Ukabila sumu ya chama cha Pwani

Ukabila sumu ya chama cha Pwani

MAUREEN ONGALA na VALENTINE OBARA

NDOTO ya tangu jadi ya ukanda wa Pwani kuwa na chama kimoja au muungano wa kieneo huenda ikasalia kuwa ndoto daima dahari iwapo vizingiti viwili vikuu havitaondolewa.

Mipango na mikakati ya kuunda ‘chama cha Wapwani’ ambayo imekuwapo kwa miaka na vikaka imekuwa ikiambulia patupu kila mara.

Hata hivyo, imefichuka kuwa kizingiti kikuu katika kufanikisha ndoto hiyo ni ukabila baina ya wanasiasa wanaojiona kuwa Wamijikenda na wale wanaochukuliwa kuwa ‘chotara’, pamoja na ubabe wa kisiasa ambapo kila kigogo anataka awe ndiye anakaa kileleni.

Sababu kuu zilizoleta vikwazo kwa juhudi za baadhi ya wanasiasa kubuni chama kimoja cha Pwani kitakachotumiwa mwaka wa 2022, zimeanza kufichuka.

Kwa mujibu wa wanasiasa wa eneo hili, juhudi hizo ambazo zilishika kasi mapema mwaka 2021 zilianza kufifia ilipobainika kuwa kuna baadhi ya viongozi walioweka mbele masilahi ya kikabila, huku wengine wakiwa na maazimio ya kutumia juhudi hizo kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

Imebainika kuwa, ukabila ni mojawapo ya sababu ambazo zilisababisha mgawanyiko kati ya viongozi waliotaka kigogo atakayechaguliwa kuongoza chama hicho kipya awe Mmijikenda, na wale walio na mtazamo kuwa Pwani ina mchanganyiko mkubwa wa makabila ambapo mengine hayafai kubaguliwa.

Mahojiano ambayo Taifa Jumapili ilifanyia baadhi ya viongozi wa kisiasa na wa kijamii wanaofahamu kuhusu mazungumzo ya kutafuta chama kimoja cha Pwani yalibainisha kuwa kikundi hicho cha kwanza kilikuwa kikipendekeza Gavana wa Kilifi Amason Kingi au mwenzake wa Kwale, Bw Salim Mvura ndiye awe msemaji wa kisiasa Pwani.

Magavana hao wawili pamoja na mwenzao wa Mombasa, Bw Hassan Joho wanatumikia kipindi cha pili cha uongozi na wote wanaelekeza macho yao kwa siasa za kitaifa mwaka ujao.

Hii inamaanisha kuwa, mmoja wao tu ndiye aliye na nafasi nzuri kupewa mamlaka ya kushauriana na serikali kuu au wanasiasa wanaopanga kuwania urais 2022 kuhusu mahitaji ya Wapwani, na hata pengine achaguliwe kuwa mgombea mwenza au apewe wadhifa mwingine mkubwa katika serikali ijayo.

Mshirikishi wa muungano wa wazee wa Kaya eneo la Pwani, Bw Tsuma Nzai asema lilikuwa pendekezo la wazee kwamba kinara wa chama kitakachobuniwa awe ni Mmijikenda lakini wazo hilo likachukuliwa vibaya na wanasiasa wengine.

Alilaumu wanasiasa wanaopinga pendekezo hilo kwa kurudisha nyuma juhudi za kuleta umoja wa Pwani.

“Ikiwa sisi tunapigania kuwa na kinara wa Pwani ambaye atakuwa Mmijikenda ilhali Gavana Kingi akiongea, kuna viongozi na wanasiasa wetu wanaompinga na kumpura mawe, ni dhahiri kuwa wao ndio wenye matatizo na wanarudisha safari yetu nyuma kila kukicha,” akasema.

Hii ni licha ya kuwa Bw Kingi amekuwa akisema mipango ya kubuni chama hicho si kwa minajili ya kumwinua yeye binafsi bali kupata nafasi bora ya kutetea masilahi ya Wapwani katika siasa za kitaifa.

Hivi majuzi, Bw Joho ambaye tayari aliwasilisha ombi kwa Chama cha ODM kutaka kupigania tikiti ya kuwania urais 2022, alikashifu siasa za kikabila Pwani.

Alipokuwa akihutubu wakati wa kuzindua kituo maalumu cha matibabu ya moyo katika Hospitali Kuu ya Rufaa ya Pwani, Bw Joho alisisitiza kuwa Pwani hujivunia umoja wa makabila mengi na haifai mtu yeyote kuanza kuingiza ukabila.

