HabariSiasa

UhuRuto warejelea 'urafiki' wao

June 1st, 2020 2 min read

CHARLES WASONGA na SAMMY WAWERU 

RAIS Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto Jumatatu walijizatiti kuonyesha kuwa ukuruba kati yao ungalipo walipovalia mavazi yanayofanana wakati wa maadhimisho ya Sherehe za 57 za Siku Kuu ya Madaraka Dei.

Kutokana na janga la ugonjwa hatari wa Covid-19 sikukuu hiyo ya kitaifa iliadhamishwa kwa namna ya kipekee katika Ikulu ya Nairobi ambapo ilihudhuria na wageni wachache waalikwa.

Licha ya uwepo wa uhasama kati ya vinara hao wawili wa Jubilee na ambao umepelekea Rais Kenyatta kuwapokonya wandani wa Dkt Ruto nyadhifa za uongozi katika seneti, Jumatatu wawili hao walionekana wakicheka pamoja.

Isitoshe, walikuwa wamevalia mavazi yanayofanana; suti nyeusi, shati nyeupe, viatu vyeusi na tai nyekundu.

Wakenya walishangazwa na mavazi ya Rais Kenyatta pamoja na Dkt Ruto wengi wakisema haikuwa sadfa bali ni jambo ambalo walipanga. Lengo hapa lilikuwa kuonyesha umma kwamba “bado tuko pamoja kama zamani” licha ya uhasama unaotokota ndani ya Jubilee.

Licha ya uhusiano wa Rais na Naibu Rais kuonekana kuwa na doa, picha ya wawili hao wakipiga gumzo na kuzua ucheshi imezua mdahalo mkali mitandaoni.

“Inachanganya kama hesabu ya wagonjwa wa Covid – 19. Kuna waliopata afueni na kupona na maafa kadhaa kuripotiwa, ila hesabu ni ileile haipunguzi,” Franklin Omwembula akaeleza kwenye mtandao wa Facebook.

Wawili hao kuonekana pamoja wakizungumza na kucheka Ikuluni, wachangiaji wa mitandao wanahoji ni kitendawili kisichokuwa na mteguzi, isijulikane walichokuwa wakijadili. “Ni mtihani usio na majibu. Niliacha kuunga yeyote mkono kwa kuwa utapata mshtuko wa moyo bure tu,” Wilson Kimuyu akachangia.

Kulingana na Esther Wangari, wanasiasa nchini hawana msimamo na si maadui, akishauri Wakenya kupevuka na kufumbua macho, wawe na hekima na kudumisha amani kila wakati.

Katika hotuba ya Naibu Rais katika maadhimisho ya Madaraka Dei 2020, Dkt Ruto alieleza kuwa na Imani na serikali ya Jubilee chini ya kigogo wake Rais Uhuru Kenyatta, hasa katika mikakati iliyowekwa kufanya maendeleo na pia kuangazia janga la corona. Baada ya kumkaribisha Rais, Rais Kenyatta alitambua kuwepo kwa Dkt Ruto, “Asante William”.

Wakati akihitimisha hotuba yake, huku akisihi wananchi kuzingatia mikakati na taratibu zilizotolewa na wizara ya afya kuzuia msambao wa Covid – 19, Rais Kenyatta alisisitiza maelezo ya Ruto akimtaja “vile Naibu wa Rais amesema” katika mchakato wa kudhibiti maenezi.

Baadhi ya Wakenya wanahisi, viongozi hao wanajua mahesabu wanayocheza. “Hawa watu huwa pamoja. Baba (akimaanisha Raila Odinga) hana bahati,” Khadasia Mavindi, akachangia akitoa hisia zake kuhusu picha ya Rais na Naibu wake kuonekana wakitangamana na kuzua ucheshi.

“Sote tunataka kuona Kenya iliyoungana. Wanaoshabikia utengano wakome, tuungane tufanye maendeleo,” Elijah Ndirangu akaeleza, Festus Mutwol akiongeza kuwa viongozi hao wawilili wanapaswa kuonyesha umoja wa aina hiyo ili Kenya isonge mbele kimaendeleo.

Baada ya gumzo, Rais Kenyatta na Naibu wake waliandamana na kuingia Ikulu.

Itakumbukuwa kuwa ni wakati wa muhula wa kwanza wa uongozi wa Jubilee ambapo wawili hao walipenda kujitokeza katika Ikulu wakiwa wamevalia mavazi yanayofanana, haswa Rais alitoa tangazo muhimu kwa taifa.

Lakini kuanzia mapema mwaka huu, imekuwa nadra zaidi kwa Rais Kenyatta na Dkt Ruto kuonekana hadharani pamoja. Isitoshe, inasemekana kuwa Naibu Rais amekuwa akikosa kuhudhuria baadhi ya mikutano ya Baraza la Kitaifa la Usalama (NSC) kuzunguzia suala la Covid-19.

Mnamo Aprili mwaka huu Naibu Rais alisema kuwa yeye na Rais hawapasi kuwa pamoja, wakati mmoja, kwa sababu ni “hatari kwa usalama,” kutokana na janga la Covid-19.

Lakini Jumatano katika Ikulu ya Nairobi Rais Kenyatta na Dkt Ruto walikaa katika jukwaa moja japo kwa umbali wa mita moja na nusu, kulingana na kanuni ya kuzuia kuenea kwa maambukizi ya Covid-19.

Akasema Dkt Ruto: “Chini ya uongozi wako, serikali itachukua hitajika ya kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu huku tukijiandaa mwelekeo mpya wa maisha.”