Habari

Uhuru, Raila washutumu wajipatiao utajiri bila jasho

July 12th, 2019 2 min read

Na SAMUEL BAYA na JOSEPH OPENDA

RAIS Uhuru Kenyatta amewataka Wakenya wafanye kazi kwa kujitolea na kwa njia ya haki ili kujenga taifa thabiti kiuchumi.

Akiongea Ijumaa katika eneo la Mang’u-Rongai, katika kaunti ya Nakuru wakati wa mazishi ya wakili Karanja Kabage, Rais Kenyatta alisema hakuna njia ya mkato ya mtu kufaulu isipokuwa kufanya kazi kwa bidi na kujitolea.

Alimpigia mfano marehemu kama mtu ambaye alijizolea umaarufu katika nyanja nyingi, hususani za kiuchumi na alikuwa mfano bora wa mtu mwenye bidii.

“Njia ya pekee ya kufanikisha maisha bora ni kufanya kazi kwa bidii na kwa njia ya haki kwa sababu hiyo ndiyo njia ya pekee ambayo itatusaidai kama taifa kuimarisha uchumi wetu,” akasema.

Rais kadhalika aliwataka Wakenya waishi kama ndugu na kupinga ukabila kwa njia yoyote ile.

Vilevile, Rais aliwatahadharisha Wakenya dhidi ya tabia ya kujiangalia wao tu wanapokuwa na nafasi huku akisema kuna haja ya kubadilisha mtizamo na kuangalia wale ambao wanawahudumia.

“Ikiwa wewe ni daktari, mwanasiasa au hata mwalimu, usijiangalie wewe binafsi ila angalia na wale ambao unawahudumia,” akasema Rais

Mwito huo pia uliungwa mkono na kinara wa upinzani Bw Raila Odinga ambaye alisema kuwa lazima kama taifa tujieushe na ufisadi ambao umerudisha taifa hili nyuma kiuchumi.

“Lazima tuache kushabikia ufisadi kama Wakenya. Ufisadi na njia ya mkato ya kutafuta pesa haifai kwa uchumi wa taifa hili. Haya ni baadhi ya mambo ambayo marehemu Kabage alipigania sana na lazima tutimize kama tunataka kumuenzi,” akasema Bw Odinga.

Ukabila

Kinara huyo wa upinzani vilevile aliwataka Wakenya waache ukabila na kuishi kwa pamoja kama kaka na dada.

“Tunatakikana tujenge taifa lenye umoja hivi kwamba Mkenya anaweza kutoka hapa na kwenda kuishi Lamu na mwingine akatoka hapa na kwenda kuishi kwingine bila kuulizwa kama anatoka wapi. Hilo ndilo taifa ambalo tunataka,” akasema Bw Odinga

Wengine waliohudhuria mazishi hayo walikuwa ni pamoja na Naibu wa Rais William Ruto, kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, maseneta, mawaziri na wabunge.

Viongozi wote walioongea walimtaja Bw Kabage kuwa Mkenya ambaye alijitolea katika kila nyanja na alitoa mchango mkubwa katika uchumi wa taifa hili.