“Nasikia wengine wakisema mambo ya ukabila. Hapa Mombasa hatutaki ukabila. Tunataka nchi nzima ijifunze kutoka kwetu kuhusu jinsi tunaweza kuinuana kimaisha kwa ushirikiano bila kujali misingi ya kikabila,” akasema.

Kando na haya, imebainika kuwa suala jingine ambalo limetatiza uundaji wa chama cha Pwani ni ubabe wa viongozi wa kisiasa.

Kwa mujibu wa wanasiasa eneo hilo, kulikuwa na mivutano tele hasa kuhusu malengo makuu ya chama ambacho kingeundwa.

Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, alidai kuwa mvutano mkubwa ulisababishwa na malengo kati ya viongozi wanaopanga kuingia kwa siasa za kitaifa, na wale ambao bado wanatarajia kuwania viti vya mashinani kama vile ubunge, useneta, udiwani na ugavana.

Kulingana naye, viongozi wanaolenga mamlaka katika serikali kuu 2022 walijali sana mashauriano yanayohusu nafasi watakazopata katika serikali ijayo, ilhali wale watakaoendelea kuwania viti vya mashinani walijali jinsi watakavyoshawishi wananchi kuwapigia kura.

Akizungumza katika mahojiano ya redio, Bi Jumwa alisema kwamba kikundi hicho cha pili cha wanasiasa ndicho kilitaka kuwe na chama kitakachotoa kipaumbele kwa majadiliano kuhusu masuala yanayohusu mwananchi moja kwa moja kama vile ugavi wa rasilimali za serikali ya kitaifa.

“Tunachoona kwa sasa ni kuwa hakuna nia. Wale viongozi, hasa magavana wanataka kuzungumza kuhusu Pwani ila wanachowazia ni hatima yao baada ya 2022. Huwa tunazungumza kwa sauti moja tukiwapangia nafasi zao zitakavyokuwa baada ya 2022, lakini hawataki kuongelea kile ambacho mwananchi atafanyiwa. Hapo ndipo tofauti inakuja baina yetu,” akaeleza.

Mbunge wa Magarini, Bw William Kingi alitoa kauli sawa na hii, akiongeza kuwa changamoto nyingine iliyotatiza uundaji wa chama cha Pwani ni jinsi juhudi hizo zilivyoingiliwa na vigogo wa kisiasa wanaotoka nje ya Pwani.

Kwa miaka mingi, eneo hilo limekuwa miongoni mwa yale yanayovutia wagombeaji wa urais lakini huwa laegemea sana upande wa upinzani.

Huku akieleza matumaini yake kuwa chama hicho hatimaye kitabuniwa kabla 2022 na akitumie kuwania ugavana Kilifi, mbunge huyo alisema kuna wanasiasa wa kitaifa ambao wanajua watakuwa hatarini kupoteza kura za urais endapo Wapwani wataamua kusimama kwa umoja jinsi inavyofanyika katika maeneo mengine kama vile Nyanza na eneo la Kati.

Imesemekana kuwa, baadhi ya wanasiasa bado wanalazimika kuwa waaminifu kwa viongozi wa vyama walivyotumia kuingia mamlakani 2017, au vyama ambavyo walihamia tangu wakati huo.

“Ninajua kuna vita vikali dhidi ya wabunge wa Pwani ambao wangali wanaendeleza juhudi za kuunda chama cha Pwani, lakini tutasimama imara. Mazungumzo bado yanaendelea na ifikapo 2022, eneo la Pwani litakuwa na chama chake. Kumekuwa na changamoto kuleta umoja wa eneo hili kwa sababu baadhi ya wanasiasa ni wabinafsi wanaotaka kulinda maslahi yao ya kisiasa,” akasema.

Vyama vinne vya Pwani ambavyo vilitambuliwa ili viongozi wao washauriane kuunda muungano au chama kimoja cha Pwani ni Kadu-Asili, Umoja Summit, Shirikisho na Republican Congress Party.

Hii si mara ya kwanza ambapo viongozi wa Pwani wanashindwa kuungana kisiasa.

Katika mwaka wa 2016, Waziri wa Ugatuzi Gideon Mung’aro ambaye wakati huo alikuwa Mbunge wa Kilifi Kaskazini, aliongoza kupitishwa kwa Azimio la Dabaso lililoleta pamoja baadhi ya viongozi wa Pwani ambao walisisitiza wito wa kuunda chama kimoja cha Pwani.

You can share this post!

CHOCHEO: Siri ya mapenzi yenye raha na yanayodumu

Tuonane kwenye debe la urais 2022 – Muturi