Uhuru, Raila wahudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais Hichilema

Uhuru, Raila wahudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais Hichilema

CHARLES WASONGA na PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta, Jumanne alikuwa miongoni mwa viongozi 10 wa Mataifa na Serikali za Afrika waliohudhuria sherehe ya kufana ya kuapishwa kwa Rais mpya wa Zambia Hakainde Hichilema jijini Lusaka.

Hichilema, 59, aliapishwa kuwa rais wa saba wa taifa hilo sambamba na Makamu wa Rais Bi Mutale Nalumango katika Uwanja wa Michezo wa National Heroes na kuongozwa na kaimu Jaji Mkuu wa Zambia Michael Musonda.

Katika hotuba yake baada ya kuapishwa, Rais Hichilema alisema serikali yake itawapa nafasi sawa raia wote wa Zambia na akaahidi kuhakikisha wote wanafurahia uhuru wao jinsi inavyobainishwa na Katiba ya nchi hiyo.

“Mimi ni mvulana tu wa vijijini mliyemfanya kuwa rais wa saba wa taifa letu tukufu. Ushindi huu ni wa raia wote wa Zambia hasa vijana waliojitokeza kwa wingi kupiga kura. Tulionyesha ulimwengu mzima ukakamavu wa demokrasia yetu,” akasema Rais Hichilema.

Kiongozi huyo mpya wa Zambia alisema serikali yake itazingatia kufufua uthabiti wa kiuchumi, udhibiti wa madeni na kuhakikisha hakuna raia wa Zambia watakaolala njaa.

“Tutalenga kujumuisha na sio kutenga, umoja na sio utengano, kujumuika pamoja na sio kuwatawanya watu wetu,” Rais Hichilema akaahidi.

Alisema kuwa uchaguzi wa amani na kubadilishwa kwa madaraka kumeonyesha sifa kubwa za kidemokrasia za Zambia kwa ulimwengu.

“Tumeonyesha ulimwengu wote uthabiti wa demokrasia, kwamba watu wameamua ni wakati wa mabadiliko na tunaweza kusema mabadiliko yako hapa,” akasema Bw Hichilema.

Viongozi waliozungumza wakati wa hafla hiyo ya kuvutia waliwapongeza wananchi wa Zambia kwa kufanya uchaguzi wa amani wakisema uchaguzi huo umeonyesha uwezo wa Afrika wa kusimamia masuala yake.

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Muungano wa Afrika (AU), na Rais Lazarus Chakwera wa Malawi ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), walizungumza kwa niaba ya viongozi na marais waliohudhuria hafla hiyo na kuwapongeza Wazambia kwa kufanya uchaguzi wa amani.

Rais Tshisekedi alimhakikishia kiongozi huyo mpya wa Zambia kwamba AU itamuunga mkono huku anapochukua majukumu ya taifa lake na kuwapongeza Wazambia kwa kudumisha demokrasia.

Kwa upande wake, Rais Chakwera alisema uchaguzi wa Zambia umeonyesha kwamba demokrasia barani Afrika imeimairika akisema taifa hilo limedhihirisha nguzo ya maadili ya kikatiba.

“Huu ndio ushindi wa moyo wa Afrika, mfano wa Afrika tunayoitaka ambayo sisi tunaifahamu… Hii hadithi ya Zambia ni hadithi bora kwamba Afrika sio changa tena, Afrika imeonyesha moyo wa umoja na ukomavu,” akasema kiongozi huyo wa Malawi.

Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo ambaye aliwakilisha jopo la watu mashuhuri barani Afrika, alisema Zambia imeonyesha kwamba sasa Afrika imekomaa na inawezekana kubadilishana mamlaka kutoka chama kimoja hadi kingine kwa njia ya amani.

Viongozi wengine kwenye sherehe hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga ambaye pia ni mjumbe wa AU kuhusu miundomsingi walikuwa ni Rais Hage Geingob wa Namibia, Filipe Nyusi wa Msumbiji na Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, Mokgweetsi Masisi wa Botswana, Samia Suluhu wa Tanzania na Mfalme Mswati III wa Eswatini pia walihudhuria.

You can share this post!

Madiwani waasi ODM baada ya Kingi kuadhibiwa

Raia wafa njaa viongozi wakipiga domo