HabariSiasa

Ujenzi wa mabwawa ya Sh188 bilioni wasitishwa

March 5th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imepata pigo kubwa katika mpango wake wa kujenga mabwawa 24 zaidi kote nchini baada ya bunge kuamuru kusitishwa kwa miradi hiyo hadi uchunguzi kufanya kuhusu manufaa ya miradi hiyo na wenye ardhi kulipwa fidia.

Kamati ya Bunge kuhusu Mazingira na Mali Asili ilisitisha miradi ya thamani ya Sh188 bilioni ambayo zabuni yake haijatolewa na serikali.

“Kamati hii inaamuru kusimamishwa kwa utekelezaji wa miradi yote ya ujenzi wa mabwawa na ambayo zabuni hazijatolewa hadi pale mipango ya ulipaji ridhaa ya wenye ardhi itakapokamilishwa na pesa hizo kutolewa. Serikali ipate ardhi kwanza kubla ya kuomba mikopo ya ufadhili wa miradi kama hiyo,” akasema Bw Kareke Mbuiki ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo.

“Bw Waziri Chelugui ikiwa wizara yako au afisa yoyote katika ngazi fulani ya serikali atakaidi amri hii basi itakuwa shauri yenu. Wakenya hawafai kulimbikizwa madeni kwa miradi ambayo baadaye utekelezaji wake utapingwa kortini na wakazi wanaotaka walipwe fidia kwa ardhi yao. Mtindo kama huu umekuwa ukiwavunja moyo wanakandarasi na kupelekea baadhi yao kuchoka na kutelekeza kazi,” akasema Bw Mbiuki, Mbunge wa Maara.

Waziri Simon Chelugui alikuwa amefika mbele ya Kamati hiyo kuwatolea ufafanuzi kuhusu hali ya ujenzi wa mabwawa kote nchini.

Wakati huo huo, kamati iliamuru Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuchunguza miradi ya ujenzi wa mabwawa yanayotelekezwa kupitia mfumo wa Engineering, Procurement, Construction na Financing (EPCF) akisema mfumo huo umekuwa ukifumiwa kuiba pesa za umma.

Ujenzi wa bwawa la Itare katika kaunti ya Nakuru ulitelekezwa kwa mfumo huo. Mradi huo ambao ulianzishwa mnamo mwaka wa 2015 unatarajiwa kugharimu Sh28.9 bilioni na utawezesha maeneo ya Molo, Nyoro, Elburgon na Nakuru kupata maji ya kutosha.

Kamati hiyo pia ilipiga marufuku mtindo wa serikali kulipa mabilioni ya fedha kama malipo ya awali kwa wanakandarasi na kutotenga pesa zozote kwa ulipaji ridhaa kwa watu ambao ardhi yao ilitwaliwa kwa mradi huo.

Miradi ya ujenzi wa mabwawa iliyositishwa ni pamoja na Kamumu, Rupingazi, Thambara, Kithino, Maara, Thingithu, Kahurura, Pesi, Kinja, Wimyumiririe, Karemeno na Londiani.

Miradi mingine ni; Maragyua IV, Bute, Bosto, Gatei, Keben, Lessos, Isiolo, Ndarugi Two, Mwache, Kiandogoro/Chania, Soin/Koru na Kabasi iliyoko katika Kaunti ya Nakuru.

Waziri Chelugui aliungama kuwa suala la ulipaji fidia kwa ardhi iliyotwaliwa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa umekuwa tatizo kubwa. Alisema mchakato huo umeingiliwa na matapeli.

“Kujivuta kwa ulipaji ridhaa kwa ardhi zilizotwaliwa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa kumekuwa sababu mojawapo ya kucheleweshwa kwa ukamilishaji wa miradi hiyo,” akasema.