Ujenzi wa daraja Starehe kucheleweshwa

Ujenzi wa daraja Starehe kucheleweshwa

Na SAMMY KIMATU

HUENDA daraja la watu kuvukia kwa miguu lililopangiwa kujengwa na serikali katika mitaa ya mabanda kaunti ndogo ya Starehe kusitishwa.

Hayo yanajiri baada ya viongozi mbalimbali kufanya mkutano na Mamlaka ya Ujenzi wa Barabara za Miji (KURA.

Awali, serikali iliweka tangazo katika vyombo vya habari ili wanakandarasi kutuma maombi ya kupewa kazi ya kujenga daraja la Kayaba/Hazina.

Mnamo mwezi Aprili mwaka huu, daraja lililokuwepo lilisombwa na maji wakati wa mafuriko huku wakazi wakibakia kuhangaika kwa kukosa mahali pa kuvukia.

Akiongea na Taifa Leo, mwakilishi wa wadi ya Landi Mawe, Bw Herman Azangu alisema mapendekozo ya viongozi yalikuwa ni daraja la Kaiyaba/Hazina isijengwa kwa sasa.

Badala yake, Bw Azangu aliongeza kwamba viongozi waliafikiana kwamba mwanakadarasi anayetengeneza barabara nne mitaani na kujenga nyumba za bei ya chini afaye kazi yote kwa pamoja.

“Badala ya serikali kutumia pesa nyingi mara mbili ni vyema kivukio cha Kayaba/Hazina kuwachwa na badala yake atakayeunda barabara mitaani humo ajenge daraja la magari na watu kwa pamoja,” Bw Azangu akasema.

Isitoshe, kulingana na tangazo la kandarasi ya ujenzi wa daraja hilo mlipa ushuru alikuwa alipe Sh24 milioni.

“Pesa hizo ni nyingi kwa daraja la watu kuvukia na miguu ilhali kutakuwa na daraja ya magari kando na daraja hilo baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara za mitaa katika ratiba ya mradi wa rais Kenyatta wa kupanua barabra mitaani sawia na kujenga nyumba za gharama ya chini,” viongozi wakasema.

Mkuu wa tarafa ya South B, Bw Michael Aswani Were alisema kandarasi ya mradi wa kujenga barabara na Nyumba umechelewa kwa mwezi moja.

Aliongeza kwamba familia zaidi ya 12,000 zitalazimika kuhama kitoka kwa nyumba zao na kutafuta pa kuhamia ili kupisha nafasi kwa kazi ya ujenzi.

Zaidi ya hayo ni kwamba mitaa mitano itaathirika na mpango huo ikiwemo wakazi wa mtaa wa mabanda wa Kayaba, Hazina, Fuata Nyayo, Mariguini na mtaa wa Commercial.

“Katika mradi huu wa rais Uhuru Kenyatta, kutajengwa nyumba zenye gharama ya chini mtaani Mariguini. Hata hivyo, barabara za lami zitajengwa katika mitaa yote tano,” Bw Were asema.

Bw Were aliwaomba wakazi kushirikiana na mwenye kandarasi wakati wote ili serikali ifikie malengo yake.

Watakaoathirika ni wapangaji waliojenga nyumba zao katika njia ya barabara pamoja na wafanyabiashara waliojenga vibanda njiani.

Mitaa yote tano itakuwa na sura mpya baada ya mtaa wa mabanda wa Kwa Reuben, Embakasi Kusini kujengwa barabara za lami, hospitali ya kisasa, visima vya maji kujengwa pamoja na stima kusambazwa mtaani.

  • Tags

You can share this post!

Reggea ilizma Ajenda Nne Kuu za Rais – Ruto

UDA ni chama cha mahasla – Ruto