UJASIRIAMALI: Karani anayekuza mboga za kienyeji

UJASIRIAMALI: Karani anayekuza mboga za kienyeji

NA SAMMY WAWERU

AKIWA na umri wa miaka 28, Ceciliah Wangui anaridhia shughuli ya kilimo anayoendeleza kinyume na mtazamo wa vijana wa rika lake.

Ni mjuzi katika ukuzaji wa mboga za kienyeji aina ya mnavu, maarufu kama managu.Tunampata kwenye shamba lake la kukodi eneo la Mutaratara, Kikuyu, Kaunti ya Kiambu akikagua mazao tayari kugeuzwa hela.

Anatabasamu anapotazama jitihada zake.

“Managu ni mojawapo ya mboga zenye mapato ya haraka,” Wangui asema.

Ni kilimobiashara alichoingilia miaka mitatu iliyopita, baada ya jaribio la kabichi na nyanya Kaunti ya Laikipia anakotoka, kukosa kumuendea alivyotaka.

Anafichua, kabichi alizokuwa amepanda kwenye robo tatu alirejesha mtaji pekee.

Nyanya nazo, hazikuwa mbaya vile ila anahoji zina kazi nyingi.

Anaambia Akilimali kuwa mnamo 2019, alikutana na mmoja wa washirika katika kanisa analohudhuria Kiambu, ambaye alibadili mawazo yake.

“Ni mkulima hodari wa mseto wa mboga za kienyeji, managu anazokuza kwa wingi na maelezo yake yalinishawishi nilipozuru shamba lake,” aelezea.

Kulingana na Wangui, kibarua kilikuwa kupata shamba japo hatimaye alipata thumni ya ekari. Anadokeza, ilimgharimu mtaji wa Sh16,500 kutoka kwa akiba yake.

Fedha hizo zinajumuisha kukodi shamba, mbolea, mbegu na leba, na mwezi mmoja baadaye anafichua alitia kibindoni faida zaidi ya Sh11,000.

Jaribio la hasara

Jaribio la pili, alilima managu na kunde.

Managu hata hivyo yalisombwa na maji ya mafuriko nazo kunde kuathirika kutokana na ukungu wa asubuhi na jioni, akikadiria hasara ya Sh43,000.

“Sikufa moyo, nilijikaza,” anaeleza.

Miaka mitatu baadaye, mkulima huyu ana kila sababu ya kutabasamu.

Kwa sasa, anaendeleza kilimo cha managu kwenye robo tatu. Amegawanya shamba kwa vikundi vya mita 24 kwa 6, kuhakikisha anakidhi mahitaji ya wanunuzi wake mfululizo.

Anasema kila kipande, aghalabu hakikosi kumuingizia kati ya Sh15,000 – 20,000.

“Gharama ya kuzalisha ikienda juu sana ni Sh5,000,” anakadiria.

Aidha, wanunuzi wake ni wa kijumla kutoka masoko ya Dagoretti, Kawangware na Kangemi ambao huendea mazao shambani, Wangui akisema huuza kulingana na ukubwa wa sehemu na gharama aliyotumia.

“Kipimo cha kilo kitanilazimu kupeleka mazao sokoni, na hiyo ni gharama nyingine.”

Ni gange ya ziada, akifichua kwamba ameajiriwa kama karani msimamizi katika kampuni moja jijini Nairobi.

Kilimo hicho hata hivyo hakijakuwa mteremko, akitaja mazao yanaposheheni sokoni mabroka humkandamiza.

Mkulima huyu mwenye Diploma ya Usimamizi, hupanda managu aina ya giant night shade kutoka Busia.

Robo ekari inahitaji kilo moja na nusu ya mbegu, akisema amekumbatia mfumo wa kusambaza mbegu kufanya upanzi. Ni mfumo wa kupanda mbegu bila mashimo wala mitaro kwa njia ya kurusha, zinapotua zinafunikwa kwa udongo kiasi.

“Unapunguza gharama na leba, japo unaibua kero kukabiliana na wadudu na magonjwa kwa sababu ya msongamano wa mimea,” aelezea Richard Omondi, mtaalamu.

Mdau huyo ambaye ni mwasisi wa Agri-Irrigation & Solutions Africa, anahimiza wakulima waliokumbatia mfumo huo kutumia vinyunyiziaji kuipa mimea maji.

  • Tags

You can share this post!

UFUGAJI: Bidii yake inavyomvunia utamu wa asali Makueni

Ingwe washikwa na wasiwasi kuhusu udhamini wa Betika

T L