Ujenzi wa bandari Kwale kuendelea

Ujenzi wa bandari Kwale kuendelea

NA WINNIE ATIENO

UJENZI wa bandari mpya eneo la Shimoni kaunti ya Kwale inayokadiriwa kugharimu Sh20 bilioni unaweza kuendelea bila pingamizi baada ya wawekezaji kukubaliana kuhusu masuala tata.

Hata hivyo, Halmashauri ya Bandari za Kenya nchini (KPA) imetakiwa kushughulikia masuala mengine ambayo yanahusiana na uharibifu wa mazingira.

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMA), mradi uliopendekezwa ungekuwa na athari mbaya kwa mazingira na jamii ya wavuvi wa Kwale.

Ujenzi wa bandari hiyo utabadilisha mandhari ya Kwale, hasa uchumi wa baharini. Hata hivyo, NEMA ilisema kuna athari mbaya kwa mazingira, hasa katika vivutio vya utalii ikiwemo mbuga ya kitaifa ya Kisite-Mpunguti ambayo ni kitovu cha utalii.

“Mbuga ya Kisite-Mpunguti ni ya kipekee nchini. Mbali na samaki na wanyama wengine wa baharini, ina aina mbalimbali za ndege. Shughuli ya ujenzi wa bandari yapaswa kuzingatia jambo hili na kutoathiri mazingira ya samaki na ndege hao,” ikasema ripoti hiyo.

Vile vile, kuna wasiwasi kuwa huenda turathi muhimu kama ‘Mapango ya Watumwa’ yaliyopo Shimoni yakaathiriwa na usasa utakaoingia punde bandari itakapoanza kufanya kazi.

Halmashauri ya Bandari inasema mambo hayo yanazingatiwa na yalijadiliwa na wadau wote husika.

“Washikadau waliidhinisha mradi huo wakati wa mkutano wa mwisho kati yao, KPA, NEMA na wadau wengine katika afisi ya Wasini/Mkwiro,” KPA ilisema kwenye mtandao wa kijamii.

Kwenye mkutano huo hivi majuzi, washikadau walielezwa juhudi na hatua zitakazochukuliwa kupunguza masuala tata katika Ripoti ya Tathmini ya Athari za Mazingira na Jamii iliyowasilishwa kwa NEMA mnamo Oktoba 23 mwaka jana.

Baada ya ukaguzi wa ripoti hiyo, NEMA ilipendekeza mkutano na jamii ya Wasini.

Njia mpya itatengwa kwa utunzaji wa samaki kama inavyotakikana kulingana na viwango vya kimataifa kinyume na hali ya sasa ambapo vyakula na mizigo vinashughulikiwa kwa pamoja.

Mwaka jana, NEMA iliorodhesha athari ikiwa ni pamoja na uvuvi, kilimo cha mwani, kupungua kwa mikoko, miongoni mwa mengine.

Lakini NEMA ilielezea hatua za kupunguza athari za mazingira.

Gavana wa Kwale Salim Mvurya alisema ujenzi wa bandari hiyo karibu na mpaka wa Kenya na Tanzania utapiga jeki uchumi wa eneo hilo mbali na kuwapa vijana ajira.

Hata hivyo, Bw Mvurya aliwahimiza vijana kupata ujuzi wa kiufundi ili kufaidika kutokana na nafasi za kazi ambazo zitapatikana kupitia kwa mradi huo.

You can share this post!

BBI: Karua atawezana?

‘Wazazi wetu walikuwa marafiki na ndio maana mimi na...