Habari

Uhuru, Raila njia panda kuhusu IEBC

August 1st, 2020 1 min read

JUSTUS OCHIENG na WALTER MENYA

RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, wako katika njia panda kuhusu hatima ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Huku ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) ikichelewa kutolewa kwa umma ili kuanzisha mchakato wa kurekebisha IEBC, miswada kadha kuhusu tume hiyo pia imekwama bungeni.

Mwezi huu, imesalia miaka miwili kabla Uchaguzi Mkuu ufanyike 2022.

Ingawa vyama vya Jubilee na ODM, vyao Rais Kenyatta na Bw Odinga mtawalia, vimekubali kwamba kuna haja kubadilisha mfumo wa uchaguzi nchini, ingali kubainika atakayeendesha mchakato huo.

Swali la ikiwa kura ya maamuzi itafanyika kabla ya 2022 pia limeibukia kuwa kizungumkuti, huku baadhi ya wabunge wakipendekeza zoezi kuandaliwa pamoja na uchaguzi.

Wale wanaotoa pendekezo hilo ni viongozi wanaoegemea mrengo wa kisiasa wa Naibu Rais William Ruto, msimamo unaopingwa vikali na wanasiasa wanaounga mkono mchakato wa BBI.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati, aliiambia Taifa Leo: “Kura ya maamuzi inaweza kufanyika wakati wowote, ikiwa tu maandalizi yake yatazingatia kanuni zote za kikatiba. Tume iko katika harakati za mwisho mwisho kumaliza taratibu zitakazofanikisha maandalizi yake.”

Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Raphael Tuju, alisema kile kinachohitajika ni “mazingira yatakayofanikisha mchakato huo wala si yule atakayeongoza tume.”

“Tunahitaji mfumo utakaotuondolea changamoto za kisiasa ambazo zimekuwa zikituandama. Hili ni kwa kuwa hatuwezi kupata maendeleo katika nchi ambayo haina amani,” akasema.

Naye Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna, alisema huenda nchi ikalazimika kutumia tume ya sasa kuendesha zoezi hilo kutokana na muda mfupi uliopo kabla ya 2022.

“Ndio itakuwa shughuli ya mwisho kwa tume kusimamia. Mojawapo ya mapendekezo yaliyopo ni IEBC kuvunjwa baada za zoezi kukamilika,” akasema.

Hata hivyo, alieleza wanatarajia kuifanyia mageuzi tume kabla ya maandalizi ya shughuli hiyo.