Makala

UJUZI NA MAARIFA: Mwalimu aliyefaulu kufuga nyuki katika makazi anamoishi

June 6th, 2019 2 min read

Na DUNCAN MWERE

SI wengi wana ujasiri na ukakamavu wa kufuga nyuki kutokana na dhana na kasumba ni wadudu hatari kufuga licha ya kuwa na manufaa tele.

Ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni.

Katika mpaka wa kaunti za Kirinyaga na Nyeri utakutana na mtaalamu gwiji wa kufuga nyuki.

Wafugaji wengine hufuga nyuki mbali na maskani ya binadamu na mahali palipo na miti na utulivu.

Lakini mambo ni tofauti katika kitongoji cha Thunguri mjini Kiangai eneobunge la Ndia, Kirinyaga ambapo mkulima anafuga nyuki katika makao anamoishi na aila yake.

Nyamu Kahiu ni galacha na mwalimu ambaye amefundisha wengi kuhusu mbinu za kutunza, kufuga na kurina asali kwa muda wa mwongo sasa.

Mfugaji na mtaalamu wa masuala ya kufuga, kutunza na kurina asali Nyamu Kahiu akionyesha baadhi ya mizinga katika eneo la Thunguri mjini Kiangai, Ndia, Kaunti ya Kirinyaga. Picha/ Duncan Mwere

Akilimali ilimtembelea katika boma lake na kumpata Njuki Nene (Nyuki mkubwa) anavyofahamika na wengi akiendelea na shughuli za kutunza nyuki wake.

Katika boma lake Nyamu, 58, anajivunia kuwa na mizinga 67 ambayo humwezesha kukidhi matilaba yake ya kila siku licha ya kuwekeza katika nyanja tofauti.

Alianza kufuga nyuki baada ya kukosa kibarua mara kwa mara.

“Mara nyingi ungeamka na kusaka ajira lakini ujira ulikuwa wa chini mno au ukose katu,” aeleza.

Mara nyingi ni wakati aliambulia patupu. Ufugaji wa nyuki hauna mahitaji mengine ikilinganishwa na ukulima mwingine wowote.

Cha msingi ni mfugaji kuwa na mizinga ya kisasa.

Awali, Nyamu alikuwa akitumia mizinga ya zamani ambayo anasadiki mfugaji hakuweza kurina asali nyingi ikilinganishwa na ya kisasa. Mizinga anayopendekeza ni Langstroth na Kenya Top Bar Hive katika janibu za Mlima Kenya.

Pili, mavazi maalumu ambayo aghalabu hutumika wakati wa kurina asali.

Hii humfaa mrinaji kwani wadudu wanaweza kumshambulia na kusababisha mauti.

Hitaji jingine ni kifaa cha moshi almaarufu Smoker ambacho hufanya nyuki kupoteza fahamu na kuzubaa. Kwa jumla vifaa hivi hugharimu takriban Sh6,000.

Nyamu anaeleza kuwa kando na asali, mkulima anaweza kunufaika na bidhaa nyingine kutokana na nyuki.

Japo asali ni bora kwa watu wa umri wote, matabibu wanapendekeza ni bora zaidi hasaa kwa watoto wachanga.

Hii huwapa uwezo wa kuhimili magonjwa mathalani kikohozi ambacho aghalabu huwapata mara kwa mara.

Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya afya ni kuwa yeyote aliyeng’atwa na nyuki anapata kinga kwa asilimia kubwa ya kukabiliana na maradhi hatari kama vile saratani.

Wataalamu wa kilimo wanaeleza ufugaji wa nyuki ni kati ya kazi isiyokabiliwa na changamoto nyingi. Wezi wanaovamia mizinga hususan wakati wa jioni na kuvuna ni kati ya changamoto inayowakabili wafugaji hasa walio mbali na eneo la kufugia.

Fauka ya hayo kuna wadudu wapendao kula asali kama vile ngedere, siafu na sisimizi. Nyamu anadokeza hivi ni visiki ambavyo mfugaji anaweza kuepuka.

“Wataalamu wamezuka na mbinu ambazo zitawezesha kuvuna asali na kufurahia kazi zao lakini nashauri wakulima wawe wanahudhuria warsha na makongamano kila wakati,” ahimiza.

Soko la bidhaa za nyuki huwa tayari kila wakati.

Uchache

Hii ni kutokana na uchache wake na manufaa yake kila wakati. Wateja wake wako kila pembe ya nchi mathalan Nyeri, Nakuru, Nairobi na Embu.

Wanakijiji waliopinga jitihada zake sasa hufika kwake kila mara kununua asali na kupata mwongozo wa kufuga nyuki.

Nyamu hurina asali aghalabu mara mbili kwa mwaka.

Kutoka kwa mizinga yake 67 anaweza kupata zaidi ya Sh500,000 na zaidi kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Hii imewezesha kuanzisha miradi na kuelimisha wanawe wanne.

Kwa sasa Nyamu amechaguliwa mwenyekiti wa kikundi cha wafugaji nyuki cha Kiangai Adults Leaners bee-keeping.

Aidha ni mmiliki wa kampuni ya Nyaka Bee-keeping.