Makala

UJUZI NA MAARIFA: Mradi wa biogesi ulivyopunguza gharama ya upishi shuleni Simoti

August 8th, 2019 3 min read

Na RICHARD MAOSI

ARDHI iliyosheheni rutuba ndiyo mandhari yaliyotukaribisha katika Kaunti ya Bomet, inayopatikana takribani kilomita 22 kutoka mjini Kericho.

Ingawa wakazi wengi hapa ni wakulima wa mifugo na mimea, baadhi yao wamejiongezea ujuzi katika nyanja zingine mbali na kilimo.

Wanafunzi wakionekana kutilia maanani suala la ukulima katika hatua ya kuongeza nafasi za ajira siku za usoni ili waje kuwa watu wa maana na wa kujitegemea.

Karne ya 21 uvumbuzi wa kisasa umekuja na faida nyingi kuliko hasara, wakulima na wajasiriamali wamefanikiwa kupiga hatua kubwa baada ya muda mfupi.

Mojawapo iliyovutia Akilimali ni Shule ya Upili ya Simoti, eneo la Bomet, jinsi walivyojibunia mradi wa kuzalisha bayogesi inayotumika kukidhi mahitaji ya wanafunzi 715 kwa mwaka.

Ni bayana kuwa mradi wa kuzalisha bayogesi umesaidia kukata gharama ya kununua gesi kutoka kwenye viwanda, kwa bei ghali ya Sh1,000 kwa kila mtungi wa kilo sita.

Kulingana na mwalimu mkuu Bw Charles Koech, anasema hii ilikuwa ni njia mojawapo ya kusaidia shule ipate sehemu mwafaka ya kutupa samadi inayotokana na ng’ombe wawili wanaofugwa shuleni.

Vilevile, Bw Koech alieleza kuwa mradi wa kuzalisha bayogesi kutokana na samadi, ungesaidia kutunza mazingira na kupunguza uwezekano wa kukata miti kiholela kwa sababu ya kutafuta kuni.

“Wakazi wengi wa mashambani wanatumia kuni katika shughuli za kupikia, lakini tumejizatiti na kugundua njia mbadala na bora kuliko ile iliyozoeleka,” akasema.

Gharama yake ni nafuu kwa sababu mkulima atahitaji samadi, paipu za kuunganisha mkondo wa gesi na nguvu kazi ya kuangalia mradi wenyewe katika kila hatua kabla ya biogesi kuwa tayari kwa matumizi.

Mradi wenyewe ulianzishwa 2018 na shule ya Simoti ilitegemea kununua samadi kutoka kwa wakulima wadogo wanaowazunguka kabla ya kujipatia mifugo wao.

Kwa siku 365 shule ya Simoti haijakuwa ikinunua gesi kwa sababu wenyewe wamefanikiwa kuzalisha kiwango kinachoweza kutosheleza mahitaji ya kila siku ambayo ni kupikia na kwenye maabara.

Bw Koech anasema shule inajipanga kuanzisha jikoni ya kisasa mwaka huu ili kuongeza jumla ya gesi inayozalishwa, iweze kutumika kuwapikia wanafunzi na kuwachemshia maji ya kuoga.

Mradi wenyewe unajumuisha usimamizi wa shule na wanafunzi ambapo kila mmoja amepatiwa jukumu la kutenda huku, wanafunzi wakionekana kuwa katika mstari wa mbele.

Mradi unatazamiwa kusaidia shule kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja na kuzuia matatizo kama vile moshi wa kuni onaoweza kuwaletea wanafunzi madhara ya kukohoa na maradhi ya pumu.

“Ukiwa na nishati hii hauna haja ya kukata miti na mazingira yataishia kuwa salama zaidi ikizingatiwa kuwa watu watakuwa wakitegemea biogesi,” mwalimu huyo mkuu aliongezea.

Matumizi ya mtambo

Wanafunzi wa Shule ya Simoti wanatumia mtambo wa kawaida ambao ni tandarua, samadi, maji na beseni, lakini hili halifuti dhana kuwa wanapata nishati ya kutosha.

Mwalimu Koech aliongezea kuwa mkulima atahitaji takribani ng’ombe wawili kulisha muundo wake kwa samadi ya kutosha ambayo ni takriban kilo nne kila siku.

Aidha, mtayarishaji atahitajika kuupatia muundo wake muda baada ya kujenga ili upate kukomaa, na kisha kumwagilia samadi kwa siku hamsini mtawalia bila kuutumia.

Hii itatoa nafasi kwa bakteria wanaopatikana ndani ya samadi kupata muda mwafaka wa kuzaana na kuchakachua samadi iliyoingia kabla ya kutoa pumzi hafifu za gesi na hatimaye bayogesi.

“Kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu, mtumiaji hapaswi kutumia mtambo wake chini ya siku 45 kwa sababu bado gesi iliyozalishwa huwa haijatosha kuzalisha nishati,” alisema.

Teknolojia rahisi

Kwa mujibu wa mwalimu wa somo la zaraa Bw Dennis Osano anasema uzalishaji wa nishati ya bayogesi unahitaji teknolojia rahisi ambapo mkulima atasaka sehemu ya kuhifadhi samadi.

Mtayarishaji anaweza kutumia tanki kubwa au beseni ambapo samadi huchakachuliwa na bakteria wanaozaana kutokana na viini vya mamilioni ya bakteria wanaoongezeka.

Baada ya muda mfupi wa siku tano hivi matokeo yake huwa ni gesi pamoja na mbolea hai inayoweza kukuza mimea, katika shamba bila kutegemea zile za viwanda zenya madini ya phosphorus na ammonia.

 

Mwalimu Japheth Manyara akiwaelekeza wanafunzi wake wakati wa kulisha mtambo wa kuzalisha biogesi. Picha/ Richard Maosi

Uzalishaji wa nishati ya kawi unahitaji sehemu tatu ambapo moja ni ya kumwaga samadi, pili ni sehemu ya kufanyia mchanganyiko wa maji na samadi na hatimaye chujio ya kuhakikisha gesi inayotolewa ni safi kwa matumizi.

Wanafunzi walitumia tandarua nyeusi, ili kufanikisha hali endelevu ya kuzalisha nishati rahisi, kwanza ili kuimarisha joto katika muundo huu unaovuta miale ya jua kwa asilimia kubwa na kuharakisha uzalishaji wa kawi.

Uzalishaji wa nishati yenyewe unategemea kujaza samadi na kutoa fursa mwafaka ya kuchakachua samadi kabla ya kuzalisha kawi ambayo haiishi kwa haraka kama aina nyingine za gesi zinazoweza kukatika njiani.

Osano anasema baada ya samadi kuchujwa inaweza kuruhusiwa kutoka nje ya muundo huu, na endapo itakingwa na kuhifadhiwa vizuri inaweza kutumika shambani kukuza mimea na ubora wake ni wa hali ya juu sana.

“Cha msingi ni kwa mkulima kuhakikisha analisha mtambo kwa samadi ya kutosha ili kupata gesi ya kutosha bila kukoma, ng’ombe wawili hivi wanatosha kufanikisha hili,” akasema.

Aliongezea kuwa ni muhimu mkulima kuhakikisha anatumia lishe sahihi ili kuhakikisha wanatoa samadi yenye ubora wa kipekee.

Samadi ya ubora wa kipekee inahitajika kuwa na mchanganyiko wa lishe ya nyasi za rangi ya kijani kibichi, lishe za viwandani na maji ya kutosha. Pia mkulima afanye juhudi kuwazuia mifugo wake wasile vitu vigumu kama mawe na karatasi zinazoshusha hadhi ya samadi.