UhuRuto wazua wasiwasi

UhuRuto wazua wasiwasi

Na WANDERI KAMAU

TOFAUTI za kisiasa na majibizano ya hadharani kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto zimetajwa kuwa tishio kwa amani na uthabiti wa kitaifa.

Wanaharakati, wanasiasa na wananchi waliozungumza na ‘Taifa Leo’ Jumatano walieleza hofu kuwa Rais Kenyatta na Dkt Ruto wanaweza kuitumbukiza Kenya katika hali sawa na ilivyokuwa kwenye uchaguzi wa 2007, ambapo mamia walikufa na maelfu wakapoteza makao.

Rais Kenyatta na Dkt Ruto ndio waliokuwa washukiwa wakuu wa ghasia hizo na walishtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) lakini kesi zao zikaporomoka.

Wadadisi wa siasa wanasema kiini cha kuungana kwa wawili hao ni ghasia za 2007 baada ya kushtakiwa katika ICC, lakini sasa wanaonekana kutojali. Wanasema ni hali inayoweza kuirejesha Kenya katika hali sawa na hiyo.

Aliyekuwa kiongozi wa Kanisa la Christ Is The Answer Ministries (CITAM) nchini, Dkt David Oginde, alisema ni wakati wawili hao wafahamu wanaubeba mustakabali wa Kenya mikononi mwao na vitendo vyao vitaamua mwelekeo wa nchi.

“Inasikitisha kumwona Rais na naibu wake wakijibizana peupe bila kufahamu hali zilizochangia wao kuungana. Wakati umefika kwao kutathmini athari za ndimi zao, hasa wakati huu nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwingine,” akasema Dkt Oginde.

Aliyekuwa mbunge wa Mukurwe-ini, Kabando wa Kabando, ambaye pia ni mwanaharakati wa kisiasa, anasema majibizano hayo yanazua taswira kama kuwa uchaguzi wa 2022 ni wa kufa kupona kwa Wakenya.

“Ingawa ni kawaida siasa kushika kasi wakati wa urithi, uchaguzi wa 2022 ni tofauti sana na ilivyokuwa 1978 wakati marehemu Daniel Moi alikuwa akichukua uongozi baada ya kifo cha Mzee Kenyatta na 2002, wakati Rais Mstaafu Mwai Kibaki alichukua uongozi kutoka kwa Bw Moi. Msingi wa utawala wa UhuRuto umekuwa ni mashtaka yaliyowakabili katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC),” akasema Bw Kabando.

Rais Kenyatta na Dkt Ruto wanalaumiwa kwa kuwasaliti Wakenya, wakati wanapitia hali ngumu za kiuchumi kutokana na athari za janga la virusi vya corona.

Tangu walipochukua uongozi mnamo 2013, utawala wa UhuRuto umeandamwa na maovu kama sakata za ufisadi, kuwatoza Wakenya ushuru wa juu, uongezeko la deni la kitaifa, ukosefu wa usalama kati ya changamoto nyingine nyingi.

Serikali ya UhuRuto pia imekuwa ikilaumiwa kwa kuendeleza ubomozi katika katika sehemu mbalimbali nchini, hivyo kuwaathiri maelfu ya wafanyabiashara wadogo wadogo, licha ya kuahidi kuwainua kiuchumi.

Kwenye sakata hizo, Wakenya wamepoteza mabilioni ya pesa, huku washukiwa wakuu wakikosa kuchukuliwa hatua zozote au kesi zao kucheleweshwa katika hali tatanishi.

Baadhi ya sakata hizo ni wizi wa fedha zilizokusudiwa kujenga mabwawa ya Arror na Kimwarer, juhudi za kukabiliana na makali ya virusi vya corona kati ya sakata zingine.

Deni la kitaifa pia limekuwa likiongezeka karibu kila mwaka, kwa sasa likikisiwa Sh8 trilioni.

Kwenye mahojiano jana, kiongozi wa chama cha Narc-Kenya, Martha Karua alisema wakati umefika kwa Rais Kenyatta kuungana na Dkt Ruto ili kutimiza ahadi walizotoa kwa Wakenya wakati wa kampeni zao mnamo 2013.

Anasema kuwa kuharamishwa kwa Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI) hakupaswi kuwa chanzo chao kuvutana, lakini wanapaswa kuungana tena kuhakikisha wametimiza Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.

Mwanaharakati Mutemi wa Kiama kutoka vuguvugu la Linda Katiba anasema UhuRuto wamesahau msingi uliowaunganisha mara tu walipopata mamlaka.

“Malumbano yanayoendelea baina yao ni dhihirisho la wazi wanavutania maslahi yao wenyewe wala hawawajali Wakenya. Wamepofushwa na mamlaka kiasi cha kusahau hali zilizowafanya kuumgana,” asema Bw Kiama.

Kasisi Sammy Wainaina wa All Saints Cathedral, Nairobi, anasema wawili hao ndio wataubeba msalaba ikiwa kuna damu yoyote itamwagika 2022 kutokana na kutojali kwao.

“Viongozi wanapaswa kufahamu wanawajibikia lolote litokeapo nchini. Wanapaswa kuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha nchi imeungana badala ya kuendeleza migawanyiko,” asema.

Hata hivyo, washirika wa viongozi hao wawili wanalaumiana baina yao, kila mmoja akiutetea mrengo wake.

Mbunge Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini) anamlaumu Dkt Ruto kwa “kuanza uchokozi dhidi ya Rais” kwa kupinga ajenda za serikali ambayo anahudumu.

 

Hata hivyo, mbunge Nelson Koech (Belgut) anataja kiini cha mzozo kati viongozi hao kuwa mtindo wa Rais kumtenga Dkt Ruto, licha yake (Ruto) kuchangia pakubwa ushindi wa serikali ya Jubilee katika chaguzi kuu za 2013 na 2017.

“Ni kinaya kuwa Rais amekuwa akitumia washirika wake wa karibu kama Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe, Katibu Mkuu Raphel Tuju kati ya wengine kuendeleza dhuluma za wazi dhidi ya kiongozi ambaye alichagia zaidi ya nusu za kura alizopata. Ni wakati Rais afahamu kuwa Dkt Ruto si kiongozi aliyeteuliwa bali mshirika sawa waliochaguliwa pamoja naye,” akaeleza Bw Koech.

Wananchi waliozungumza na ‘Taifa Leo’ walisema ni wakati viongozi hao kufahamu kuwa wananchi ndio watakaoumia kutokana na majibizano yao.

“Maombi ya Wakenya kwa Rais na naibu wake ni kufahamu kuwa walichaguliwa na wananchi ili kuwafanyia kazi na kutimiza ahadi zao. Wanapaswa kushirikiana pamoja kwa miezi michache iliyopita ili kutimiza ahadi walizotoa,” asema Bi Stela Saru, kutoka Maseno, Kaunti ya Kisumu.

Bi Felistas Ndonyi kutoka Kaunti ya Machakos anasema wawili hao wanapaswa kujua wao ni kama mume na mkewe, na wanatazamwa na Wakenya wote kama watoto wao.

“Wakati wazazi wanapogombana na hatimaye, watoto wao ndio huteseka. Vivyo hivyo, viongozi hao wanapaswa kufahamu Wakenya ndio wanaoendelea kuteseka wanaporushiana cheche za maneno,” akasema Bi Ndonyi.

You can share this post!

Kingi apuuzilia mbali shinikizo kumtaka ajiunge na Ruto

Bayern Munich wasagasaga Bremer SV kwa mabao 12-0 katika...