UJASIRIAMALI: Ameunda jina kuwa bingwa wa asali ‘legit’

UJASIRIAMALI: Ameunda jina kuwa bingwa wa asali ‘legit’

Na PETER CHANGTOEK

BAADA ya kugundua kuwa kuna asali feki zinazouzwa katika maeneo mengi, hususan jijini Nairobi, aliamua kujitosa katika shughuli ya kununua na kuongeza thamani asali kwa kuongeza viungo kadhaa,na kupakia na kuwauzia wateja wake.

Joan Chemtai aliamua kuitumia fursa hiyo kuanzisha biashara hiyo, ambapo aliamua kuwapa wakulima takriban 100 kandarasi, ili wawe wakimuuzia asali ambayo haijachakatwa.

“Tunashukuru sana kwa sababu wateja wetu hufurahia bidhaa zetu. Nilianzisha biashara ya asali mnamo 2018, kwa kutumia takriban Sh2 milioni,” afichua Chemtai.

Huuzia asali katika duka lake lijulikanalo kama Nairobi Honey Shop, lililoko katika jumba la Cargen, barabara ya Harambee Avenue, mkabala wa jengo la Electricity House.

Chemtai, ambaye ana shahada katika masuala ya biashara kutoka Chuo Kikuu cha Kabarak, anasema kuwa asilimia 99 ya asali anazouza, hutoka katika Kaunti ya Baringo, alikozaliwa. Hata hivyo, hununua asali kutoka Kitui na nchini Tanzania.Anafichua kuwa asali kutoka Kaunti ya Baringo, hupatikana kwa msimu mmoja tu kwa mwaka, na hivyo, hulazimika kununua kwa wingi, hasa wakati ambapo bei huwa chini.

“Hununua asali zikiwa mbichi, halafu huchakata kutoka mwanzoni hadi mwishoni. Tunadhibiti bidhaa zetu; jambo ambalo limetuwezesha kuondoa hatari ya kuharibiwa kwazo,” asema Chemtai, ambaye ni mama wa watoto wawili.

Anadokeza kuwa, biashara yake haikuathiriwa sana na ugonjwa wa Covid-19, uliozisambaratisha biashara nyingi.

Hii ni kwa sababu wateja wengi hupenda kununua asali zilizochanganywa na viungo kama vile tangawizi na malimau, kwa ajili ya kuongeza kinga mwilini, dhidi ya virusi vya ugonjwa huo.

Ili kukabiliana na ushindani ulioko katika biashara ya asali, Chemtai anadokeza kuwa, ubora wa asali unafaa kuzingatiwa mno.

“Pia, kampuni yetu imeshirikiana na maabara ya Kirdi (Kenya Industrial Research and Development Institute), kwa ajili ya kuboresha bidhaa zetu,” asema, akiongeza kwamba, hilo limewawezesha kutengeneza bidhaa zilizo bora, ikilinganishwa na za washindani wao.

Mjasiriamali huyo anasema kwamba, kabla hajajitosa katika shughuli hiyo ya uongezaji thamani asali, alifanya utafiti kwanza, kuhusu kiasi cha fedha za kuanzisha biashara, faida na jinsi ya kupata asali.

Hata hivyo, ansema kwamba, kuna changamoto kadha wa kadha ambazo amewahi kuzipitia katika shughuli hiyo.

Mojawapo ya changamoto hizo ni barabara duni, hususan katika maeneo anakonunulia asali, ambapo kwa wakati fulani barabara zenyewe hazipitiki.

“Pia, hupata changamoto ya bei za asali, kwa sababu kuna asali feki sokoni, ambazo si ghali, na watu hupenda vitu vya bei nafuu,” aongeza Chemtai.

Mjasiriamali huyo, anafichua kwamba, wamekuwa wakichakata bidhaa zao kule Kirdi, lakini siku chache zilizopita, walipata sehemu ya kuendeshea shughuli zao katika eneo la Kitengela.

Wamekuwa wakinunua vifaa vya kupakia asali kwa bei tofauti tofauti, kutoka kwa kampuni ya Safepak.

“Bei ni tofauti, kwa kutegemea saizi. Hununua chupa za kilo moja (chupa 90) kwa Sh2,440, za gramu 500 (chupa 91) kwa Sh1,680 na za kilo moja na nusu (chupa 60) kwa Sh1,380,” aeleza Chemtai.

Mfanyabishara huyo anasema kuwa, huuza asali kilo moja kwa Sh950, gramu 500 kwa Sh500, gundinyuki (propolis) gramu 375 kwa Sh800, gramu 500 za asali ya nyuki wasio na usena (stingless bee honey) kwa Sh1,200. Aidha, huuza asali kilo tano kwa Sh6,300.

Anasema kuwa, ladha, uzito na rangi ya asali hutegemea mahali ambapo asali yenyewe imetolewa. Hii ni kwa sababu ya mimea na mbochi/nekta tofauti tofauti inayofyonzwa na nyuki.

Anawashauri wale wanaonuia kujitosa katika uuzaji wa asali kuhakikisha kuwa, wanapata asali bora na kuwa na vifaa maalumu vya kuchakatia asali.

Pia, anawahauri watambue soko kwanza na kuhakikisha kuwa wanapata asali bila kukosa.

Chemtai, amabye ana wafanyakazi watano, anasema kuwa kwa kudura za Mwenyezi Mungu, anapania kuipanua biashara hiyo, na kuwaajiri wafanyakazi wengi.

Mbali na asali, yeye pia huuza bidhaa nyinginezo, kama vile matunda yaliyokaushwa, poda ya ‘moringa’, mbegu za maboga, mbegu za ‘chia’ miongoni mwa bidhaa nyinginezo.

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Yatani asije akasahau kuwa wakazi wa...

Mseminari ndani kumiliki filamu za ngono

T L