Maendeleo yameathiri maisha mitaa ya mabanda

Maendeleo yameathiri maisha mitaa ya mabanda

Na SAMMY KIMATU

MAELFU ya wakazi katika mitaa ya mabanda ya Mukuru iliyoko katika Kaunti ya Nairobi watafurahia matunda ya mradi wa ujenzi wa barabara ulioanzishwa mitaani.

Mradi huo uko chini ya mpango wa Ajenda Nne Kuu za serikali ya Rais Uhuru Kenyatta.

Mradi huo unalenga kuboresha maisha ya wananchi kwenye mitaa hiyo ikiwemo ujenzi wa nyumba za gharama ya chini sawia na barabara za lami.

Aidha, faida nyingine katika mradi huo ni kupatikana kwa maji mitaani baada ya serikali kupitia kwa Idara ya kutoa Huduma Jijini Nairobi (NMS) kuchimba visima vya maji ndani ya mitaa ya Mukuru.

Katika awamu ya kwanza, mradi huo umeshuhudiwa katika mitaa ya mabanda kwenye kaunti ndogo ya Embakasi Kusini, Makadara na kaunti ndogo ya Starehe.

Katika kaunti ndogo ya Starehe, mradi wa ujenzi wa barabara za lami ulizinduliwa kutoka Barabara ya Aoko kutoka kwa makao makuu ya kaunti (tarafa) kupitia mtaa wa Hazina na mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba.

Akizidua mradi huo, mkuu wa tarafa ya South B, Bw Michael Aswani Were alisema barabara ya lami inajengwa chini ya kipindi cha mwaka mmoja na inaunganisha barabara ya Aoko na barabara ya Entreprise katika Eneo la Viwanda.

“Barabara ya lami yenye urefu wa kilomita moja na nusu yenye upana wa futi 18 inaanzia kutoka kwa ofisi yangu kupitia mtaa wa mabanda wa Mukuru-Hazina kuelekea mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba. Kutoka Mukuru-Kayaba, barabara inaenda mbele na kutokea barabara ya Entreprise iliyoko kwenye Eneo la Viwanda,” Bw Were akaambia Taifa Leo.

Hata hivyo, kuna changamoto kadhaa katika mchakato mzima wa miradi hii ya maendeleo.

Picha ya awali ikionyesha mtaa wa Mukuru-Kayaba, South B, kaunti ndogo ya Starehe ambapo vibanda vilivyo pichani vilibomolewa kutoka kulia na kufikia kushoto kwenye ukuta wa shule ya msingi ya Mukuru. PICHA | SAMMY KIMATU

Kwa mfano, katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Hazina na mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba, zaidi ya familia 3,000 zilipoteza makao yao.

Bw Were alikariri kwamba wakazi hao walilazimika kuhama makwao kutafuta makao kwingineko ili kupisha mradi wa ujenzi wa barabara ya lami.

Wakazi hao walikuwa ni pamoja na waliopanga nyumba za kulala na wengine ni wale ambao vibanda vyao vilikuwa vya biashara na waliozoea kupata mkate wao wa kila siku kutokana na biashara hapo vibandani.

Miongoni mwa mijengo iliyobomolewa ni nyumba za orofa tatu na nyingine za orofa nne zilizojengwa kwa mawe.

Nyingine zilikuwa ni vibanda vya kuuza nyama, saluni, vinyozi, maduka ya kuuza dawa, vibanda vya nafaka, vilabu, vyoo vya umma, vibanda vya mboga, vituo vya kuuzia vifaa vya kielektroniki, maduka ya M-Pesa, vibanda vya kuuza vyakula na dobi miongoni mwa shughuli nyingine.

Mbali na mitaa hiyo, mitaa mingine ambayo kazi ya ujenzi wa barabara inaendelea ni pamoja na Mukuru-Lunga Lunga, Mukuru-Sinai na Mukuru-Jamaica yote ikiwa imo ndani ya kaunti ndogo ya Makadara.

Katika kaunti ndogo ya Starehe, kazi ya kuondoa vibanda na nyumba ili tingatinga lianze kuchimba barabara imeanza katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Fuata Nyayo.

Kwa mujibu wa Bw Were, kazi hiyo imepangiwa kuendelea katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Commercial na Mukuru-Mariguini.

Hata hivyo, katika mtaa wa Mariguini, Bw Were aliongeza kwamba kando na ujenzi wa barabara, mtaa huo umepangiwa kujengwa nyumba za mawe za orofa za bei nafuu.

“Japo ujenzi wa barabara katika mtaa wa Mariguini upo, serikali imeorodhesha kiasi fulani cha nyumba za orofa za mawe ambazo wenyeji watapewa na serikali walipie kodi iliyo na afueni kama njia moja ya kuboresha maisha yao,” Bw Were asema.

Katika eneobunge la Embakasi Kusini, serikali imekamilisha ujenzi wa barabara za lami, kuchimba visima vya maji, kukarabati mitaro ya kupitisha maji machafu na stima kuwakishwa barabarani na nyumbani ndani ya mtaa huo.

Katika mtaa jirani wa Mukuru-Kwa Njenga, maelfu ya wakazi walilazimika kuhama makwao baada ya serikali kubomoa nyumba zao.

Hata hivyo, hatua hiyo ilikuwa na pandashuka zake wakazi wakiandamana kupinga ubomozi huo.

Tingatinga lilibomoa nyumba za mabati pamoja na kuangusha mijengo iliyojengwa kwa mawe na za orofa kuanzia tano hadi kumi.

Tofauti na mitaa mingine ambayo wakazi walipewa muda wa kutosha wa kujibomolea kabla ya notisi ya kuhama kuisha, wao walidai hawakupewa notisi.

Kuongeza msumari moto kwenye donda sugu, ubomozi wa Mukuru-Kwa Njenga ulikinzana na mitaa mingine.

Badala ya tingatinga kubomoa vibanda kulingana na upana na urefu uliopimwa na soroveya wa serikali kupitia Halmashauri ya Ujenzi wa Barabara za Miji (KURA), ubomozi ulikuwa wa mtaa mzima.

Kufuatia tukio hilo, mashirika ya kupigania haki za binadamu, wanasiasa na makanisa walilalamikia serikali kufuatia kitendo hicho.

Baadaye, ubomozi ulisitishwa na serikali huku wakazi wakiahidiwa fidia na kuambiwa ‘watashughulikiwa’ hivi karibuni.

Kufikia jana, baadhi ya waathiriwa walionekana wakipiga kambi katika yaliyokuwa makao yao wakiwa ndani ya mahema ya karatasi za nailoni.

“Tuna matumaini makubwa kusubiri kuona ni lini serikali yetu itakapotimiza ahadi ya kututafutia makao mbadala ama kutulipa fidia,” mwathiriwa aliyeomba kutotajwa akasema.

skimatu@ke.nationmedia.com

  • Tags

You can share this post!

Ukitaka kuvuna vinono kutokana na ufugaji wa ndege, tambua...

Lusaka awarai wanasiasa Waluhya wasibuni vyama vingine

T L