Uhuru sasa awategemea Raila, Kalonzo na Mudavadi kuvumisha BBI mlimani

Uhuru sasa awategemea Raila, Kalonzo na Mudavadi kuvumisha BBI mlimani

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta amezindua mkakati mpya wa kisiasa kuwafikia wenyeji wa Mlima Kenya, kwa kuwatumia wandani wake kupitia kituo cha redio na televisheni cha Kameme.

Kwenye mahojiano hayo, wandani hao wamekuwa wakiwarai wenyeji kuunga mkono ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), wakisema ni wao watakaofaidika zaidi kutokana na mapendekezo yake iwapo itapitishwa na Wakenya.

Vituo hivyo viwili vinahusishwa na familia ya Rais Kenyatta.

Vigogo hao ni kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, kiongozi wa Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee, Bw David Murathe, na kinara wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka ambaye alihojiwa jana.

Rais Kenyatta ndiye alikuwa wa kwanza kuhojiwa na vituo hivyo mnamo Januari 18.

Kinyume na mahojiano ya vigogo wenzake, Rais Kenyatta alihojiwa kwa pamoja na vituo vinne vikubwa vya redio vinavyopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Gikuyu. Vituo hivyo ni Kameme FM, Inooro FM, Coro FM na Gukena FM.

Kwenye mahojiano hayo ambayo yalidumu muda wa saa moja na nusu, Rais aliwasisitizia wenyeji kuwa BBI ndiyo njia ya pekee ambayo itawasuluhishia changamoto zinazowakumba.

Vile vile, alitumia mahojiano hayo kumshambulia vikali Naibu Rais William Ruto na wanasiasa wa mrengo wa ‘Tangatanga’, akiwataja kuwa kikwazo katika juhudi za kuleta umoja na uthabiti nchini.

“Chukueni kilicho chenu kwanza. Msikubali kupotoshwa kuhusu ahadi msiojua kama zitatimizwa baadaye. BBI ndiyo njia pekee itakayotuhakikishia tumepata mgao wa fedha tunaohitaji kisheria, hata ikiwa mmoja wetu hatakuwa uongozini,” akashauri Rais Kenyatta.

Siku mbili baada ya mahojiano ya Rais, Bw Mudavadi alihojiwa na kituo cha redio cha Kameme.

Kwenye mahojiano hayo, Bw Mudavadi alitoa ujumbe sawa na Rais Kenyatta, akiwarai wenyeji hao kuikumbatia BBI.

Ndizo kauli sawa zilizotolewa na Mabwana Odinga, Murathe na Musyoka.

Kutokana na mkakati huo mpya, wadadisi wanasema Rais ameegemea matumizi ya kituo hicho, kwani wandani wake wako huru kueleza hisia zao bila kuogopa kuwa chini ya masharti fulani.

Kulingana na Prof Macharia Munene ambaye ni mdadisi wa siasa, hatua ya Rais Kenyatta kuwahutubia wenyeji kwa kutumia vituo hivyo kulikuwa “kuzindua” kampeni za kuipigia debe BBI kwenye ngome yake.

Anasema mwanzo rasmi wa kampeni hizo ulikuwa kuandaliwa kwa kikao cha Sagana, Kaunti ya Nyeri, ambacho kilifanyika kati ya Ijumaa na Jumapili.

“Ingawa ni kawaida kwa wanasiasa kutumia vyombo vya habari kuwafikia wafuasi wao, Rais Kenyatta anatumia kituo cha Kameme kama mojawapo ya njia nyingi kuhakikisha ripoti ya BBI imepita. Sababu kuu ni kuwa ripoti hiyo ni mradi wake,” akasema Prof Munene.

Vile vile, aliongeza kuwa lengo la kuwatumia waandani wake ni kuondoa dhana miongoni mwa wenyeji kwamba ripoti hiyo ni njama ya kumkweza kiongozi fulani mamlakani.

Wakosoaji wa Rais Kenyatta wamekuwa wakidai kuwa ripoti hiyo ni mpango fiche wa “kumtengenezea njia” Bw Odinga kuwania urais 2022.

Wabunge wa ‘Tangatanga’ wamekuwa wakimlaumu Rais kwa kuwashinikiza viongozi kuunga mkono ripoti, ilhali kuna masuala muhimu yanayowaathiri wenyeji kama kudorora kwa sekta ya kilimo.

Baadhi ya viongozi ambao wamejitokeza kuipinga ripoti hiyo ni kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua, aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri kati ya wengine.

You can share this post!

Joho ashauriwa kuhusu urais 2022

Siasa za Raila, UhuRuto zatishia amani