KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uingereza na Amerika waambulia sare tasa katika mechi ya Kundi B uwanjani Al Bayt

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uingereza na Amerika waambulia sare tasa katika mechi ya Kundi B uwanjani Al Bayt

Na MASHIRIKA

UINGEREZA walipoteza nafasi ya kuwa kikosi cha kwanza kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya Kombe la Dunia mwaka huu baada ya kuambulia sare tasa dhidi ya Amerika katika mchuano wao wa pili wa Kundi B ugani Al Bayt mnamo Ijumaa usiku.

Masogora wa kocha Gareth Southgate walishuka dimbani wakipigiwa upatu wa kutandika Amerika baada ya kupokeza Iran kichapo cha 6-2 katika pambano la ufunguzi wa Kundi B mnamo Novemba 21, 2022 uwanjani Khalifa International.

Amerika walianza mechi kwa matao ya juu na wakapoteza nafasi nyingi za wazi kupitia kwa Weston McKennie na Christian Pulisic waliomtatiza pakubwa beki Harry Maguire katika safu ya nyuma ya Uingereza.

Mason Mount na Bukayo Saka nao walimshughulisha vilivyo kipa Matt Turner wa Amerika kabla ya nafasi ya Saka kujazwa na Marcus Rashford katika kipindi cha pili.

Licha ya sare, Uingereza almaarufu The Three Lions wanapigiwa upatu wa kufuzu kwa raundi ya muondoano ikizingatiwa kwamba watafunga kampeni za makundi kwa mechi dhidi ya Wales waliopepetwa na Iran 2-0 mapema Ijumaa. Amerika walitoshana nguvu na Wales kwa sare ya 1-1 katika mchuano wa kwanza wa Kundi B.

Licha ya kujivunia rekodi nzuri dhidi ya Amerika katika mashindano mengine, Uingereza waliwahi kupoteza mchuano wa Kombe la Dunia dhidi ya Amerika mnamo 1950 kisha kuambulia sare mnamo 2010 nchini Afrika Kusini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Mpango wa madereva na makondakta kupokea...

Hatutambui mkataba wa kusitisha vita – M23

T L