Uingereza yapiga marufuku wasafiri kutoka Burundi na Rwanda

Uingereza yapiga marufuku wasafiri kutoka Burundi na Rwanda

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

UINGEREZA imepiga marufuku wasafiri kutoka Burundi na Rwanda kuingia nchini humo katika juhudi za kuzuia aina mpya ya virusi vya corona.

Hatua hii inajiri wiki moja baada ya nchi hiyo kupiga marufuku wasafiri kutoka Tanzania na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC)

Serikali ya Uingereza inasema inalenga kuzuia aina mpya ya virusi vya corona iliyogunduliwa Afrika Kusini kupenya katika nchi hiyo.

Waziri wa Uchukuzi Grant Schapps alisema wasafiri kutoka Rwanda na Burundi hawataruhusiwa kuingia Uingereza kuanzia saa saba Ijumaa.

Raia wa Uingereza na Ireland na wa mataifa mengine walio na vibali vya kuishi nchi hiyo wataruhusiwa lakini ni lazima wajitenge kwa siku 10 wakiwa nyumbani.

Waziri Shapps alisema abiria wote ni lazima wathibitishwe walipimwa corona na wajaze fomu ya kuonyesha wanakoishi kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini humo.

Wanaokataa kufanya hivyo wanaweza kutozwa faini ya Sh60,000.

Wiki jana, serikali ya Rwanda ilifunga jiji kuu la Kigali kwa siku 15 katika juhudi za kuthibiti wimbi la pili la maambukizi ya corona.

Mapema mwezi huu wa Januari, Burundi ilifunga mipaka yake yote kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.

You can share this post!

Wambora achaguliwa mwenyekiti wa CoG

Biden aondoa marufuku ya Trump kuhusu uavyaji mimba