Habari

Uhuru, Raila sasa waamua BBI haitabadilishwa

November 2nd, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, wameunga washirika wao wa kisiasa kutangaza wazi kuwa mapendekezo ya ripoti ya Jopokazi la Maridhiano BBI haitabadilishwa kabla ya kura ya maamuzi.

Hii ni tofauti na kauli yao wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo kwamba, malalamishi ya Wakenya yangezingatiwa.

Naibu wa Rais William Ruto na washirika wake wamekuwa wakitaka ripoti hiyo ifanyiwe marekebisho kabla ya kufanyika kwa kura ya maamuzi.

Taarifa ya pamoja iliyosomwa Jumatatu na Seneta wa Siaya, James Orengo baada ya mkutano wa siku mbili wa viongozi wanaounga mkono BBI uliofanyika mjini Naivasha ilisema kuwa, mswada huo hautafanyiwa marekebisho zaidi.

“Jumla ya wabunge na maseneta 300 tumeafikiana kuunga mkono mchakato wa kutaka kurekebisha Katiba kwa kuzingatia mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti ya BBI,” akasema Bw Orengo.

Rais Kenyatta na Bw Odinga walikuwa miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo.

Wakati wa uzinduzi wa ripoti ya mwisho ya BBI katika ukumbi wa Bomas, Nairobi, wiki iliyopita, Naibu wa Rais William Ruto alikosoa baadhi ya mapendekezo yaliyomo katika ripoti hiyo huku akisisitiza kuwa kuna haja ya kuirekebisha kabla ya kura ya maamuzi.

Dkt Ruto anapinga pendekezo la kutaka vyama vya kisiasa kuwa na wawakilishi wao ndani ya Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), seneti kupunguziwa majukumu ya kugawa pesa za kaunti na kubuniwa kwa baraza la polisi miongoni mwa mapendekezo mengine.

Akizungumza Jumatatu alipokutana na viongozi na wasomi kutoka eneo la Ukambani, Dkt Ruto alisisitiza kuwa inawezekana kufanyia mabadiliko baadhi ya maswala tata kwenye ripoti ya BBI.

Alisema kwamba, maafikiano yataepushia nchi kampeni kali kabla ya kura ya maamuzi.

“Tunaweza kuketi chini na kuafikiana kuhusu masuala tata ndani ya BBI ili tuweze kutembea pamoja kama taifa,” akasema Dkt Ruto.

Wandani wa Naibu wa Rais wametishia kuanzisha kampeni ya kuwasihi Wakenya kukataa BBI iwapo matakwa yao hayatashughulikiwa.

Wandani wa Dkt Ruto wakiongozwa na seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen na mwenzake wa Nandi Samson Cherargei, walilalama kuwa hawakualikwa kuhudhuria mkutano wa Naivasha.

Lakini Mbunge Maalumu Maina Kamanda anashikilia kuwa wanaopinga walifaa kutoa mapendekezo yao mbele ya jopokazi la BBI lilipokuwa likikusanya maoni kutoka kwa Wakenya.

Wadadisi wanasema, Dkt Ruto huenda asipinge BBI kwa sababu hataki kufanya kampeni mara mbili; kampeni ya kura ya maamuzi na Uchaguzi Mkuu wa 2022. Waliohudhuria mkutano wa Naivasha waliafikiana kuhusu mwongozo wa ugavi wa maeneobunge mapya. Kulingana na mwongozo huo, eneobunge linafaa kuwa na angalau watu 132,138.

Iwapo mapendekezo hayo yatapitishwa, idadi ya wabunge katika Kaunti ya Nairobi itaongezeka karibu maradufu kutoka 17 sasa hadi 33.

Kaunti ya Mombasa itaongezewa wabunge watatu, kutoka sita hadi tisa huku Kilifi ikiongezewa wabunge wanne hivyo kufanya idadi ya viti vya ubunge kuwa 11.

Baadhi ya kaunti ambazo hazitapata maeneobunge mapya ni Busia, Migori, Kisii, Vihiga, Baringo, Nandi, Elgeyo Marakwet, Samburu, Pokot Magharibi, Nyeri, Nyandarua, Tharaka Nithi, Isiolo na Masarbit.