UJASIRIAMALI: Uraibu wa kuoka wageuka biashara

UJASIRIAMALI: Uraibu wa kuoka wageuka biashara

NA PETER CHANGTOEK

HAPPINESS Soila alijitosa katika uokaji wa keki miaka mitano iliyopita kama uraibu. Hata hivyo, uraibu huo uligeuka kuwa biashara ya kuridhisha baadaye, inyompa riziki. 

“Ninapotengeneza keki, hupata furaha sana. Nilisomea uokaji wa keki katika Valentine Cake House 2015,” asema Soila, ambaye pia alijifunza zaidi kupitia kwa kozi nyingine mwaka 2020.

Anasema kuwa, ili kuanzisha shughuli ya utengenezaji wa keki, mja anastahili kuwa na mtaji wa takribani Sh100,000 na Sh10,000 ili kuanzisha shughuli ya kutengeneza gururu.

Alivinunua vifaa vya kuokea keki vilivyomgharimu Sh18,000 na Sh24,000 mtawalia, wakati alipokuwa akianzisha shughuli hiyo, na mtaji wake wote ukamgharimu Sh100,000, pesa taslimu.

Soila, ambaye huendesha shughuli hiyo katika duka lake la Happy Bakers mjini Nyeri. Anafichua kwamba, huyanunua maziwa anayoyatumia katika shughuli hiyo kutoka kwa Jeveld Dairy katika kaunti hiyo kwa Sh60 kwa lita.

“Mimi hununua maziwa lita 15 kila siku. Mbali na maziwa, kuna baadhi ya viungo vya kuongeza kwa maziwa ambavyo hununua kutoka Nairobi,” asema.

Aidha, huuza gururu iliyotiwa ladha ya matunda mbalimbali.

“Tuna gururu iliyo na ladha ya karakara, machungwa, maembe, limau, nazi, njugu, vanila na matunda ya stroberi. Hununua stroberi kwa Sh100 angaa mara moja kwa wiki,” afichua.

Huuza gururu 250ml kwa Sh50, 500ml kwa Sh100, lita moja kwa Sh200 na lita tano kwa Sh950. “Huuza glasi moja ya 250ml kwa Sh50 na hupakia kuanzia lita moja na kwa brandi yetu,” aongeza.

Soila anafichua kwamba, huuza lita 10-15 za bidhaa hiyo kwa siku moja.

“Ukiuza lita moja, inafaa kukupa Sh1,600. Baada ya kuondoa gharama, unafaa kubaki na Sh900-Sh1,000 kwa siku,” afichua, akiongeza kuwa, gururu ya matunda aina ya ‘blueberry’ ndiyo hupendwa mno na wateja wengi.

Mbali na gururu, Soila huoka keki aina tofauti tofauti, mathalani ‘pinnacle colada’. Aidha, hutengeneza keki zilizotiwa ladha ya chokoleti, karakara, machungwa, n.k.

Anadokeza kuwa, huuza keki kwa bei kuanzia Sh2,000 na zaidi kwa kilo moja. Hata hivyo, bei hutegemea aina ya ladha ambayo keki inayo.

“Sisi huuza keki za stroberi kwa Sh2,200 kwa kilo, na zenye ladha ya matunda halisi kwa Sh3,000, za vanilla kwa Sh2,000 kwa kilo, na pinnacle colada kwa Sh2,500,” asema, akiongeza kuwa, wao pia huuza keki zenye uzani wa kilo mbili kwa Sh4,000 na zaidi, ikitegemea aina ya ladha iliyotumika wakati wa kutengeneza.

Soila anaongeza kuwa, hutengeneza keki kuambatana na oda anazozipokea kutoka kwa wateja wake. Hata hivyo, katika duka lake lililoko katika jengo la Homage mjini Nyeri, kuna keki ndogo ambazo huuzwa na gururu, ambazo wateja huzinunua na kula papo hapo, ambazo huziuza kwa Sh80 kila moja.

Yeye hutengeneza angaa keki tatu hadi tano kwa siku, ambapo huunda faida ya Sh2,000-Sh3,000 kila siku kwa keki pekee.

“Huuza Nairobi, Nakuru, Mweiga, Karatina. Hupata wateja mitandaoni – kwa Facebook, Instagram, WhatsApp na tuna wateja wanaotumwa na watu wengine,” aongeza.

Hata hivyo, anasema kwamba kuna baadhi ya changamoto ambazo amewahi kuzipitia katika biashara hiyo, kama vile kupanda kwa bei za malighafi.

“Tulikuwa tukinunua lita moja (maziwa) kwa Sh50, lakini kwa sasa, tunanunua kwa Sh60,” asema Soila.

Anaongeza kwamba, wakati wa Covid-19, hafla mbalimbali zilipopigwa marufuku, waliathirika kwa sababu hutegemea harusi na hafla nyinginezo kuuza zaidi.

Mbali na uokaji wa keki na utengenezaji wa gururu, Soila pia hutoa mafunzo kwa watu wanaotaka kuanzisha shughuli ya uokaji keki.

Amewahi kutoa mafunzo katika kaunti za Nairobi, Kitui, Narok, Nyeri, miongoni mwa nyinginezo. Hutoza Sh6,000 kwa mafunzo hayo.

  • Tags

You can share this post!

MITAMBO: Bailers za kisasa zinazotumia GPS

Muffins za karoti na zisizo na mayai

T L