Uingereza waponda San Marino 5-0 katika mechi ya kuwinda tiketi ya Kombe la Dunia

Uingereza waponda San Marino 5-0 katika mechi ya kuwinda tiketi ya Kombe la Dunia

Na MASHIRIKA

UINGEREZA walianza kampeni zao za kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia kwa kusajili ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya San Marino katika mechi iliyowakutanisha uwanjani Wembley mnamo Alhamisi.

San Marino wanaoshikilia nafasi ya 210 kwenye orodha ya viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), walilemewa na Uingereza katika mechi hiyo licha ya kikosi hicho cha kocha Gareth Southgate kukosa huduma za nahodha Harry Kane katika kipindi cha kwanza.

Uingereza walikita kambi katika lango la wageni wao kwa takriban dakika zote 90 za mchezo na ambacho kocha Southgate alisema kilimsikitisha zaidi ni kwamba safu yake ya ushambuliaji ilikuwa butu.

Uingereza walikuwa bila washambuliaji Marcus Rashford, Mason Greenwood na Bukayo Saka. Nafasi zao zilitwaliwa na James Ward-Prowse aliyefungia Uingereza bao lake la kwanza pamoja na Ollie Watkins wa Aston Villa aliyekuwa akiwajibikia Uingereza kwa mara ya kwanza.

Bao la Ward-Prowse katika dakika ya 14 lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na beki Ben Chilwell wa Chelsea. Dominic Calvert-Lewin wa Everton alifanya mambo kuwa 2-0 kunako dakika ya 21 baada ya kukamilisha krosi ya Reece James wa Chelsea. Nyota huyo alipachika wavuni goli la tatu katika dakika ya 53 baada ya Raheem Sterling kufungia Uingereza goli jingine kunako dakika ya 31.

Uingereza wangalifunga mabao mengi zaidi katika kipindi cha pili ila wakanyimwa nafasi hizo na kipa wa San Marino, Elia Benedettini aliyepangua na kudhibiti vilivyo makombora mazito aliyoelekezewa na Chilwell, Mason Mount, Jesse Lingard na Ward-Prowse.

Uingereza kwa sasa wanajiandaa kutua mjini Tirana kuvaana na Albania katika mchuano wao ujao wa Kundi I mnamo Machi 28 kabla ya kualika Poland uwanjani Wembley siku tatu baadaye.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Rais Uhuru alionyesha heshima kubwa...

Kikwete amtunuka sifa Dkt Magufuli akieleza jinsi...