Ukambani nao wafuata minofu Ikulu

Ukambani nao wafuata minofu Ikulu

Na KITAVI MUTUA

RAIS Uhuru Kenyatta atapeleka minofu ya serikali Ukambani, katika juhudi za kutuliza malalamiko kuwa ametenga eneo hilo kimaendeleo.

Ziara hiyo ya kiongozi wa nchi itakayofanyika Juni 28 na Juni 29, ilipangwa Jumatatu kwenye mkutano kati yake na viongozi wa eneo la Ukambani, wakiongozwa na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka katika Ikulu ya Nairobi.

Magavana, maseneta, wabunge na madiwani kutoka kaunti za Kitui, Machakos na Makueni walitumiwa mwaliko wa kwenda Ikulu mnamo Jumapili usiku, siku mbili tu baada ya magavana Charity Ngilu (Kitui) na Alfred Mutua (Machakos) kudai kuwa eneo la Ukambani limepuuzwa kimaendeleo, licha ya kuunga mkono handisheki.

Mwaliko huo kwa viongozi ulitumwa baada ya Rais Kenyatta kuwapigia simu Bw Kalonzo, Bi Ngilu na Bw Mutua mnamo Jumapili, ambapo aliwaambia angetaka kukutana na viongozi wa Ukambani jana ili kusikiza matakwa yao.

Katika ziara yake Ukambani, Rais Kenyatta amepangiwa kukagua mradi wa Bwawa la Thwake, ujenzi wa mji wa kiteknolojia wa Konza kabla ya kufululiza hadi Kaunti ya Kitui kufungua kiwanda cha nguo cha Kicotec.

Rais Kenyatta pia atazuru kiwanda cha kutengeneza mawe na kokoto ya ujenzi katika Kaunti ya Kitui.

“Eneo la Ukambani lina zaidi ya watu milioni tano na hatufai kuachwa nyuma katika meza ya kugawana rasilimali,” Gavana Ngilu aliambia Taifa Leo.

Mnamo Ijumaa, wakati wa hafla ya mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Kibwezi Kalembe Ndile, yaliyohudhuriwa na kinara wa ODM Raila Odinga katika Kaunti ya Makueni, Bi Ngilu na Dkt Mutua walilalama kuwa eneo la Ukambani limepuuzwa kimaendeleo, na kuwa hawakutengewa mradi wowote katika bajeti iliyosomwa wiki iliyopita.

“Bajeti ya mwaka ujao tumepewa nini? Hakuna chochote cha kujivunia licha ya kuunga mkono handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga,” akasema Bi Ngilu.

Gavana Mutua alisema serikali za kaunti zinahangaika kutekeleza hata miradi midogo na kulipa mishahara, kwa sababu ya kutopewa fedha kutoka kwa Hazina Kuu ya Kitaifa.

“Tunapozungumza sasa, wafanyakazi wa Kitui, Machakos na Makueni hawajalipwa mishahara yao kwa sababu hatuna fedha,” akasema Gavana Mutua.

Bw Musyoka, hata hivyo, alitofautiana nao akisema kuwa wanafaa kutumia pesa ambazo serikali za kaunti zinapata kutoka kwa serikali ya kitaifa kutekeleza miradi ya maendeleo.

Kiongozi huyo wa Wiper alishutumu magavana kwa kushindwa kukabiliana na mafisadi, ambao wamekuwa wakiiba fedha zinazofaa kutumiwa katika miradi ya maendeleo.

Katika eneo la Luo Nyanza, Rais Kenyatta alizindua mradi wa Sh3.8 bilioni wa ukarabati wa reli ya kati ya Nakuru na Kisumu, ukarabati wa bandari ya Kisumu wa Sh3 bilioni, kituo cha kisasa cha kibiashara cha Uhuru (sh350 milioni), Kituo cha Makontena cha Kibos na mradi wa umeme kati ya mingineyo.

Jana, Rais Kenyatta aliwahakikishia viongozi wa Ukambani kuwa serikali yake itapeleka miradi ya maendeleo katika maeneo yote ya nchi.

Rais Kenyatta alionya wanasiasa dhidi ya kupiga siasa kila mara badala ya kushughulikia miradi ya maendeleo.

“Nimeamua kuelekeza juhudi zangu katika masuala ya maendeleo na wala si ajenda za kisiasa,” akasema Rais Kenyatta.

Miradi mingine ambayo wanataka Rais Kenyatta kuipa kipaumbele ni maji na barabara.

Miongoni mwa miradi hiyo ni utengenezaji wa barabara inayounganisha kaunti za Kitui na Makueni na nyingine inayounganisha Kitui na Kaunti ya Tana River.

Viongozi hao pia wanataka kufufuliwa kwa mradi wa uchimbaji wa makaa ya mawe na mradi wa kilimo wa Wikithuki, Mwingi.

You can share this post!

Uhispania na Uswidi waumiza nyasi bure kwenye kipute cha...

Leicester City kuvunja benki ili kumsajili Coutinho kutoka...