Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uhusiano wa Isimu na taaluma nyinginezo

February 23rd, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

KWA mujibu wa maelezo ya wataalam kuhusu dhana ya isimu, ni bayana kwamba isimujamii ni taaluma mojawapo ya isimu inayochunguza namna lugha inavyotumika katika jamii anuwai na uhusiano baina yake.

Tawi la isimujamii huchunguza matumizi ya lugha katika mazingira tofauti, aina mbalimbali za lugha na mazingira yake pamoja na uhusiano wa lugha na utamaduni wa jamii inayoitumia.

Hata hivyo, ni vyema kuelewa kwamba bila kuwepo kwa jamii hakuna lugha na bila kuwepo kwa lugha hakuna jamii.

Hii ni kumaanisha kwamba lugha na jamii hukamilishana ili kukidhi haja za mawasiliano.

Isimu ni taaluma pana na kutokana na hali hii inaoana na kuingiliana na taaluma nyinginezo jinsi ifuatavyo:

Isimu na Sosholojia

Sosholojia ni  taaluma inayoshughulikia uchunguzi na uchanganuzi wa matabaka na makundi ya watu katika jamii.

Kuna makundi tofautitofauti katika jamii kwa mfano: matabaka ya wanaojimudu kifedha na tabaka la wachochole, tabaka la watawala na wanaotawaliwa na kadhalika.

Uhusiano unaojitokeza baina ya isimujamii na isimu sosholojia ni kwamba katika jamii kuna tabaka mbalimbali na kila tabaka lina namna tofauti tofauti ya kutumia lugha kulingana na mazingira. Kwa mfano vijana wana lugha wanayotumia ambayo ni tofauti na lugha inayotumiwa na wazee.

Vilevile, tabaka la wasomi lina lugha tofauti inayotumika na kueleweka baina yao.

Hivyo basi, ni muhimu kwa mwanaisimu yeyote yule kuyafahamu vyema matabaka yaliyo katika jamii yake na jinsi lugha inavyotumika katika matabaka hayo.

Isimujamii na Anthropolojia

Anthropolojia  ni taalama inayohusisha kuchunguza mila na desturi za jamii fulani na jinsi zinavyotumika katika maisha yao ya kila uchao.

Uhusiano wa isimujamii na isimu anthropolojia ni kuwa matumizi ya lugha katika jamii huambatana na mila na desturi zilizomo katika jamii ili kutumia lugha ambayo hujitokeza katika msamiati wa lugha husika.

Kwa mfano, katika jamii yenye utamaduni wa upashaji tohara na ukeketaji, kuna msamiati wa kurejelea kwa aliyetahiriwa na yule ambaye bado hajapitia hatua hiyo.

Hali hii ni tofauti na jamii ambazo hazina utamaduni.

Hivyo basi baadhi ya maeneo lugha inamotumika katika mazingira fulani huonekana ya kawaida ilhali katika mazingira mengine huonekana kama ukiukaji wa kaida za jamii husika.

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Msanjila, Y. P. (1990). “Problems of Teaching Through the Medium of Kiswahili in Teacher Training Colleges in Tanzania”. Journal of Multilingual and Multicultural Development II/4:307 – 318

Mtembezi, I. J. (1997). “Njia Mbili Zilimshinda Fisi: Tanzania na Suala la Lugha ya Kufundishia”. Dar es Salaam: BAKITA.

Mulokozi, M. M. (1991). “English versus Kiswahili ni Tanzania’s Secondary Education”. Swahili Studie Ghent.