneobunge yao katika uchaguzi mkuu ujao,” Bw Kuttuny akaambia Taifa Jumapili mnamo Jumamosi.

You can share this post!

JAMVI: Misimamo mikali OKA inaweza kuwafaidi au kuwabomoa...

Lewandowski aweka rekodi ya ufungaji katika mechi za...