Habari

UhuRuto, Raila watakumbatia ‘Punguza Mizigo’?

July 20th, 2019 4 min read

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA wanasubiri kuona ikiwa Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga wataunga kura ya maamuzi ya Punguza Mizigo ambayo imeanza kupata upinzani kutoka kwa baadhi ya wabunge na makundi ya kutetea haki za wanawake.

Washirika wa wanasiasa hao ambao wamekuwa wakilumbana kuhusu kura ya maamuzi wametoa hisia tofauti kuhusu mswada huo.

Kiongozi wa wengi katika Seneti, Kipchumba Murkomen na mwenzake katika bunge la kitaifa Aden Duale ambao ni washirika wa Dkt Ruto wametofautiana kuhusu mswada huo.

Bw Murkomen alisema Seneti itaupitisha naye Bw Duale akasema Bunge la Kitaifa litaukataa.

Wadadisi wanasema juhudi za chama cha Thirdway Alliance za kutaka katiba irekebishwe kupunguza gharama ya kuendesha serikali, haziwezi kufurahisha wabunge ambao Dkt Ruto na Bw Odinga hutegemea kuendeleza ajenda zao za kisiasa.

Wanasema kwamba baadhi ya mapendekezo ya chama hicho kinachoongozwa na wakili Ekuro Aukot hasa kutaka kupunguza idadi ya wabunge na kufuta nyadhifa za wawakilishi wa wanawake zitawakera wanasiasa.

Wabunge hasa wa chama cha ODM, tayari wamepuuza juhudi za Bw Aukot wakisema kwamba hazitafaulu na wadadisi wanasema ni kwa sababu mapendekezo yake yanatofautiana na msimamo kiongozi wa chama hicho kuhusu kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu.

ODM kinachoongozwa na Raila Odinga, kinataka wadhifa wa waziri mkuu na manaibu wawili ubuniwe pendekezo ambalo Bw Aukot anasema ni kuongezea Wakenya mzigo wa kuendesha serikali.

Kulingana na mwenyekiti wa chama hicho John Mbadi, wabunge hawataunga kampeni ya Punguza Mzigo kwa sababu haikutokana muafaka wa wanasiasa kama Kamati ya Maridhiano ambayo inaendelea kukusanya maoni kutoka kwa umma.

Kamati hiyo iliundwa na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kufuatia muafaka wao wa Machi 9 2018 maarufu kama handisheki.

Miongoni mwa mapendekezo ambayo yametolewa kwa kamati hiyo ni kura ya mageuzi kubuni wadhifa wa waziri mkuu na manaibu wawili.

Bw Mbadi alitaja mswada wa Dkt Aukot kama maoni ya mtu binafsi na kukosoa pendekezo la kupunguza idadi ya wabunge.

Kufikia sasa, ODM hakijawasilisha maoni yake kwa BBI japo wanachama wake wakiongozwa na Bw Odinga wamekuwa wakipigia debe kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu na manaibu wawili.

Hata hivyo katiba inaruhusu Mkenya kuwasilisha mswada wa kubadilisha katiba mradi tu atimize mahitaji ya kisheria ikiwa ni pamoja na kuungwa na wapigakura wasiopunguza 1 milioni.

Baadhi ya wanasiasa wanahisi kwamba Dkt Aukot angesubiri ripoti ya BBI imalize kazi yake ya kukusanya maoni kutoka kwa Wakenya ili mapendekezo yake yashirikishe maoni ya wengi.

“Aliharakisha mchakato huu, angesubiri ripoti ya BBI kwa sababu itakuwa na maoni ya wengi. Ushirikishi ni muhimu katika kubadilisha katiba,” alisema mbunge maalamu Godfrey Osotsi.

Kwenye mapendekezo yake, Dkt Aukot anataka nafasi za wabunge wa kuteuliwa zipunguzwe kutoka 12 hadi sita hatua ambayo wadadisi wanasema itakuwa ni sawa na kubagua baadhi ya makundi katika jamii kama vile walemavu na vijana.

BBI

Kulingana na mchanganuzi wa siasa, Stephen Wafula, kuna uwezekano kwamba mapendekezo ya Thirdway Alliance yataainishwa na ya kamati ya BBI katika mswada ambao utawasilishwa kwa Wakenya kwenye kura ya maamuzi.

