UIGIZAJI: Lynn aamini hatua moja baada ya nyingine itamfikisha kileleni

UIGIZAJI: Lynn aamini hatua moja baada ya nyingine itamfikisha kileleni

Na JOHN KIMWERE

LYDIA Adhiambo Owino ni miongoni mwa wasanii chipukizi wanaopania kutinga upeo wa kimataifa miaka ijayo katika tasnia ya uigizaji.

Ingawa hajapiga hatua kubwa katika jukwaa la maigizo, mwanadada huyu anayefahamika kama Lynn amesema, ”Tangu nikiwa mtoto nilitamani kuhitimu pengine kuwa mwimbaji, mwanahabari au mwigizaji.”

Mbali na uigizaji, yeye hufanya kazi ya mauzo katika kampuni ya simu ya Safaricom kitengo cha Home Fibre.

Binti huyu akiwa akiwa mdogo alipenda sana kutizama msanii mcheshi, Vicky Vike maarufu ‘Awinja’ aliyekuwa akishiriki kipindi cha Papa Shirandula.

Kipindi hicho kilikuwa kinapeperushwa kupitia Citizen TV.

Anadokeza kuwa anataka kujijenga kisanaa akilenga kutinga upeo kimataifa miaka ijayo. Anasema kuwa ana imani kubwa kuwa ndio anaanza kupiga ngoma lakini ipo siku kazi yake itakapokubalika na wanaomchekelea.

”Ninaamini nina kipaji cha kufanya kweli katika masuala ya uigizaji ingawa ninaelewa bayana kuwa shughuli sio mteremko. Ingawa sikufanikiwa kusoma hadi chuo kikuu kama nilivyotarajia niliamua kujiunga na uigizaji pia vichekesho ili kutimiza ndoto yangu,” akasema.

Ameshiriki maigizo ndani ya miaka miwili ambapo amefanya kazi na makundi kadhaa ambayo huonyesha kazi zao kupitia mtandao wa YouTube ikiwamo Stateman Media, Glighlakes Production na Love to Laugh Comedy.

Kisura huyo anajivunia kushiriki vipindi viwili vya kuigiza: ‘Kortini’ na ‘Perfect Match’ ambavyo hupeperushwa kupitia Ebru TV.

Kwa waigizaji wa Afrika Mashariki dada huyu anasema huvutiwa na kazi zake msanii wa Bongo, Wema Sepetu anayejivunia kushiriki filamu kama ‘Kisogo,’ ‘More than a women,’ ‘Heaven sent,’ na ‘Day after a Death’ na nyinginezo.

Pia hupendezwa na kazi zake mchekeshaji mahiri mzawa wa Uganda, Anne Kansiime.

Anaamini kuwa wasanii wa Kenya wakipata ufadhili wanatosha mboga kufanya kazi nzuri na kuvutia wapenzi wa burudani na kugeukia filamu za waigizaji wazalendo.

Serikali

Anakariri kwenye juhudi za kuinua uchumi wa taifa hili, serikali inapaswa kutenga fedha kusaidia waigizaji chipukizi maana wakishikwa mkono vizuri wana uwezo wa kuibuka mastaa miaka ijayo.

”Taifa hili limefurika wasanii wengi tu wanaume na wanawake wanaohitaji sapoti ili kukuza vipaji vyao katika tasnia ya maigizo,” anasema.

Lydia Adhiambo Owino almaarufu ‘Lynn’.┬áPicha/John Kimwere

Ushauri

Anashauri wasichana waliopata ujauzito wakiwa na umri mdogo kamwe wasikate tamaa bado wana nafasi ya kujirekebisha na kuishi maisha mema.

Anadokeza kuwa pia jamii inapaswa kuwaonesha mapenzi wala sio kuwaponda kama waliokosea.

Anasema hawezi kuweka katika kaburi la sahau akiwa na umri wa miaka 16 alilia sana alipopata ujauzito na mpenzi wake kusepa.

Anawataka waigizaji chipukizi hapa nchini waache kubaguana bali waige mtindo wa wenzao katika mataifa yanayoendelea kama Nigeria na Afrika Kusini ambao kila msanii husapoti mwenzie.

You can share this post!

Talaka ya NASA yakamilika sasa chama cha ODM kikijiondoa

BKPL: Mathare United kuwinda alama tatu