Ujenzi wa Uhuru Park wasimamishwa

Ujenzi wa Uhuru Park wasimamishwa

Na RICHARD MUNGUTI

UJENZI unaondelea katika bustani ya Uhuru Park umesimamishwa na mahakama kuu mara moja.

Kusitishwa kwa ujenzi huu ni pigo kubwa kwa Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) ambao muda wake utakamilika Machi 2022. Korti ilisimamisha ukataji miti na kubomolewa kwa jukwaa ambapo viongozi na wananchi hukaa wakati wa sherehe za kitaifa

Mradi huu wa kujenga upya bustani hii ni miongoni mwa miradi mikuu ambayo NMS imefanya tangu izinduliwe na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Feburuary 15 2019. Agizo la kusimamisha ujenzi huo ilitolewa na Jaji Edward Waboto katika Mahakama kuu Malimani.

Jaji Wabwoto aliwaamuru NMS , wenye kutekeleza kandarasi hiyo na maajenti wao wakome mara moja kuendelea na ujenzi huo hadi kesi iliyoshtakiwa na chama cha kisiasa cha Communist Party of Kenya (PCK) isikizwe na kuamuliwa.

Katika uamuzi wake , Jaji Wabwoto alisema ujenzi huo wa bustani ya Uhuru Park ulianza kufanywa bila idhini ya Mamlaka ya Kitaifa ya Kuthibiti Mazingira (NEMA). “NEMA iliyounga mkono kesi hiyo iliyoshtakiwa na PCK imekiri haikutayarisha ripoti kuhusu athari za mradi huu wa ujenzi wa bustani ya Uhuru Park kwa mazingira na kwa jamii.

Hakuna leseni iliyotolewa kuhusu mradi huu na NEMA,”alisema Jaji Wabwoto. Alisema sheria za NEMA zasema kabla mradi kama huu kuanzishwa lazima ripoti zitolewe kuhusu athari zake kwa mazingira na jamii. “Ushahidi uliowasilishwa mbele yangu ni kwamba sheria nambari 28 na 59 za NEMA zimekiukwa na pia Kifungu nambari 69 (1) cha Katiba kuhusu uthibiti wa mazingira na Serikali,”Jaji Wabwoto alisema akisitisha ujenzi huo wa bustani ya Uhuru Park.

Katika kesi iliyowasilishwa na Rais wa Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) Nelson Havi ,CPK kinasema mamilioni ya pesa za walipa ushuru zinatumiwa kimakosa na NMS. Pia kimesema miti iliyopandwa miaka mingi iliyopita imekatwa na NMS inayoendelea na ujenzi huo.

Mbali na kukata miti CPK kimesema jukwaa iliyojengwa miongo mingi iliyopita imebomolewa. CPK kinasema kuwa bustani hiyo imeborongwa na sasa hakuna mahala wanananchi wanaweza kupumzika. Mahakama imeeleza sheria haikuzingatiwa kwa vile wananchi hawakuulizwa maoni yao kabla ya ubomoaji wa minara katika bustani hiyo kuanza kutekelezwa.

“Bunge la kaunti ya Nairobi ilijadili alasiri moja kwamba bustani ya Uhuru Park ijengwe upya. Wananchi hawakuulizwa maoni yao,” Bw Havi anasema katika kesi hiyo. Chama hiki cha kisiasa kimedokeza katika kesi hiyo kwamba NMS ilianza ujenzi upya wa bustani hii ya Uhuru Park kwa njia ya siri na kupeleka maafisa wa kijeshi kulinda bustani hiyo.

CPK kinasema katika kesi iliyowasilishwa katika idara ya mazingira kwamba bustani hii ya tangu jadi imebolewa na kuepelekea wakazi wa Nairobi kukosa mahala pa kustarehe pamoja na familia zao. CPK kimesema baadhi ya makanisa yamekuwa yakifanya mikutano yao ya maombi katika bustani hii.

“Ni sheria kwamba kabla ya mradi utakaogharamiwa na pesa za umma maoni ya umma yashirikishwe. Kabla ya ujenzi wa bustani ya Uhuru Park kuanzishwa maoni ya wananchi hayakusakwa. Mradi huu unaendelea kinyume cha sheria,” asema Bw Havi katika kesi anayoratibisha kuwa ya dharura.

Chama hiki chaomba mahakama isitishe ujenzi huo kwa vile hakuidhinishwa kwa mujibu wa sheria. CPK kimewashtaki NMS, Mkurugenzi Mkuu wa NMS Meja Generali Mohamed Badi , Kaunti ya Nairobi, Mwanasheria Mkuu na Mamlaka ya Kitaifa ya Mazingira (NEMA).

You can share this post!

Everton yazamisha chombo cha Arsenal katika EPL ugani...

Ujanja mpya wa kampeni za Raila, Ruto

T L