Uingereza na Ujerumani waambulia sare ya 3-3 katika Nations League uwanjani Wembley

Uingereza na Ujerumani waambulia sare ya 3-3 katika Nations League uwanjani Wembley

Na MASHIRIKA

UINGEREZA waliambua sare ya 3-3 dhidi ya Ujerumani katika pambano la mwisho la Kundi A3 kwenye Uefa Nations League mnamo Jumatatu usiku ugani Wembley.

Masihara ya kipa Nick Pope langoni mwa Uingereza katika dakika za mwisho wa mechi yaliwezesha Ujerumani kusawazisha kupitia kwa Kai Havertz aliyepachika wavuni mabao mawili katika gozi hilo.

Chini ya kocha Hansi Flick, Ujerumani walianza mechi kwa matao ya juu huku wakiwekwa kifua mbele na Ilkay Gundogan aliyefunga penalti iliyosababishwa na beki Harry Maguire aliyemchezea visivyo Jamal Musiala katika dakika ya 52. Havertz alifanya mambo kuwa 2-0 kunako dakika ya 67.

Uingereza waliokuwa wakikodolea macho kichapo cha tatu mfululizo walijinyanyua upesi kupitia kwa bao la Luke Shaw katika dakika ya 71. Mason Mount alijaza kimiani bao la pili kunako dakika ya 75 kabla ya nahodha  Harry Kane kufunga penalti ya dakika ya 83 baada ya Jude Bellingham kuangushwa na Nico Schlotterbeck ndani ya kijisanduku.

Pope aliyewajibishwa katika nafasi ya kipa Jordan Pickford alishindwa kudhibiti kombora la Serge Gnabry ambalo Havertz aliliwahi na kujaza wavuni. Sare dhidi ya Ujerumani ni msururu wa matokeo duni zaidi kwa Uingereza kuwahi kusajili tangu 1993.

Uingereza walishuka dimbani wakiwa tayari wameteremshwa ngazi kutoka kundi la vikosi vya haiba kubwa vya Nations League baada ya Italia kuwakomoa 1-0 mnamo Septemba 23, 2022 ugani San Siro, Milan.

Matokeo hayo yaliyoendeleza masaibu ya kocha Gareth Southgate ambaye sasa ameshuhudia kikosi chake kikikosa kushinda mechi yoyote kati ya sita zilizopita. Hiyo ni rekodi duni zaidi kwa Uingereza tangu Juni 2014.

Baada ya kuchapwa na Italia, walishuka hadi mkiani mwa Kundi A3, nyuma ya Ujerumani walioaibishwa na Hungary kwa kichapo cha 1-0 usiku wa Septemba 23, 2022.

Licha ya kuponda Italia 5-2 katika mkondo wa kwanza wa Nations League mnamo Juni, Ujerumani wamesuasua kwenye kipute hicho kwa kutoshinda mechi yoyote nyingine kati ya tano katika Kundi A3.

Kichapo kutoka kwa Hungary kilikuwa cha kwanza kwa Ujerumani kupokezwa tangu Uingereza iwazamishe 2-0 katika hatua ya 16-bora ya Euro 2020 miezi 15 iliyopita Aidha, masogora hao wa kocha Hansi Flick wameshinda mechi moja pekee kati ya saba tangu kivumbi cha Nations League kianzishwe. Uingereza walilazimishia Ujerumani sare ya 1-1 walipokutana katika mkondo wa kwanza wa Nations League jijini Munich mnamo Juni, 2022.

MATOKEO YA NATIONS LEAGUE (Jumatatu):

Uingereza 3-3 Ujerumani

Hungary 0-2 Italia

Gibraltar 1-2 Georgia

N. Macedonia 0-1 Bulgaria

San Marino 0-4 Estonia

Montenegro 0-2 Finland

Romania 4-1 Bosnia

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Uholanzi, Croatia zatinga 4-bora

Italia wakomoa Hungary jijini Budapest katika Uefa Nations...

T L