Mwandani mmoja wa Dkt Ruto anasema ni mswada utakaowasilishwa kwa umma ambao utamfanya atangaze msimamo wake kuhusu mageuzi ya katiba.

“Kwa sasa tuna maoni ya watu mbali mbali ambayo wametoa katika majukwaa tofauti ikiwa ni pamoja na BBI na hata Punguza Mizigo. Hata hivyo, kama kiongozi wa kitaifa na Mkenya mwenye haki ya kutoa maoni, wakati ukifika Naibu Rais ataeleza msimamo wake kamili kuhusu yatakayowasilishwa,” alisema mwanasiasa huyo aliyeomba tusitaje jina lake kwa sababu sio msemaji rasmi wa Dkt Ruto.

Kwa kuwa Thirdway Alliance kinapendekeza mfumo utakaohakikisha gharama ya kuendesha serikali itapungua pakubwa, Wakenya wanasubiri kuona iwapo Naibu Ruto ambaye amekuwa akipuuza wito wa kubadilisha katiba ataunga mkono mapendekezo hayo.

Kulingana na Dkt Ruto, badala ya kubuni wadhifa wa waziri mkuu, wadhifa wa kiongozi rasmi wa upinzani bungeni unapaswa kurejeshwa ili ushikiliwe na anayeibuka wa pili kwenye uchaguzi wa urais.

Dkt Ruto anamezea mate urais na kulingana na Dkt Aukot, Rais anapaswa kuhudumu kwa kipindi kimoja cha miaka saba pekee na kustaafu.

Rais Kenyatta pia amekuwa akilalama kwamba gharama ya kuendesha serikali iko juu na imenyima Wakenya pesa za maendeleo.

Baadhi ya wadadisi wanasema pendekezo hili linaweza kumpatia Rais Uhuru Kenyatta nafasi ya kuendelea kutawala hadi 2029 likipitishwa kwenye kura ya maamuzi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Sidhani kwamba Dkt Ruto na washirika wake wa kisiasa wanaweza kukubali mpangilio kama huu kwa sasa kwa sababu unaweza kuchelewesha ndoto yake ya kuwa rais. Kwa sababu hii anaweza kukosa kuchangamkia mapendekezo ya Dkt Aukot,” asema mdadisi wa masuala ya kisiasa, George Airo.

Hata hivyo, Seneta wa Kaunti ya Nandi Samson Cherargei – mwandani mwingine wa Dkt Ruto – anasema ataunga mswada unaonuia kupatia seneti mamlaka makubwa.

Kulingana na Bw Charargei, baadhi ya mapendekezo ya Dkt Aukot ni sawa na yaliyopendekezwa na seneti.

Bw Airo anasema japo mapendekezo ya Dkt Aukot yanalenga kupunguzia Wakenya gharama ya kuendesha serikali, ni sumu kwa wanasiasa hasa wabunge wanaohisi kwamba yataathiri ushawishi na umaarufu wao.

Chama hicho kinapendekeza Rais awe akihudumu kwa kipindi kimoja cha miaka saba tofauti na sasa ambapo katiba inamruhusu kutetea kiti chake kwa kipindi cha pili cha miaka mitano.

Kwenye kampeni yake maarufu kama Punguza Mizigo, Dkt Aukot anapendekeza seneti ikabidhiwe mamlaka zaidi kuliko bunge la kitaifa.

Dkt Aukot anasema kwamba chama chake kinalenga kupatia ugatuzi nguvu zaidi, kuhakikisha usawa wa jinsia, kurahisisha urais, kupunguza gharama ya kuendesha serikali, kuhakikisha kuna uadilifu na kupunguza gharama ya kufanya uchaguzi nchini.

Watu kadhaa, mashirika na wanasiasa wamekuwa wakitoa mapendekezo yao kwa Kamati ya Maridhiano (BBI) kuhusu sehemu za katiba wanazotaka zirekebishwe.

“Ukifuatilia mapendekezo yanayowasilishwa mbele ya kamati ya maridhiano ambayo ina baraka za viongozi wakuu wa kisiasa nchini Rais Kenyatta na Raila Odinga, utagundua kwamba yanatofautiana na ya Dkt Aukot. Kwa msingi huu, kuna uwezekano wa mapendekezo yake, japo yanalenga kumfaidi mlipa ushuru yakapingwa kutokana na ushawishi wa viongozi,” aeleza Bw Airo.