Uhuru sasa kuzuru Ukambani

Uhuru sasa kuzuru Ukambani

Na CHARLES WASONGA

IKULU ya Rais sasa inasema kuwa ziara ya Rais Uhuru Kenyatta katika eneo la Ukambani itajikita katika ukaguzi wa miradi ya maendeleo pekee na sio mikutano ya hadhara kutokana na janga la Covid-19.

Kwenye taarifa iliyotumwa na msemaji wa Ikulu Kanze Dena kwa vyombo vya habari, Jumanne, mabadiliko hayo yamefikiwa kufuatia mkutano wa mashauriano kati ya viongozi kutoka kaunti za Machakos, Makueni na Kitui.

Viongozi hao walisema wanatambua kuwa maambukizi ya virusi vya corona yameongezeka nchini Kenya na katika mataifa mengi ya Afrika na ipo haja ya tahadhari kuchukuliwa kuzuia hali hiyo nchini.

“Kwa kuzingatia hali ilivyo nchini na kulingana na Agizo la kuzuia kuenea kwa Covid-19 linalozuia mikutano ya hadhara nchini, mkutano huo umeamua kupunguzwa kwa shughuli wakati wa ziara ya Rais.

“Kwa hivyo, tungeweza kutangaza kuwa Rais atafanya ziara katika eneo la Ukambani kukafua miradi ya maendeleo pekee na wala hatahutubia mikutano ya hadhara. Ataandamana na viongozi wote wa eneo hilo,” ikaeleza taarifa hiyo kutoka Ikulu ya Nairobi.

Hata hivyo, mkutano huo utafanyika katika tarehe ambazo zitatangazwa baadaye.

Mnamo Jumatatu, Ikulu ilitangaza kuahirishwa kwa ziara ya siku mbili ya Rais Kenyatta katika eneo la Ukambani kuanzia Jumanne Julai 6, 2021 hadi Julai 7, 2021 kwa kile ambacho Ikulu ilitaja ni “janga la Covid-19”.

Mkutano huo wa mashauriano baina ya viongozi wa Ukambani uliofanyika Jumanne, ulihudhuriwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Gavana wa Kitui Charity Ngilu, mwenza wa Machakos Afred Mutua, maseneta; Mutula Kilonzo Junior (Makueni), Enock Wambua (Kitui), Agnes Kavindu (Machakos) na Naibu Gavana wa Makueni Adelina Mwau miongoni mwa wengine.

You can share this post!

TAHARIRI: Saba Saba iende mbali, isirudi tena

FAUSTINE NGILA: Wapi utekelezwaji wa Ripoti ya Blokcheni?