Ujasiri wa kipekee wa Mudavadi kura ya 2022 ikikaribia

Ujasiri wa kipekee wa Mudavadi kura ya 2022 ikikaribia

Na BENSON MATHEKA

Licha ya ngome yake ya eneo la Magharibi kuonekana kumponyoka, kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi anasonga mbele na kampeni yake akilenga kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Ingawa wadadisi wa siasa wanadai kwamba ana nafasi finyu sana kushinda kiti hicho ikizingatiwa hana ufuasi mkubwa kote nchini kama washindani wake wakuu wawili Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, makamu rais na naibu waziri mkuu huyo wa zamani ameonyesha ujasiri wa kuhakikisha kwamba jina lake litakuwa kwenye debe mwaka ujao.

Wiki hii, iliripotiwa kwamba ameagiza magari mapya ya kifahari ya kutumia katika kampeni zake za urais, akaanzisha ofisi ya kusimamia kampeni zake na akamteua Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja kuwa msimamizi wa kampeni zake.

Katika kile kinachoonyesha ujasiri na kutobanduka katika kinyang’anyiro cha kumrithi Rais Uhuru Kenyatta mwaka ujao, Mudavadi ameajiri washauri. Haya yanajiri wiki chache baada ya viongozi wa jamii ya Mulembe kumvua wadhifa wa msemaji wa jamii na kumtwika Katibu Mkuu wa Muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini Francis Atwoli wadhifa huo.

Atwoli ameonyesha wazi kuwa anamuunga mkono Bw Odinga.Imeibuka kuwa ujasiri wake unatokana na kuungwa mkono na baadhi ya watu wenye ushawishi serikalini na eneo la Mlima Kenya wanaohisi kwamba atawakilisha vyema maslahi yao akimrithi Rais Kenyatta.

Inasemekana kuwa wafanya biashara maarufu wamekuwa wakifadhili baadhi ya shughuli zake za kisiasa na kwamba wameahidi kumsaidia. Wadadisi wa siasa wanasema japo ni kawaida ya wafanyabiashara kufadhili wanasiasa wakati wa kampeni, hatua ya mabwanyenye wa Mlima Kenya kumuunga mkono Bw Mudavadi chini ya maji inazua maswali mengi.

“Sio hivyo tu, kuna minong’ono kwamba baadhi ya watu serikalini wanaunga muungano wa One Kenya Alliance (OKA) ambao Bw Mudavadi ni mmoja wa vinara,” asema mdadisi wa siasa Francis Kimeto.

Washirika wa Bw Mudavadi wanasema kwamba amejitolea kuona kuwa atapeperusha bendera ya muungano wa OKA.Jana( Jumamosi), Bw Mudavadi alikuwa mwenyeji wa vinara wenzake katika OKA eneo la Magharibi katika kile ambacho wachanganuzi wa siasa wanasema ni kuokoa umaarufu wake ambao umeshuka eneo hilo.

Duru zinasema kuwa vinara wa OKA akiwemo Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper) Moses Wetangula( Ford Kenya) na Gideon Moi (Kanu) wanapanga kuzindua kampeni zao za urais kila mmoja kivyake kabla ya kuteua mmoja wao kupeperusha bendera ya muungano huo Januari mwaka ujao.Kimeto anasema bali na kukaa ngumu, Bw Mudavadi amekataa kabisa kumuunga Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu ujao.

“Ujasiri ambao ameonyesha kuelekea 2022, ni tofauti na Musalia Mudavadi katika chaguzi za awali. Siri inaweza kuwa anatumiwa na baadhi ya watu wenye ushawishi au ameamua kuchukua msimamo mkali kivyake,” asema.

Kumekuwa na juhudi za kupatanisha vinara wa OKA na Bw Odinga ili kumshinda Dkt Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao jambo ambalo inasemakana Musalia amekataa licha ya wenzake kuonyesha dalili za kulegeza msimamo.

“Kwa kukataa kumuunga Bw Odinga ambaye kulingana na matokeo ya chaguzi zilizopita ni maarufu eneo la Magharibi kuliko yeye, huenda Mudavadi ana nia fiche iwapo hatapata tiketi ya OKA, muungano huo ukidumu hadi uchaguzi mkuu ujao,” asema mdadisi wa siasa Emmanuel Kasaki.

Anasema kuwa ujasiri wa Mudavadi unaweza kuchangiwa na idadi ya wapigakura wa jamii ya Mulembe anayoweza kutumia kupigania tiketi ya urais katika OKA au katika muungano mwingine wowote wa kisiasa.

Eneo la magharibi lina takriban kura milioni mbili na nusu kulingana na sajili ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) 2017.“Tatizo ni kwamba ameshindwa kuunganisha eneo hilo nyuma yake. Hata magavana wa eneo hilo ambao wana ushawishi mkubwa mashinani wamemuunga Bw Odinga,” asema Kasaki.

Kulingana na naibu kiongozi wa chama cha ANC, Ayub Savula, Mudavadi angali mbabe wa siasa eneo la Magharibi na ushirikiano wake na Bw Wetangula unampa nguvu zaidi.“Ukweli ambao watu wanafaa kuelewa ni kwamba eneo la Magharibi na jamii ya Mulembe liko nyuma ya Musalia Mudavadi.

Habari kwamba washindani wetu wamepenya eneo hilo ni porojo,” asema Savula.Mbunge huyo wa Lugari anasema kwamba ANC imeweka mikakati na hivi karibuni wapinzani wao watang’amua kwamba wamekuwa wakipoteza muda na nguvu kujaribu kupenya eneo la Magharibi.

Kimeto anasema hilo linawezekana ikiwa viongozi wote wa eneo la Magharibi na wafanyabiashara watamuunga mkono Bw Mudavadi.“Kwa sasa, kuna hisia kwamba yeye ni mradi wa watu fulani,” asema.

You can share this post!

Muturi atetea MCAs kuhusu digrii

Maafisa tisa Kuppet wamezea mate siasa

T L