Habari

Uhuru, Raila wakutana kisiri ufuoni

June 16th, 2019 3 min read

Na CAROLINE WAFULA na VICTOR RABALLA

RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, Ijumaa jioni walifanya mkutano wa kisiri katika kilabu maalum cha Yacht Club mjini Kisumu.

Viongozi hao waliwasili katika klabu hicho kilichoko katika mtaa wa Milimani, ufuoni mwa Ziwa Victoria kwa msafara wa magari 12 pekee ambapo walifanya mazungumzo kwa saa moja huku wakila chakula cha jioni.

Rais Kenyatta na Bw Odinga walikuwa wametoka kuhudhuria mazishi ya mama ya Gavana wa Kisumu, Anyang Nyong’o katika kijiji cha Ratta, eneobunge la Seme.

Hafla hiyo, iliyohudhuriwa na viongozi wengi, ilikamilika mwendo wa saa kumi na moja za jioni kabla ya kupanda helikopta tofauti hadi uwanja wa ndege wa Kisumu.

Walipotua, walipanda katika gari moja na kuondoka wakipiga gumzo.

Ajabu ni kwamba, magari kwenye msafara wa wawili hao hayakuwa yale wanayotumia katika shughuli rasmi kwani hayakuwa na ving’ora na vijibendera wala pikipiki za polisi kama ilivyo kawaida kwa msafara wa Rais.

Hali hiyo ilifanya wananchi kutotambua kwamba magari yaliyowabeba Rais Kenyatta na Bw Odinga yalikuwa kwenye msafara.

Kabla ya kuelelea kilabu hicho, wawili hao walifanya ziara ya ghafla katika Chuo cha Mafunzo kuhusu Viumbe vya Majini (Marine Training Institute) kilichoko karibu na bandari ya Kisumu. Walikagua shughuli za ujenzi zinazoendelea hapo huku maafisa wa usalama wakiwazuia wananchi na wanahabari kukaribia eneo hilo.

Duru ziliambia Taifa Jumapili kwamba, mkutano huo wa faragha katika Yacht Club ulihudhuriwa na Waziri wa Usalama Fred Matiang’i na mtu mwingine ambaye hakutambuliwa japo alikisiwa kuwa mkuu wa utumishi wa umma Joseph Kinyua.

Duru zilisema walishiriki mlo wa ugali wa rangi ya kahawia (brown), samaki aina ya tilapia na mboga za kienyeji.

“Vilevile, waliagiza chupa kadha za bia na juisi huku wakipiga gumzo kwa muda wa takriban saa moja hivi,” akasema mhudumu mmoja katika klabu hicho ambaye alitudokezea yaliyojiri katika mkutano huo.

Ni katika klabu hii ambapo viongozi hao wawili, ambao tangu waridhiane kisiasa mnamo Machi 9, mwaka jana, wamekuwa wakijiita “ndugu,” walitembelea mnamo Januari 19 baada ya kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa mwenyekiti wa Hazina ya Ustawishaji wa Vijana, Bruce Odhiambo katika eneo bunge la Muhoroni.

Wakati huo pia, Rais Kenyatta aliwashangaza walinzi wake na maafisa wa itifaki alipobadili mpango wa kusafiri wakati uliopangwa na kuamua kujivinjari Kisumu akisafiri kwa magari ya kawaida.

Ijumaa, Rais alipowasili katika Yatch Club kwa mara ya pili akiandamana na Bw Odinga na wageni wake wachache, wahudumu walichangamka huku viongozi hao wakielekea moja kwa moja katika chumba maalum karibu na ufuo wa Ziwa Victoria.

“Kama kawaida yake, Rais aliwasalimia wateja na wahudumu kwa kuwapungia mikono kabla ya kuketi katika chumba hicho kilichokuwa na viti vinne,” mhudumu mmoja, ambaye aliomba tulibane jina lake, alituelezea.

Rais Kenyatta alisikika akifurahia upepo wa ziwa.

“Ziwa linafurahisha kwani gugumaji limepungua kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na awali tulipokuwa hapa,” alisikika akisema.

Uwepo wa Dkt Matiang’i katika mkutano huo wa Rais Kenyatta na Bw Odinga unatokana na cheo alichotunukiwa cha Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Mawaziri ya Kushirikisha utekelezaji wa miradi ya Serikali Kuu.

Vilevile, Waziri Matiang’i amekuwa haelewani na wanasiasa wandani wa Naibu Rais William Ruto wanayemchukulia kama anayetumiwa kuzima ndoto kiongozi huyo kuingia Ikulu 2022.

Maafisa wengine wachache walioandamana na Rais Kenyatta na Odinga waliketi katika mahala tofauti kwa chakula cha jioni na vinywaji. Mbunge Mwakilishi wa Kisumu ambaye inadaiwa ndiye aliandaa mipango ya mkutano huo pia alionekana katika kilabu hicho.

Lakini mawaziri wengine walioandamana na Rais mazishini, kama vile George Magoha (Elimu), Eugene Wamalwa (Ugatuzi), Sicily Kariuki (Afya) na Raphael Tuju hawakuwepo katika klabu hiyo.

Hata hivyo, shughuli katika klabu hiyo maalum ziliendelea kama kawaida licha ya uwepo wa viongozi hao.

Mwendo wa saa moja na nusu usiku, viongozi hao wawili waliondoka jinsi walivyowasili na kuelekea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kisumu ambapo Rais Kenyatta aliabiri helikopta ya kijeshi kurejea Nairobi.

Rais na ujumbe wake walipoondoka Yacht Club, maafisa wa Ikulu waliwazawadi wahudumu kwa hela chache “ kwa kazi nzuri”.

Safari ya Rais kuelekea uwanja wa ndege ilikuwa ya kasi ya chini. Msafara wake ulipitia barabara za Jomo Kenyatta Highway, Oginga Odinga , Obote na Busia. Wenye magari na waendeshaji boda boda hawakufahamu huo ulikuwa msafara wa Rais kwani walionekana wakiyapita magari hayo kwa kasi.

MAELEZO ZAIDI NA: CHARLES WASONGA