UJASIRIAMALI: Wadumisha soko la maua ya waridi

UJASIRIAMALI: Wadumisha soko la maua ya waridi

NA LABAAN SHABAAN

KAMPUNI ya maua ya Red Lands Roses eneo la Ruiru Kaunti ya Kiambu imedumu kwa takriban miaka 30.

Ni maarufu nchini kwa ufanisi wa kilimo cha maua ya waridi takriban mia mbili yenye thamani ya juu.

Maua hayo ya waridi hukuzwa kwenye shamba la hekta 28 ndani ya vivungulio zaidi ya ishirini bila matumizi ya udongo.

Mfumo huu unasaidia kutumia tena maji na kuzuia kupotea kwa madini hivyo kuokoa maji kwa asilimia hamsini.

Baada ya mlipuko wa virusi vya corona Kenya mwaka wa 2020, kampuni nyingi sawa na Red Lands ziliathiriwa na kusukasuka kwa uchumi duniani.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Red Land, Roses Disha Copreaux anasema ilibidi wajali maslahi ya wafanyakazi wake kwanza kwa sababu ni njia ya msingi kuweka kampuni imara.

“Kampuni nyingi ziliwafuta kazi wafanyakazi wao baada ya anga kufungwa na biashara duniani kulemazwa. Hata sasa bado tunawajali wafanyakazi wetu baada ya vita kati ya Urusi na Ukraine,” Disha anaambia Akilimali.

Ili kufaulu katika kilimo cha maua, mkulima anahitajika kuzingatia kiwango kikubwa cha uangalifu kwa sababu maua ni zao bichi na huharibika upesi.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Red Lands Roses Disha Copreaux akibeba shada la maua shambani. PICHA | LABAAN SHABAAN

Red Lands Roses huuza mazao yake kwa wapangaji hafla na kwa nia ya kupata sarafu za mataifa ya kigeni.

“Kila mkulima wa maua ana soko lake mahususi. Soko letu linahitaji maua ya waridi ya viwango vya juu na mintarafu hii tunahakikisha kuna ubora kuanzia upanzi hadi usafirishaji kwenda sokoni. Hebu fikiria hii, ukienda sokoni kununua tufaha upate imeburuzwa, sidhani utainunua,” Disha anaongeza.

Vizuizi vya kiuchumi dhidi ya Urusi vimesababisha kampuni nyingi za maua kupoteza wateja na kuingia hasara ikizingatiwa kuwa Urusi ni soko kubwa sana la mazao mabichi kutoka Kenya. Disha anasema Red Lands Roses imesitisha mauzo Urusi na ikajipanga kusaka masoko mbadala.

“Sisi hatutegemei mteja mmoja tu na pia hatutumii madalali kwa sababu ya sera yetu kuuza moja kwa moja kwa mteja wa mwisho. Najua wengi waliathiriwa na mzozo wa Urusi-Ukraine ila kampuni yetu imefaulu kusaka masoko mengine Ulaya, Afrika, Asia na Amerika,” anaeleza.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Maua Kenya (KFC), Clement Tulezi, amethibitisha kuwa oda za maua na mimea ya mapambo kutoka Urusi na Ukraine zilisitishwa tangu Februari 2022. Urusi iliagiza mazao ya takriban Sh18 bilioni mwaka wa 2021.

“Zaidi ya asilimia 70 ya maua ya Kenya yanauzwa Ulaya nyingi yayo yakipitia mnada wa maua ya Uholanzi. Masoko mengine makubwa ni Japan, Australia na China,” Tulezi anasema.

Katika shamba la maua la Isinya Roses Kaunti ya Kajiado, angalau mashada ya maua 40,000 husafirishwa hadi soko la Urusi kila siku. Ila sasa maua haya yako katika hatari ya kunyauka yakihifadhiwa sana bila kufikishwa sokoni.

Tofauti na Red Lands Roses, kampuni hii iliwapa wafanyakazi wake likizo ya lazima ili kupoza zigo la kusuasua kwa uchumi katika operesheni zake.

Urusi iliondolewa kutoka kwenye mfumo wa malipo baina ya benki duniani maarufu SWIFT. Bila mfumo huu uwezeshwaji wa kupokea malipo hulemazwa.

“Kwa sasa vikwazo dhidi ya Urusi vimetunyima uwezo wa kuuza maua nchini humo kwa sababu ya ukosefu wa SWIFT. Awali tuliuza maua kwenda nchi nyingine kupitia Urusi, tukio lisilowezekana sasa,” Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Isinya Roses Annath Kumar anaambia Akilimali.

Ripoti ya Halmashauri ya Kitaifa Takwimu inaonyesha kuwa Kenya iliuza takriban tani laki mbili na kumi ya maua ambayo ina thamani ya Sh110 bilioni mwaka 2021.

Hii inafanya kilimo cha maua kuwa ngazi sawa kuteka sarafu za kigeni pamoja na majani chai, malipo kutoka raia walio mataifa ya kigeni na utalii.

  • Tags

You can share this post!

Wanasiasa wafufua magenge ya uhalifu

Akita kwa kilimo mseto baada ya kuacha ualimu

T L