Makala

UJASIRIAMALI: Mseto wa mboga hasa za kiasili unampa msingi muhimu maishani

May 9th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MKULIMA Lilian Nyakerario amepania kukuza aina mbalimbali za mboga, zikiwemo managu (mnavu), malenge, sukumawiki, sagaa, kanzera, kunde na terere katika eneo la Kasarani, Kaunti ya Nairobi.

Kilimo hiki, anasema kuwa amekifanya kutoka mwaka wa 2000 baada ya kujaribu kufanya kazi za vibarua vya kila sampuli ambavyo havikumfaidi kabisa.

Ukosefu wa kazi ulimpa changamoto ya kuanza kilimo ili apate riziki ya kila siku.

Hapo ndipo alipofanikiwa kupata sehemu ya shamba la ekari moja kando ya barabara ya Kasarani-Mwiki.

Bi Nyakerario mwenye umri wa miaka 37 na mzaliwa wa Kaunti ya Kisii, anasema kwamba yeye na ndugu zake walifunzwa kilimo na baba yao kutoka utotoni na kutokea hapo, shauku yake kwa mkulima ikakua na kukomaa ndani yake.

Kulingana naye, huwa anafika shambani kila siku kuvuna na kisha kuuza mavuno yake katika soko la Baba Dogo.

“Kila siku huwa ninarauka asubuhi kufanya kazi za shambani huku nikivuna mboga ambazo huwa najiuzia mwenyewe baadaye alasiri kuanzia saa tisa,” asema.

Kulingana naye, mavuno yake ya kila siku ni kati ya magunia mawili na matatu ambayo baada ya kuuza mwisho wa siku, huwa yanampa angalau Sh3,000.

“Najivunia kazi hii ya kilimo cha mboga maanake imeniajiri na kunipa riziki ya kila siku, na tena iliyo na uhakika. Hii ni tofauti sana na kazi za vibarua ambavyo havikuwa vya kutegemewa pakubwa nyakati zingine,” akaongeza Bi Nyakerario kwa kusisitiza kwamba kwa sasa anaweza kuwasomesha watoto wake watatu pamoja na kujiwezesha kutimiza mahitaji mengine ya msingi ambayo ni ya binafsi,” anasimulia.

Mboga hizi, Bi Nyakerario anasema, huwa anazinyunyizia maji mara tatu kwa wiki. Ili zinawiri vizuri zaidi, huwa anazitilia mbolea za kununuliwa dukani au hata zile za kiasili zinatotokana na kuku au mabaki mbalimbali ya vyakula vya ng’ombe.

Watu wawili

Anazidi kusema ya kuwa wakati mwingine, huwa anaajiri watu wawili wa kumsaidia kupalilia mboga zake ambapo huwa anawalipa Sh200 kila mmoja kwa siku.

Katika kila sehemu ya shamba lake dogo, huwa anavuna managu baada ya siku saba na sukumawiki kila baada ya siku tano. Kuvuna huku huwa anakufanya kwa mzunguko.

Aghalabu huwa anaanza kwa kuvuna managu almaarufu mchicha mwezi mmoja baada ya kupanda na kuvuna kwa muda wa miezi mitatu.

Baadhi ya changamoto ambazo huwa anakumbana nazo ni pamoja na ukose- fu wa maji haswa nyakati za kiangazi.

Wakati huu huwa inambidi kutumia mashine za kupiga maji ambazo ni ghali mno kutokana na ukubwa wa gharama ya mafuta.

Changamoto nyingine hutokea pale ambapo wadudu wanapovamia mboga zake.

Anaelezea ya kuwa ukosefu wa ufahamu mwingi kuhusu dawa za kutumia ili kukabiliana vilivyo na wadudu huathiri kilimo chake kwani wakati mwingine wadudu hatari huvamia mboga na asijue tiba ya haraka au dawa ya kutilia shambani.

Mwito wake ni kwa maafisa wa kilimo ambao anasema wanapaswa kuwaelimisha wakulima kuhusu jinsi ya kupigana na wadudu mbali na kuwaelezea jinsi ya kuboresha kilimo chao ili waweze kuongeza mazao yao.

Isitoshe, anawaomba watu wajue thamani ya mboga za kiasili kama hizi ambazo zina madini kwa wingi.

Hili anasema litawezesha watu kupata afya bora na kwa upande wake ataweza kupata mapato ya juu kutokana na mauzo mengi.