Habari

Uhuru, Raila wapokea stakabadhi yenye mapendekezo ya BBI

October 21st, 2020 1 min read

Na MWANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wamepokea rasmi stakabadhi yenye mapendekezo ya Mpango wa Maridhiano (BBI) katika Ikulu Ndogo ya Kisii katika Kaunti ya Kisii, Jumatano.

Hafla hii imeandaliwa siku moja baada ya Kisii kuwa mwenyeji wa sherehe za Mashujaa jana Jumanne ambapo kiongozi wa nchi alihutubia Wakenya akiwa katika uwanja wa Gusii.

Kiongozi wa nchi amesifu jopokazi la BBI ambalo limefanya kazi na Wakenya mbalimbali kuandaa ripoti hiyo ambayo kulingana na viongozi mbalimbali, itasaidia kumaliza matatizo yanayolikabili taifa.

“Tuisome stakabadhi hii kwa makini bila kuingiza hisia za kisiasa kwa sababu imesheheni mengi muhimu na bila shaka tukikubaliana, itatuvunia matunda na kutuunganisha,” amesema Rais Kenyatta akiahidi kwamba kutakuwa na kikao, katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi, Jumatatu wiki ijayo, cha kusoma sentensi baada ya sentensi na kuelewa yaliyomo.

Naye Odinga amesema pamoja na Rais waliamua waipokee ripoti hiyo Kisii kwa sababu ndiko walikoanzia mchakato wa kukusanya maoni.

“Hii ripoti ina mapendekezo mazuri ya kuimarisha maisha yetu na ya vizazi vijavyo,” amesema Odinga.

Jopokazi la BBI linaongozwa na Seneta wa Garissa Mohamed Yusuf Haji na ilijumuisha pia wanachama wengine 13 wakiwa ni Adams Oloo, Agnes Kavindu, Seneta wa Busia Amos Wako, Florence Omose, Saeed Mwanguni, James Matundura, Major John Seii, Askofu Lawi Imathiu, Maison Leshomo, Morompi ole Ronkai, Askofu Peter Njenga, Rose Moseu, na Askofu Mkuu Zecheus Okot.

Makarani wa jopokazi hilo ni Martin Kimani na Paul Mwangi.